Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein, akizungumza na Uongozi wa Wizara ya Afya Zanzibar katika Mkutano wa Utekelezaji wa Mpango Kazi (Bango Kitita) kwa mwezi wa Julia 2018 hadi Marchi 2019, uliofanyika katika ukumbi wa Ikulu Ndogo Kibweni Zanzibar .
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesisitiza kuwa chochote kinachoingia nchini kwa ajili ya matumizi ya binaadamu zikiwemo dawa na vyakula
ni lazima zifuate sheria na taratibu zilizopo.
Hayo aliyasema leo, katika ukumbi wa Ikulu ndogo
Kibweni mjini Zanzibar alipokutana na uongozi wa Wizara ya Afya wakati ilipowasilisha
taarifa ya utekelezaji wa Mpango Kazi wa Wizara hiyo kwa Kipindi cha Julai 2018
hadi Machi 2019.
Dk. Shein alieleza kuwa ni kinyume na sheria na
maadili ya dawa kuingiza, kuuza ama kuitangaza bila ya kufuata sheria na
taratibu zilizopo na kueleza haja kwa Wizara ya Afya kulivalia njuga suala hilo
kutokana na kujitokeza kwa wafanyabiashara wa dawa zikiwemo za kiswahili bila
ya kufuata taratibu zilizopo.
Dk. Shein alieleza kuwa hafurahishwi na tabia ya
baadhi ya wafanyabiashara wa dawa wakiwemo waganga wa jadi wanaojitangaza na
kuwafahamisha watu ju ya ubora wa dawa zao na kueleza kuwa hiyo ni kwenda
kinyume na utaratibu na sheria zilizopo.
Alisema kuwa hizo ni mbinu zinazotumika kuwahadaa
wagonjwa na haikubaliki si kwa Zanzibar tu hata nchi nyingi duniani kufanya
biashara ya dawa namna hiyo kwani kila kitu hasa dawa hufuata taratibu na sheria
zilizowekwa kulingana na maadili ya huduma hiyo.
“Haya mambo lazima Wizara ya Afya tuyajuwe,
tunapaswa kuwa na utaratibu, hivyo tuziweze vizuri Sheria zetu pamoja na Sera
ya Afya kwani hali hii ikiendelea wafanyabaishara ya dawa hasa tiba asili watakuja
kutuumizia watu wetu”,alisisitiza Dk. Shein.
Aidha, Rais Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuupongeza
uongozi wa Wizara ya Afya kwa kutekeleza vyema majukumu yao na kueleza kuwa
Wizara hiyo imefanya kazi nzuri.
Aliongeza kuwa ni kawaida kazi ya mwanaadamu huwa
haikosi kasoro lakini hata hivyo juhudi za makusudi zimeweza kuchukuliwa na
uongozi pamoja na wafanyakazi wa Wizara hiyo katika kuhakikisha mafanikio
makubwa yanapatikana.
Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein aliitaka Wizara
hiyo kutoridhika na mafanikio na juhudi hizo zilizofikiwa na kutaka kasi zaidi
iongezwe ili mafanikio zaidi yaweze kupatikana zikiwemo huduma bora za afya kwa
wananchi wote.
Dk. Shein alitumia fursa hiyo kumpongeza Makamo wa
Pili wa Rais Balozi Seif Ali Idd kwa kumsaidia vyema kazi za Serikali pamoja na
kumpongeza Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Dk. Abdulhamid
Yahya Mzee nae kuendelea kumsaidia.
Katika kikao hicho, Makamo wa Pili wa Rais wa
Zanzibar Balozi Seif Ali Idd nae alihudhuria na kutumia fursa hiyo kuupongeza
uongozi wa Wizara hiyo kwa kuendelea kutekeleza vyema majukumu yake huku
akimpongeza Rais Dk. Shein kwa mafanikio yaliopatikana chini ya uongozi wake.
Nae Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee aliipongeza Wizara hiyo kwa kuwasilisha
vyema Mpango Kazi wake .
Nae Waziri wa Afya, Hamad Rashid Mohamed alieleza
kuwa Wizara ya Afya imepiga hatua kubwa katika utoaji wa huduma kwa wananchi
chini ya uongozi wa Rais Dk. Shein ambapo mafanikio kadhaa yamepatikana.
Alisema kuwa mafanikio kadhaa yamepatikana ikiwa
ni pamoja na kuongezeka kwa wataalamu wa afya, ambapo jumla ya wafanyakazi 439
kutoka Unguja 242 na Pemba 197 wa kada mbali mbali wakiwemo madaktari 7 tayari wameajiriwa.
Aliongeza kuwa kuimarika kwa huduma za uchunguzi
wa maradhi na huduma za matibabu nako kumeongezeka sambamba na kupatikana kwa
lift mpya katika Hospitali ya Mnazi Mmoja ambapo kunaifanya hospitali hiyo kuwa
na lift mbili ambazo zote zinafanya kazi sambamba na upatikanaji wa dawa muhimu
katika vituo vya afya kwa kuimarika na kufikia zaidi ya asilimia 90 kutoka
asilimia 50.
Akiyataja mafanikio mengine ni pamoja na
kukamilika kwa ujenzi wa chumba cha upasuaji katika hospitali ya Micheweni na
kupandishwa daraja Hospitali za vijiji ya Kivunge na Makunduchi kuwa Hospitali
za Wilaya ambapo kupandishwa hadhi hospitali hizo ni sehemu ya utekelezaji wa
Ilani ya CCM.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment