Habari za Punde

Waziri wa Afya wa Zanzibar Mhe. Hamad Rashid Mohammed Afanya Ziara ua Kutembelea Kituo Cha Afya Rahaleo na Makaazi ya Madaktari wa China na Cuba.

Na Ramadhani Ali – Maelezo Zanzibar.
Waziri wa Afya Hamad Rashid Mohamed amesisitiza msimamo wake wa kufuatilia na kupambana na Wafanyakazi wakorofi  wenye tabia ya kuwatolea lugha chafu  wagonjwa wanapofika vituo vya afya kutafuta huduma.
Amesema Wafanyakazi wengi wa vituo vya afya ni wazuri na wanatekeleza wajibu wao kwa uadilifu mkubwa lakini bado wapo wafanyakazi wachache wenye tabia ya kuwanyanyasa wagonjwa na kuwaharibia sifa nzuri wenzao.
Waziri Hamad Rashid ameeleza hayo alipokuwa akizungumza na Wafanyakazi wa Kituo cha afya cha Rahaleo baada ya kufanya ziara ya ghafla katika kituo hicho.
Aliwakumbusha wafanyakazi wa sekta ya afya kuwa kilio kikubwa cha Wananchi kilikuwa ni upungufu wa dawa na lugha mbaya kwa wagonjwa lakini tatizo la dawa Serikali imelipatia ufumbuzi .
Aliwataka wafanyakazi wa afya kubadilika na kuwafanyia wema na kuwapa upendo  wananchi wanapofika katika vituo vyao  kwa vile lugha nzuri inawapa nafuu wagonjwa .
Hata hivyo Waziri wa Afya amewataka wagonjwa na jamaa za wagonjwa wanapofika vituo vya afya kufuata taratibu zilizowekwa ili kujenga maelewano mazuri na wafanyakazi.
Aidha Waziri Hamad Rashid ameziagiza Manispaa na Mabaraza ya Miji kuimarisha usafi katika vituo vya afya kufuatia uamuzi wa Serikali wa kufanya ugatuzi na vituo hivyo kuwa chini yao.
Mfanyakazi wa Maabara wa Kituo cha Rahaleo Ineneni Fadhil Abdalla alimueleza Waziri Hamad kuwa baadhi ya wananachi wanaopeleka wagonjwa vituo vya afya wamekuwa chanzo kikubwa cha kuvuruga uhusiano mwema baina yao na wagonjwa.
Amewashauri wananchi kwa upande wao kuwa wavumilivu na kuwasaidia  wanapofika kupatiwa huduma ili kazi zao ziwe nyepesi zaidi.
Wakati huo huo Waziri wa Afya alitembelea makaazi ya Madaktari wa China na Cuba katika mtaa wa Vuga na kuwashukuru  kwa kazi nzuri wanayofanya ya kuwahudumia wananchi wa Zanzibar.
Alitoa pongezi maalum kwa Serikali ya Cuba kwa msaada  mkubwa uliopelekea kuanzishwa shahada ya kwanza katika Chuo cha Taaluma za Sayansi za afya na kukubali kuwapokea wanafunzi wanaochuka shahada hiyo kwa masomo zaidi katika nchi yao.
Amewaomba wahadhiri wa Cuba wanaofundisha Chuo hicho kutoa ushauri kwa Wizara ya afya juu ya kuimarisha huduma ya afya ya msingi na mbinu zitakaosaidia kupunguza idadi ya wagonjwa wa Zanzibar wanaopelekwa nje kwa ajili ya matibabu.
IMETOLEWA NA MAELEZO ZANZIBAR

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.