Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein, akiwa katika Sala ya kuuombea Mwili wa Marehemu Ali Juma Shamuhuna Sala iliofanyika katika msikiti wa Kijiji Kwao Donge leo kulia Mtoto wa Marehemu Shamuhuna na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakishiriki katika Sala hiyo.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj
Dk. Ali Mohamed Shein ameongoza mamia ya wananchi katika mazishi ya Marehemu
Ali Juma Shamuhuna yaliyofanyika kijijini kwao Donge Eneani, Mkoa wa Kaskazini
Unguja.
Rais Dk. Shein
aliungana na viongozi mbali mbali wa Serikali, dini na vyama vya siasa pamoja
na ndugu, jamaa, marafiki na wananchi kadhaa akiwemo Makamo wa Pili wa Rais
Balozi Seif Ali Idd, Spika wa Baraza la Wawakilishi Zubeir Ali Maulid na viongozi
wengineo.
Mapema Rais Dk. Shein
aliungana na wananchi katika sala ya kumuombea dua Marehemu hapo hapo kijini
kwao Donge Eneani ambapo baada ya sala hiyo taratibu za mazishi zilifanyika.
Akisoma Wasfu wa
Marehemu Ali Juma Shamuhuna, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais
Mohamed Aboud alisema kuwa Marehemu Shamuhuna ambaye alikuwa Waziri wa Elimu na
Mafunzo ya Amali Mstaafu alizaliwa katika kijiji cha Donge mnamo tarehe 01 Januari mwaka 1944.
Katika uhai wake Marehemu
Shamuhuna alipata elimu ya Msingi katika skuli ya Kiembe Samaki na Skuli ya
Msingi ya Makunduchi mwaka 1952 hadi 1959 ambapo pia, alisoma skuli ya
Sekondari ya Lumumba Kidato cha Kwanza hadi cha Nne mnamo mwaka 1959 hadi 1963.
Kwa upande wa Elimu ya
Juu, Marehemu Shamuhuna alisoma Diploma ya Juu ya “Diary Technology”, “B.SC
Animal Production” mwaka 1977 hadi 1980, “M.B.SC Animal Genetics and Breeding”
mwaka 1981 hadi 1982 pamoja na “B.A Economic Inter Trade” mwaka 1992 hadi mwaka
1996.
Marehemu Shamuhuna kwa
upande wa ajira aliwahi kuwa Meneja Mkuu katika Shamba la Mifugo Kizimbani
mnamo mwaka 1966 hadi 1969, alikuwa Meneja Mkuu wa Shamba la Wanyama Kizimbani,
Tunguu, Pangeni na Hanyegwa Mchana mnamo mwaka 1969 hadi 1976.
Pia, Marhemu Shamuhuna
aliwahi kuwa Meneja Mkuu wa Ushirika wa Uzalishaji wa Wanyama mnamo mwaka 1981
hadi 1985, Mkuu wa Mradi wa “World Food Programme” ulioendeshwa na Shirika la
Umoja wa Mataifa la (UNDP) mwaka 1985 hadi 1988 na hatimae kufikia Katibu Mkuu
Wizara ya Kilimo mwaka 1988 hadi 1990.
Kwa upande wa nafasi
za Kisiasa, Marehemu Shamuhuna alikuwa Mwanachama mwaminifu wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM), na alikamata nyadhifa mbalimbali ikiwemo Mhasibu katika Tawi
la Kwahani mwaka 1981 hadi 1985, Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Mkoa mwaka 1985
hadi 2012.
Pia, Marehemu
Shamuhuna aliwahi kuwa Mjumbe wa Kuteuliwa kwa uteuzi wa Rais katika Baraza la
Wawakilishi (BLW) mwaka 1995 hadi 2000 ambapo pia, aliwahi kuwa Mbunge wa Bunge
la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia (BLW) mnamo mwaka 1995 hadi 2000.
Aidha, Marehemu
Shamuhuna aliwahi kuwa Kamishna wa Tume ya Muwafaka 2001 hadi mwaka 2002 ambapo
pia, aliwa hukuwa Mwakilishi wa Jimbo la Donge mwaka 2000 hadi 2015 baada ya
hapo alistaafu shughuli za kisiasa.
Sambamba na hayo,
Marehemu Shamuhuna amewahi kushika nyadhifa mbalimbali za Uwaziri katika
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ikiwa ni pamoja na kuwa Naibu Waziri Kiongozi
na Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali,
Waziri wa Ardhi, Waziri wa Nchi Ofisiya Rais Mipango.
Marehemu Shamuhuna amefariki dunia jana jioni
(19.05.2019), huko Fuoni Wilaya ya Magharibi B, Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja,
ambako alikuwa akiugua.
Marehemu amewacha
watoto tisa na kizuka mmoja, Mwenyezi Mungu ailaze mahala pema peponi, roho ya
Marehemu Ali Juma Shamuhuna, Amin.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
Postal Address:
2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment