Habari za Punde

Uzinduzi wa Tamthilia ya Mtumwa Hadi Siti Binti Saad


Mjumbe wa Bodi ya Taasisi ya Mwanaharakati ya Bibi Siti Binti Saad Bwana Mbarawa akimkabidhi Balozi Seif picha mahiri ya kuchora ya Bibi siti na Kikundi chake wakati wa enzi zake ya uimbaji.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizindua Kitabu cha Tamthilia ya Mwanaharakati Bibi Siti Binti Saad kilichoandikwa na Profesa Em,manuel Mbogo.
Balozi Seif Kulia akikabidhi Hati ya Uwanachama wa  Taasisi ya Mwanaharakati Bibi Siti Binti Saad Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mheshimwa Ayoub Mohamed Mahmoud.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Kitabu cha Tamthilia ya Mwanaharakati Bibi Siti Binti Saad kilichoandikwa na Profesa Em,manuel Mbogo.
Waswahili wakijimwaga kwenye burdani ya muziki wa asili uliokuwa ukitumbuizwa na Kikundi cha Taarab cha Akheri Zamani hapo katika Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil Kikwajuni Mjini Zanzibar.
 Balozi Seif Kati kati waliokaa vitini akiwa katika picha ya pamoja na Wanachama wa Taasisi ya Mwanaharakati Bibi Siti Binti Saad mara baada ya uzinduzi wa Kitabu cha Tamthilia ya Mwanaharakati huyo.
Balozi Seif Kati kati waliokaa vitini akiwa katika picha ya pamoja na Kikundi cha Taarab cha Akheri zamani kilichokuwa kikitoa burdani kwenye hafla ya uzinduzi wa Kitabu cha Tamthilia ya Mwanaharakati Bibi Siti Binti Saad.

Picha na – OMPR – ZNZ.
Na.Othman Khamis OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema wakati umefika kwa Wasomi au Watu wa kawaifa wenye uwezo na Taaluma ya kuandika kuibua na kuiweka hadharani hazina ya Mashujaa wa fani mbali mbali ili Vizazi vya sasa na vile vijavyo viweze kufaidika na michango yao.
Alisema Visiwa vya Zanzibar vimebahatika kukaliwa na mashujaa wa fani tofauti ikiwemo, Uchumi, Siasa na Utamaduni, lakini kwa bahati mbaya Wasomi wengi wamekuwa wavivu kutafiti maisha yao na hatimae kuyawasilisha kwa Jamii kwa nia ya Vitabu.
Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati akizindua Tamthilia ya Mtumwa hadi Siti Binti Saad iliyotungwa na Mwandishi Mahiri na mpenzi mkubwa wa Lugha ya Kiswahili Nchini Profesa Emmanuel Mbogo hapo katika Ukumbi wa Sheikh Idiss Abdulwakil Kikwajuni Mjini Zanzibar.
Alisema kunakili hadhithi na kuzichapisha kwenye Vitabu ni njia murua na muwafaka  ya kuwaenzi mashujaa hao na itapendeza zaidi iwapo simulizi zao zitachapishwa kwa kutumia Lugha Mama na sanifu iliyozoeleka ya Kiswahili ili zipate wasomaji wengi zaidi.
Balozi Seif alieleza anaamini kuwa Historia ya Zanzibar haiwezi kukamilika bila ya kuelezea maisha ya Msanii maarufu wa Taarabu Afrika Mashariki Bibi Siti Binti Saad ambapo kwa bahati nzuzi Profesa Emmanuel Mbogo ameifanya kazi hiyo ya kuinawirisha Historia ya Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisisitiza kwamba Uandishi wa Historia za Mashujaa wa Fani mbali mbali Visiwani Zanzibar na Mwambao wa Afrika Mashariki ni muhimu kwa Jamii kwa vile Hadithi zao husaidia kuchangamsha na kushajiisha kuiga mwenendo wa maisha yao.
“ Kwa hakika Hadhithi za Maisha ya Mashujaa zikisomwa na kuzingatiwa hutuangazia mwanga  wa kuona uwezekano wa kubadilisha maisha yetu pengine siku moja na sisi tukaweza kugeuka tukawa kama wao au zaidi”. Alisema Balozi Seif.
Alimpongeza na kumshukuru Profesa Emmanuel Mbogo kwa mchango wake wa kupanda mbegu ya mashujaa wa baadae kupitia Tamthilia  yake  inayohusu Maisha ya Siti Binti Saad inayoweza kuzalisha katika Jamii hii akina Siti Binti Saad wengine  katika siku zijazo.
Balozi Seif alitoa wito kwa Vijana wa sasa kuisomaTamthilia hiyo ya Mtumwa hadi Siti Binti Saad na kuizingatia kwa vile inatoa funzo la umuhimu wa kung’ang’ania ndoto mpaka itowe matunda anayoyakusudia Mtu.
Alisema Vijana wengi kwa sasa wamejenga hulka ya kutojiamini na kuacha ndoto zao za Kimaisha na badala yake hutafuta njia za mkato ambazo mara nyingi haziwezi kuwaletea hatma njema ya maisha yao.
Balozi Seif aliwanasihi Vijana kuiga  mfano bora wa Marehemu  shujaa Bibi Siti Binti Saad kutokana na ujasiri wake aliyoujenga wakati alipoamua kuzisimamia ndoto zake zilizompa shime ya kujifunza kusoma na kuimba.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar akichambua baadhi ya maneno yaliyomo ndani ya Tamthilia hiyo ya kurasa 88 kwenye onyesho la kwanza katika kichwa cha Habari kisemacho Uchumba, akijikita zaidi kwenye lugha ya Mahaba alisema kwa sasa imetoweka katika jamii Nchini.
Alisema kutoweka kwa maneno matamu kunachangia kwa kiasi kikubwa Vijana wengi walio kwenye Ndoa kutumia njia ya mkato ya kutoa Talaka kwa Wake zao kutokana na kushindwa kuwashawishi kudumu kwenye ndoa kwa kutumia lugha ya Mahaba.
Balozi Seif  alifahamisha kwamba kukosekana kwa maneno matamu Mitaani hata katika Familia kipindi hichi cha kizazi cha sasa inawezekana ikawa ndio chanzo cha kuvunjika kwa uhusiano katika Jamii.
“ Tafadhali egesha sikio lako kifuani kwangu ili upate kusikia jinsi moyo  wangu unavyodunda, ukikutaja, ukikuita na kusema  - Mtumwa,  nakupenda”. Balozi Seif akikariri baadhi ya maneno matamu kutoka kwa Bwana Khamis akitafuta penzi la Mkewe Bi. Siti.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliipongeza Taasisi ya Siti Binti Saad Zanzibar kwa juhudi iliyochukuwa ya kufanikisha tukio hilo muhimu la uzinduzi wa Tamthilia ya Shujaa huyo wa Sanaa Afrika Mashariki ambayo itaendelea kubakia  sehemu ya Urithi wa Taifa hili.
Akitoa maelezo ya siku ya Urithi wa Utamaduni Duniani Mshika Fedha wa Taasisi ya Mwanaharakati Bibi Siti Binti Saad Bibi Aziza Saleh alisema Taasisi hiyo kupitia Azimio linaloshajiisha Nchi zilizomo katika Uhifadhi wa Urithi wa Kimataifa limeandaa mambo yanayorithisha Vijana kurithi Tamaduni za Taifa.
Bibi Aziza alisema zipo hatua ambazo tayari zimeshachukuliwa kutekeleza Malengo hayo ikiwemo Makongamano ya Watu na Jumuiya tofauti, kutoa mafunzo ya uchoraji wa aina mbali mbali hata kuendeleza Lugha adhimu ya Kiswahili ambayo kwa sasa inashika nafasi ya Kumi Duniani.
Alieleza kwamba Taasisi ya Mwanaharakati Bibi Siti Binti Saad bado inazingatia kutosahau thamani ya Utamaduni wa asilia unaopaswa kuonyeshwa kwa Vijana wa kisasa hasa upishi na vyakula vya Ladu za mtama, vileja, visheti pamoja na kashata za nazi na njugu  ili wathamini cha asili.
Akimkaribisha kuzindua Tamthilia ya Mtumwa hadi Siti Binti Saad Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwanaharakati Bibi Siti Binti Saad,  Bibi Nasra Hilal alisema yapo mafanikio makubwa yaliyopatikana tokea kuasisiwa kwa Taasisi hiyo Miaka Mitano iliyopita.
Bibi Nasra alisema ushirikiano wa karibu uliopatikana baina ya Wana Taasisi hiyo na Wadau wa Utamaduni wa Mswahili umewezesha kupiga hatua kubwa Malengo ya kuanzishwa kwa Taasisi hiyo ikiwemo matayarisho ya ujenzi wa Jengo la Utamaduni la Taasisi ya Mwanaharakati Bibi Siti Binti Saad.
Katika hafla hiyo ya uzinduzi wa Tamthilia ya Mwanaharakati Bibi Siti Binti Saad Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alikabidhi Hati za Uanachama wa Heshima kwa washirika wa Taasisi hiyo.
Uzinduzi huo wa Tamthilia ya Mtumwa hadi Siti Binti Saad umefanyika ukiambatana ndani ya Wiki ya Uhifadhi wa Urithi wa Utamaduni Duniani { World Culture Heritage Day } inayoadhimishwa na Umoja wa Mataifa { UN } kila ifikapo Tarehe 18 Aprili ya Kila Mwaka.
Mji Mkongwe wa Zanzibar { Maarufu Stone Town } umebahatika kuwemo miongoni mwa Miji iliyoidhinishwa na  Shirika la Umoja wa Mataifa linalosimamia Elimu, Sayansi na Utamaduni {Unesco} kuwa ndani ya Urithi wa Kimataifa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.