Habari za Punde

CCM wilaya yaiagiza halmashauri kutatua changamoto sekta ya afya



 
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Kusini Unguja Ndg. Abdulazizi Hamad Ibrahim, akizungumza na Wafanyakazi wa Kituo cha Afya katika Jimbo la Makunduzi Mkoa wa Kusini Unguja wakati wa ziara yake katika Wilaya hiyo kuona changamoto zinazozikabili Vituo vya Afya katika Wilaya yake. 
NA IS-HAKA OMAR.Zanzibar.
MWENYEKITI wa CCM Wilaya ya Kusini Unguja Ndg. Abdulaziz Hamad Ibrahim, ameitaka halmashauri ya wilaya hiyo kutatua changamoto zinazovikabili vituo vya afya katika jimbo la Makunduchi ili kwenda sambamba na matakwa ya ugatuzi.
Maelekezo hayo ameyatoa katika ziara ya kamati ya siasa ya wilaya hiyo ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2015/2020 katika vituo vya afya vilivyomo ndani ya jimbo la Makunduchi.
Alisema serikali imefikia uamuzi wa kufanya ugatuzi katika sekta ya afya kwa kuzipatia mamlaka ya usimamizi halmashauri za wilaya kwa lengo la kuimarisha huduma za afya ili wananchi wapate huduma bora na kwa wakati muafaka.
Mwenyekiti huyo aliipongeza serikali kupitia halmashauri ya wilaya kwa kuimarisha upatikanaji wa vifaa tiba na huduma mbali mbali za msingi za afya, lakini bado vituo vingi vinakabiliwa na changamoto ya miundombinu duni ya majengo hali inayosababisha usumbufu kwa wananchi na watumishi wa afya.
Abdulaziz alisema uongozi wa halmashauri ya wilaya hiyo wanatakiwa kufanya ziara za mara kwa mara katika vituo vya afya kwa lengo la kuratibu changamoto zinazovikabili vituo hivyo ili viendelee kutoa huduma bora za afya.
Katika maelezo yake Mwenyekiti huyo kwa niaba ya kamati ya siasa ya wilaya hiyo, alimshukuru Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein kwa kusimamia mfumo wa utoaji wa huduma za afya bure.
“Tumetembelea vituo vya afya mbali mbali vilivyopo katika jimbo la Makunduchi na kujionea namna vinavyotoa huduma za afya kwa wananchi, lakini pia tumebaini uwepo wa changamoto. Tumetoa maelekezo kwa wahusika zitatuliwe kabla ya Mwaka 2020”, alisema Mwenyekiti huyo.
Alisema CCM wilayani humo itaendea kuisimamia serikali itekeleze kwa ufanisi ilani ya uchaguzi hasa katika masusla ya utoaji wa huduma za afya ili kila mwananchi apate fursa hiyo bila vikwazo.
Wakizungumza kwa wakati tofauti maofisa utabibu wa vituo vya afya katika jimbo hilo waliipongeza serikali kuu kwa kufanya ugatuzi ambao umeongeza upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wananchi wa vijijini.
Maofisa hao walizitaja changamoto zinazowakabili kuwa ni pamoja na uchakavu wa majengo ya vituo, ukosefu wa uzio, ukosefu wa huduma za usafiri kwa watumishi wanaoishi mbali na vituo hivyo, ukosefu wa walinzi kwa baadhi ya vituo.
Ziara hiyo imefanyika katika vituo vya afya vya Mtende, Kibuteni, Kizimkazi Mkunguni, Kizimkazi Dimbani  na Muyuni.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.