Habari za Punde

Serikali Kuwajengea Uwezo Mafundi Sanifu wa (MAJENGO) na Mafundi Mchundo Kupitia Miradi Inayotekelezwa Nchini.



Na. Paschal Dotto-Maelezo.                                                                                                        
Serikali Kupitia Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, imesema kuwa itaendelea kuwajengea uwezo na uzoefu mafundi sanifu na mafundi Michundo, ili waendelee kutekeleza kazi zao kwa ufanisi na kuongeza wataalam katika kada hiyo kwani fani hizo zina watu wachache.

Akizungumza  Jijini Dar es Salaam katika Mkutano wa Wasanifu Majengo na mafundi Michundo, Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano,Dkt. Elius Mwakalinga alisema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano imejikita katika kuhakikisha kuwa ujenzi wa miundombinu unafanikiwa kwa kiasi kikubwa.

“Serikali imedhamiria kujenga miundombinu ili kuwezesha ukuaji wa Sekta ya Viwanda nchini, hivyo Mafundi sanifu wanategemewa sana katika kuwezesha miundombinu hii, ili Tanzania iweze kufikia ndoto ya kuwa kwenye uchumi wa kati kupitia viwanda, na katika kutekeleza hilo mwaka wa Fedha 2019/2020, Wizara ya Ujenzi imejikita katika ajenda tatu ikiwemo kuwajengea uwezo wasanifu na wahandisi wote nchini”, Alisema Dkt. Mwakalinga.

Dkt. Mwakalinga alisema kuwa Serikali inahakikisha watalaam chini ya Taaluma ya Uhandisi, Usanifu Majengo, Ukadiriaji Majenzi na kada zingine katika sekta ya ujenzi wanaongezeka kiidadi na kujengewa ujuzi mahsusi ili kuwa na uwezo na kumudu mahitaji ya nchi ya wataalam hao.

Aidha, Dkt. Mwakalinga aliwathibitishia kuwa serikali inaendelea kushirikiana na bodi mbalimbali za taaluma za kihandisi kwa kutoa miradi inayotekelezwa nchini ili kuwawezesha watalaam hao kupata uzoefu na kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa na kazi hiyo itaanza rasmi mwaka wa fedha 2019/2020, Julai Mosi.

“Napenda niwadhihirishie kuwa, Serikali ya Awamu ya Tano, chini ya uongozi wa Rais Magufuli, inayo dhamira ya dhati ya kuendeleza fani ya usanifu kwa kutumia miradi yake inayotekelezwa, kama vile ujenzi wa Reli ya kisasa, SGR, Ujenzi wa Interchange Ubungo, Ujenzi wa Bwawa kubwa la kuzalisha umeme mto Rufiji, na ujenzi wa Daraja la Selander, kwa hiyo miradi hii itaweza kutoa uzoefu mkubwa kwa wataalum wetu”, alisema Dkt. Mwakalinga.

Katika kuongeza uzoefu wa watalaam hao, Dkt Mwakalinga amesema ni lazima kuwepo na maarifa na vitendea kazi ambavyo kwa sasa ni uwepo wa miradi ya kimaendeleo ambayo inatekelezwa na Serikali na sasa mafundi sanifu wanahitajika ili kuiwezesha miradi hii kutekelezwa pasipo gharama kubwa.

Akaongeza kuwa Serikali inapoendelea na zoezi la kuwapa uwezo watalaam hao inawaomba wawe waadilifu, wenye kujituma na wenye weledi mkubwa maana kazi yao hiyo ni kubwa sana kuliko kazi zingine za kihandisi.

“Kama nilivyosema hapo awali tutaendelea kuwajengea uwezo watalaam wetu kwa kutumia miradi tuliyonayo, lakini kujenga uwezo kuna uhusiano mkubwa na masuala ya kujituma, kuijitoa kwa moyo kwa taifa, kufanya kazi kwa bidii na weledi mkubwa, hii ndiyo itakuwa tiketi ya kupata kazi na tutachagua watalaam kulingana na vigezo hivyo,”Alisisitiza Mwakalinga.

Akizungumzia kuhusu changamoto za uhaba wa wataalam hao, Dkt. Mwaklinga aliainisha kuwa, kwa takwimu za Shirika la kazi duniani, ILO, zinabaini kuwa Mhandisi mmoja anapaswa kufanya kazi na Mafundi Sanifu watano, na Mafundi Stadi 25, na kuongeza kuwa hiyo inaonyesha umuhimu wa wasanifu na mafundi stadi katika sekta ya ujenzi.

Kwa Upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili Wahandisi (ERB), Prof. Ninatubu Lema, alisema kuwa Wasanafi wanahitajika kijituma ili kuanzisha viwanda vidogovidogo vya kutengeneza vitu mbalimbali ambavyo vinaweza kuuzwa nchini.

“Mnatakiwa Mafundi Sanifu kuwa wabunifu katika kujenga na kutengeneza uwezo kwa kufanya  wajasiriamali wa kujenga viwanda vidogovidogo, ili mtu mmoja aajiri watu watano, watu sita au watu 10 na kutengeneza vitu vidogovidogo vya kuuzwa hapa nchini, … tuko tayari kuratibu na kwenda kwenye nchi za wenzetu kama India, China kutazama hivyo viwanda vidogovidogo.”, Alisema, Prof.Lema.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.