Habari za Punde

Balozi Seif afungua Tamasha la Michezo la Zahlife Uwanja wa Amaan Zanzibar.

Na Othman Khamis, OMPR
Wizara zinazoshughulikia michezo nchini zimetolewa wito wa kufundisha michezo kwa Vijana ili iwe fursa kubwa ya biashara itakayowawezesha kuchangamkia ajira zinazopatikana kupitia mashindano makubwa ya michezo inayokuwa ikifanyika ndani na nje ya nchi.
Wito huo umetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati akilifungua Tamasha la Mashindano ya Michezo ya Vyuo Vikuu na Taasisi za Elimu ya Juu Zanzibar {ZAHILFE} hapo katika Uwanja wa Amani Mjini Zanzibar.
Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeamua kwa makusudi kulirudisha vuguvugu la Michezo katika Skuli na Taasisi za Elimu ya juu kwa kuanzisha Idara Maalum inayosimamia Michezo na Utamaduni ndani ya Wizara ya Elimu ili kuirejeshea hadhi yake Sekta hiyo muhimu ya Michezo.
Balozi Seif alisema wakati umefika sasa kwa Jamii kubadilisha mitazamo yao katika kuiona Michezo ni Burdani tu, badala yake wanalazimika kusaidia kuchangia Sekta hiyo ambayo kwa sasa imetanuka na kuwa ya kibiashara zaidi hali itakayowafanya Vijana wao kukomboka Kimaisha.
Alisema wapo Vijana wa Kitanzania ambao kwa sasa wanashiriki mashindano mbali mbali kwenye Timu ya Kigeni nje ya Nchi. Hivyo alielezea matumaini yake kwamba ndani ya Mashindano hayo wamo Vijana watakaokuwa na hadhi ya kucheza katika Kiwango cha Kitaifa na Kimataifa.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema umuhimu mkubwa unaopatikana ndani ya sekta ya michezo husaidia Taifa kujenga umoja, maelewano na mshikamano miongoni mwa Wanamichezo, Vijana na hata Jamii kwa ujumla.
Alisema hatua hiyo hupelekea Vijana kutoka Vyuo na Maskuli mbali mbali kupata nafasi ya kukutana na kubadilishana mawazo katika mambo tofauti ya kimaisha zikiwemo fursa za ajira kupitia Michezo.
Aliipongeza Wizara ya Elimu na Mafunzo ya  Amali Zanzibar  kwa kutekeleza kwa vitendo Sera ya Michezo ya Zanzibar ya Mwaka 2007 ambayo imeweka bayana umuhimu wa michezo kwa Makundi mbali mbali Vikiwemo Vyuo Vikuu, Taasisi za Elimu na Juu na Skuli ya Jumla.
Akizungumzia nidhamu ambayo ndio ngao ya Mwanamichezo mzuri Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema kwa kiasi kikubwa sifa hiyo muhimu humsaidia Mwanafunzi katika ufaulu wake na kupata matokeo mazuri katika masomo yake.
Balozi Seif alitoa wosia kwa vijana na Wanamichezo hata Nchini kujua umuhimu wa suala zima la nidhamu itakayowawezesha kukamilisha mashindano yao kwa mafanikio na ufanisi mkubwa.
Alikumbusha umuhimu wa nidhamu na kufahamisha kwamba Jamii ya Kimataifa imeshuhudia muda mfupi uliopita  jinsi Timu ya Taifa ya Japan na Senegal zote zikiwa na nukta pamoja na magoli ya kufunga sawa lakini Japan ikateuliwa kusonga mbele raundi ya Pili ya mashindao ya Kombe la Dunia yanayoendelea Nchini Urusi hivi sasa.
Hii imetokana na nidhamu kubwa iliyoonyesha Timu hiyo ya Bara la Asia ambayo imeonyesha mfano kwa  kundi la Wanamichezo wanaopaswa kuiga tabia hiyo nzuri.
Akisoma Risala Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyuo Vikuu na Taasisi za Elimu ya Juu Zanzibar { ZAHILFE} Abdulatif Qadir Mussa alisema kwamba Taasisi yao imefanikiwa kupiga hatua kubwa ya maendeleo kwa kuwaunganisha wanachama wake.
Abdulatif alisema Zahilfe imeweza kusimamia vyema ustawi wa Wanafunzi kwa kuratibu Semina mbali mbali za Mikopo ya Elimu ya juu jambo ambalo limewezesha kuviunganisha Vyuo Vikuu katika kusimamia Haki zao za Kielimu.
Mwenyekiti huyo wa Shirikisho la Vyuo Vikuu na Taasisi za Elimu ya Juu Zanzibar kwa niaba ya wanachama wenzake wameipongeza Serikali Kuu  kwa jitihada inazoendelea kuchukuwa za kuzitafutia ufumbuzi changamoto zinazowakabili Wanafunzi wa Elimu ya Juu.
Alisema ushirikiano huo mkubwa umepelekea Wanachama  wa shirikisho hilokuaminika ndani ya Jamii na hatimae baadhi yao tayari wameshakabidhiwa nyadhifa mbali mbali za kulitumikia Taifa katika fani ya Siasa na Kiserikali.
Akimkaribisha Mgeni Rasmi kulifungua Tamasha hilo la Mashindano ya Michezo ya Vyuo Vikuu na Taasisi za Elimu ya Juu Zanzibar, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Riziki Pemba Juma alisema Wizara itaendelea kusimamia vipaji vya Vijana vinavyoibuka katika mashindano na michezo mbali mbali
Waziri Riziki alisema ushiriki wa Timu za vyuo Vikuu vya Zanzibar katika Mashindano ya Michezo mbali mbali Nje ya Nchini unaendelea kuinawa uso Zanzibar ikilenda kuirejeshea hadhi yake Kimataifa.
Alisema Serikali kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar itahakikisha kwamba inaendelea kuthamini ushindi unaoletwa Ncxhini na Wanamichezo wote wanaoiletea sifa Zanzibar katika mashindano ya Kitaifa na Kimataifa.
Ujumbe wa Mwaka huu wa Tamasha la la Mashindano ya Michezo ya Vyuo Vikuu na Taasisi za Elimu ya Juu Zanzibar {ZAHILFE} unasema Kijana shiriki michezo na tupihe vita Rushwa na uhujumu wa Uchumi kwa Maendeleo ya Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.