Habari za Punde

RC Kusini Pemba azindua mfuko maalum wa harambee ya uchangiaji wa ujenzi wa skuli ya Mtambile

Na Salmin Juma, Pemba


Wanajamii wa Mtambile mkoa wa kusini Pemba wametakiwa kuachana na utegemezi wa kutegemea wafadhili kutoka nje na badala yake kujitokeza kwa wingi kuchangia katika ujenzi wa skuli ya ghorofa inayotarajiwa kujengwa muda wowote kutoka sasa.


Kauli hiyo imetolewa leo na Mkuu wa mkoa wa kusini Pemba Mh, Hemed Suleiman  wakati  alipokua akizindua mfuko  maalum  wa harambee ya uchangiaji wa ujenzi wa skuli  ya Mtambile uliofanyika skulini  hapo.

Mh, Hemed amesema iwapo wana mtambile watakuwa mstari wa mbele katika kutoa michango yao basi uwongozi wa mkoa wa kusini Pemba upo tayari kushirikiana nao bega kwa bega kufanikisha ujezi huo ili   kuwapatia wanafunzi mazingira bora na rafiki kwa masomo na kuondokana na usumbufu unao wakabili hivisasa ikiwa ni pamoja na  uhaba wa madarasa ya kusomea na uchakavu  wa mabanda yenyewe hali ambayo inawafanya wasome katika mazingira magumu.

”Wana Mtambile lazima tubadilike tuache matumizi yasiyo ya lazima, kama kufanya maholi na mialiko ya machai katika maharusi yetu na badala yake tuzitumie fedha hizi kwa kujenga mambo ya maendeleo kama hii skuli, kwani tusipo jenga wenyewe hakuna atakae kuja kutujengea”alisema Mkuu wa mkoa huyo.

Aidha amewatoa hofu wanamtambile kwa kuwahakikishia kuwa pesa yeyote itakayo tolewa kwa ajili ya mchango wa skuli hiyo haitatumika kwa shuhuli nyengine zaidi ya ujenzi huo na kuwatahadharisha wanakamati kuwa  yeyote atakae jaribu kuzidokoa atamshughulikia ipasavyo.

Sambamba na hayo Mh, Hemed amewataka kila mfanyakazi wa serikali ambaye ni mzaliwa wa Mtambile kuchangia ujenzi wa skuli hiyo kwa kiwango cha laki moja ndani ya mezi mitatu pia nakuwata wanamtambile
walio nje ya nchi nao kujitokeza kutoa mchango wao ili kuwezesha kufanikisha ujenzi  wa skuli hiyo.

Akisoma risala ya wanafunzi wa skuli hiyo Mwalimu Yussuf Zubeir  Ame amesema skuli yao inafanikiwa kupasisha wanafunzi kwa madaraja yote ila wameshindwa kuondosha zero katika skulini yao kutokana na utoro kwa baadhi ya wanafunzi.

Amesema kuwa pia skuli inakabiliwa na changamoto  ya ubovu wa majengo pamoja na  uhaba wa madarasa ya kusomea hali ambayo imepelekea chumba kimoja kubeba wanafunzi wasiopungua sabiini na tano.

Akimkaribisha mgeni rasmi mkuu wa wilaya ya Mkoani Mh,Issa Juma Rashid amewataka wananchi kuamka katika kuleta maendeleo katika maeneo yao sambamba na kuahidi kuwa uongozi wa wilaya upo tayari kushirikiana nao
kwa hali na mali kufanikisha ujenzi wa skuli  hiyo ili kuwapatia watoto elimu bora inayoendana na wakati.

Katika harambee hiyo jumla ya Shilingi Milioni kumi na nane , laki nane, thelathini na tatu elfu mia nane na hamsini zimepatikana pamoja na mifuko ya saruji 420  ambapo jumla ya shilingi milioni mia moja na thelathini na tatu zinahitajika ili kukamilisha ujenzi huo

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.