Habari za Punde

TRA, POLISI YAKAMATA MAJAHAZI MANNE YENYE BIDHAA MBALIMBALI KUPITIA NJIA YA MAGENDO


Na Veronica Kazimoto,Tanga,
 Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi mkoani Tanga imekamata majahazi manne yenye bidhaa mbalimbali katika Kijiji cha Kigombe wilayani Muheza kwa kupitia njia ya magendo zikitokea visiwani Zanzibar.

Akizungumza hivi karibuni baada ya kukamata majahazi hayo, Meneja wa Forodha kutoka TRA mkoani hapa Edward Ndupa alisema kuwa, bidhaa zilizokamatwa ni pamoja na tani 5 ya sukari, vitenge, khanga na mafuta ya kupikia madumu 470 ya lita 20 kila moja.

"Tumefanikiwa kukamata majahazi manne yakiwa na tani 5 za sukari, vitenge, khanga pamoja na mafuta ya kupikia madumu 470 ambapo thamani ya bidhaa zote hizo ni takribani shilingi milioni 35", alisema Ndupa.

Ndupa ameeleza kuwa, mpaka sasa wafanyabiashara wenye bidhaa hizo hawajafahamika hivyo, Mamlaka inafanya utaratibu wa kuzitaifisha moja kwa moja.

Naye Kamanda wa Polisi mkoani hapa,  Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) 
Edward Bukombe amewataka wafanyabiashara wote wanaojihusisha na biashara za magendo kuacha mara moja vitendo hivyo na kuongeza kuwa, jeshi hilo litaendelea kushirikiana na TRA kwa ajili ya   kuwakamata wale wote wanaosafirisha bidhaa kupitia njia sizizo rasmi.

"Natoa wito kwa wafanyabiashara wote wanaokwepa kulipa kodi na kupitisha bidhaa zao katika njia za magendo kuacha mara moja tabia hiyo. Sisi kama Jeshi la Polisi, tumejipanga vizuri na tutaendelea kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania kuwabaini na kuwakamata wafanyabiashara wanaokiuka sheria ikiwa ni pamoja na kukamata bidhaa husika," Alisisitiza Bukombe.

SACP Edward Bukombe amewahimiza wafanyabiashara kufuata sheria, kanuni na taratibu ili waweze kufanya biashara zao bila kubughudhiwa na hatimaye waweze kujiingizia kipato kilicho halali.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.