Habari za Punde

Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango Kituo Cha Utafiti Naliendele Mkoani Mtwara Kupewa Fedha za Kutosha.





Na Benny Mwaipaja, WFM, Mtwara
WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, ameuahidi uongozi wa Kituo cha Utafiti wa Kilimo Naliendele kwamba Serikali itakiwezesha Kituo hicho na vituo vingine vya utafiti nchini ili viendeleze kazi ya utafiti wa mazao ya kilimo ambacho kinategemewa na watanzania wengi katika kujikwamua kiuchumi.

Dkt. Mpango ametoa ahadi hiyo alipotembelea Kituo cha Utafiti Naliendele, mkoani Mtwara, ambacho uongozi wake ulielezea wasiwasi wake wa kupata rasilimali fedha za kuendeleza utafiti wa mazao likiwemo zao la korosho pamoja na watumishi baada ya kuondolewa kwa fedha za ushuru wa korosho  inayouzwa nje, zilizokuwa zikitumika kuendeleza utafiti huo.

Alisema kuwa Serikali inatambua umuhimu wa shughuli za utafiti katika kuendeleza uchumi na maendeleo ya nchi kwa ujumla na kwamba atajitahidi kama Waziri wa Fedha na Mipango kwa kushirikiana na Waziri mwenzake anayeshughulikia kilimo ili taasisi hiyo isikwame kufanya shughuli zake.

"Niwahakikishie kabisa kwamba Serikali haitakubali utafiti wa mazao yote unaofanyika hapa likiwemo zao la korosho udhurike, litakuwa ni janga kubwa, kwahiyo upatikanaji wa fedha za Kituo hiki litakuwa ni moja ya vipaumbele vyangu" alisisitiza Dkt. Mpango

Alisema kuwa kilimo ndiyo uti wa mgongo wa Taifa na kwamba hakutakuwa na mapinduzi ya viwanda bila kilimo kwa sababu viwanda vinavyojengwa vinatarajiwa kuongeza thamani ya mazo ya kilimo pamoja na mazao ya mifugo na uvuvi.

Awali, Mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti wa Kilimo Naliendele, Dkt. Omari Mponda, alieleza kuwa Kituo chake kinahitaji zaidi ya shilingi bilioni 7 kwa mwaka ili kiweze kuendeleza shughuli za utafiti hasa baadaya Serikali kuamua kupanua shughuli za utafiti wa zao la korosho kwenye mikoa mingine nchini.

Alisema kuwa hivi sasa Kituo kimeelekeza nguvu zake katika utafiti wa ugonjwa mpya unaoathiri kwa kiwango kikubwa zao la korosho ujulikanao kama mnyauko fusari (Fusarium wilt) , ulioathiri zao hilo katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Mkuranga, Masasi, Tandahimba, Mtwara na Liwale, lakini changamoto kubwa inayowakumba ni ukosefu wa fedha za kuendeleza utafiti huo.

"Mheshimiwa Waziri, Kituo hiki pia kina zaidi ya asilimia 50 ya watumishi ambao wameajiriwa kwa njia ya mikataba na wanahitaji kulipwa vizuri ili wabaki Kituoni hapa kuendeleza shughuli za utafiti ndio maana nasema tuna mahitaji makubwa ya fedha na tunaiomba Serikali iliangalie jambo hili" Alisema Dkt. Mponda.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.