Habari za Punde

Katika kukabiliana na matatizo ya akili Serikali yaamua kupeleka huduma za afya ya akili kwenye vituo vya afya

Na Ramadhani Ali – Maelezo                 
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeamua kupeleka huduma za afya ya akili katika vituo vya afya vya daraja la pili Unguja na Pemba pamoja na Hospitali tatu za Wilaya Pemba na Hospitali za Cottage ili kusogeza huduma hizo karibu na  wananchi.
Katika kufanikisha mpango huo Wizara ya Afya imeandaa mafunzo ya siku tatu kwa watoa huduma za afya kutoka vituo mbali mbali vya Serikali na vikosi vya ulinzi ili kuwajengea uwezo watendaji wa vituo hivyo.
Akifungua mafunzo ya siku tatu katika Hospitali ya wagonjwa wa akili Kidongo chekundu, Naibu Waziri wa Afya Harusi Suleiman alisema matatizo ya afya ya akili ni miongoni mwa matatizo yanayoongezeka kwa kasi hivi sasa.
Alisema takwimu za afya ya akili zinaonyesha kuwa maradhi hayo yanashika nafasi ya 13 na asilimia kubwa ya wagonjwa hao hawapati matibabu kutokana na kutojulikana katika hatua za awali.
Aliongeza kuwa Shirika la Afya Duniani limebaini kuwa kati ya wafanyakazi sita mmoja anamatatizo ya afya ya akili, asilimia 45 ya wafanyakazi wanaugua matatizo mbali mbali ya akili na asilimia 85 ya wafanyakazi wana shida mbali mbali za afya ya akili lakini bado hawajagundulika na kuanza tiba sahihi.
Aliwashauri wananchi kuwa tayari kutumia huduma za afya ya akili katika vituo vya afya vya karibu licha ya kwamba katika hatua za awali kutakuwa na changamoto mbali mbali za utendaji.
Naibu Waziri alitoa shukrani kwa Chuo Kikuu cha Haukeland cha Norway na Shirika linalosaidia huduma za afya Zanzibar HIPZ kwa mchango  wao mkubwa katika kufanikisha mpango huo.
Akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo hayo, Mkurugenzi Kinga na Elimu ya Afya Dkt. Fadhil Abdalla aliwashauri watoa huduma za afya kutafuta elimu ya fani hiyo kwani zipo fursa nyingi za kujiendelleza.
Alitanabahisha kuwa wataalamu wa kada ya afya ya akili Zanzibar bado ni kidogo na hawakidhi mahitaji yatakayokuwepo baada ya kupeleka huduma hizo vituo vya afya vya vijijini.
Mkuu wa Kitengo cha maradhi yasiyoambukiza (NCD) Omar Mwalimu ambapo kitengo hicho kinashirikiana na Hospitali ya Kidongo chekundu kufanikisha mpango huo alisema lengo ni kuwatambua wagonjwa wa afya ya akili katika hatua za awali na kuwapatia huduma mapema.
Alisema kwa miaka mingi kumekuwa na tatizo la kupeleka wagonjwa wa afya akili Hospitali ya Kidongo chekundu kutokana na kukosekana huduma hiyo sehemu nyengine katika visiwa vya Zanzibar lakini kuanzishwa kwa mpango huo tatizo hilo litapungua.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.