Habari za Punde

Kilele cha maadhimisho ya siku ya maadili na haki za binadamu ZanzibarTAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU KILELE CHA MAADHIMISHO YA SIKU YA MAADILI NA HAKI ZA BINAADAMU ZANZIBAR YATAKAYOFANYIKA TAREHE 10/12/2018.
Kila ifikapo tarehe 9 Disemba ya kila mwaka dunia huadhimisha siku ya kupinga rushwa ambayo imeridhiwa na kupitishwa na Umoja wa Mataifa kupitia mkataba wa Kupinga Rushwa ulioidhinishwa mwaka 2003. Vile vile, katika jitihada za kuondoa aina zote za ubaguzi, kueneza uhuru na kupambana na vitendo vya uvunjifu wa haki za binaadamu tarehe 10 Disemba, 1948 Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipitisha Azimio la Kimataifa la Haki za Binaadamu na kuchaguliwa rasmi kuwa kila ifikapo tarehe 10 Disemba ya kila mwaka ni siku ya Haki za Binaadamu duniani.

Kwa kuwa kila ifikapo tarehe 9 Disemba ya kila mwaka Jamuhuri ya Muungano waTanzania huadhimisha   siku ya Uhuru wa Tanganyika. Kwa upande wa Tanzania Serikali ya Jamuhuri ya Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeamua kuwa tarehe 10 Disemba  kila mwaka iwe ndio siku ya kuadhimisha kilele cha siku ya Maadili na Haki za Binaadamu.  

Taasisi zinazohusika moja kwa moja na usimamizi wa jukumu la Maadili na Haki za Binaadamu ni tano (5) nazo ni : Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi, Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Idara ya Utawala Bora na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora. Kupitia siku hii ya maadhimisho ya siku ya Maadili na Haki za Binaadamu, taasisi hizi hufanya shughuli mbali mbali ikiwemo kuratibu matukio yenye mnasaba na uimarishaji wa Maadili na Utawala Bora nchini.

Katika kuadhimisha siku hii adhimu, Taasisi zinasimamia Maadili na Haki za Binaadamu zimefanya shughuli mbali mbali ikiwemo utoaji elimu kama ifuatavyo:-

1.      Kuandaa na kurusha vipindi kupitia vyombo mbali mbali vya habari;
2.      Kuandaa mikutano na Sekta mbali mbali;
3.      Kuandaa mikutano katika shehia mbali mbali za Unguja na Pemba;
4.      Kuandaa mkutano na sasi za kiraia;
5.      Kufanyika kwa uzinduzi wa klabu za mapambano dhidi ya rushwa;
6.      Kufanyika kwa bonanza la mpira wa miguu; na
7.      Kuandaa makongamano mbali mbali.

Maadhimisho  haya ya siku ya Maadili na Haki za Binaadamu  kila mwaka huja na ujumbe mahasusi ambapo ujumbe wa mwaka huu unasema “tuimarishe uadilifu, uwajibikaji, haki za binaadamu na mapambano dhidi ya rushwa kwa maendeleo ya taifa”. Sherehe za mwaka huu zinatarajiwa kufanyika kesho Jumaatatu tarehe 10 Disemba, 2018 katika uwanja wa Gombani Mpya Chake Chake Pemba.  Wageni mbali mbali wa kitaifa, viongozi wa umma na wajumbe wa kimataifa wanatarajiwa kuwepo katika maadhimisho hayo ambayo Mgeni Rasmin atakuwa Makamo wa Pili wa Rais, Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi.

Wananchi wote wa kisiwa cha Pemba wanaombwa kushiriki katika maadhimisho hayo kwani mapambano dhidi ya rushwa, maadili ya uongozi, haki za binaadamu ndio chachu ya maendeleo ya wananchi na nchi yetu. 

Hivyo, bila ya kuwepo kwa nguvu za pamoja na mashirikiano baina ya mamlaka husika na wananchi mapambano haya hayawezi kufanikiwa. Mambo mbali mbali yatakuwepo katika kilele cha maadhimisho hayo yakiwemo utoaji wa taarifa za kimaendeleo katika sekta husika, kupata msaada wa haki na elimu ya wajibu wa raia na elimu ya utawala bora.
Ahsanteni nyote mnakaribishwa.

Imetolewa na
…………………………………..
Assaa A. Rashid
Mwenyekiti wa Kamati ya Maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binaadamu Zanzibar ambae pia ni Mwenyekiti wa Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.