Habari za Punde

Siku Zikiendelea Wananchi wa Zanzibar Wakiendelea na Harakati za Kununua Vitu Mbalimbali Mtaa wa Mchangani.

Wananchi Kisiwani Zanzibar wakiwa katika harakati za maandalizi ya Sikukuu ya Eid Fitry baada ya kumaliza Mfungio wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kwa kununua bidhaa mbalimbali kwa mahitaji yao katika matumizi ya Sikukuu
WATEJA wa bidhaa za nguzo kwa ajili ya Skukuu Eid-Fitri katika maduka mbali mbali ya visiwa vya Unguja, wamepungua  ikilinganishwa na mwaka uliopita.
Uchunguzi wa Zanzibar Leo, umebaini kuwapo kwa hali hiyo, baada ya Wafanyabiashara mbali mbali wa bidhaa hizo katika maeneo ya Darajani na Saateni ambapo wamekiri juu ya kuwapo kwa hali hiyo.
Mmoja wa wafanyabiashara hao, Fatma Adinani alisema, biashara ya nguo za watoto imekuwa ngumu ambapo kwa siku anaweza kuuza kati ya nguo tatu hadi nne, ikiwa ni tofauti na kipindi kilichopita.
“Tangu ninapofungua duka langu saa nne asubuhi hadi saa 11:00 za jioni hazifiki hata nguo nne ninazouza baraka ya wateja kuuliza bei na kuondoka”,alisema.
Nae, Mfanyabiashara aliejitambulisha kwa jina la Hamadi Mohamed Juma (42),alisema biashara ya nguo na viatu imekuwa nzito ambapo kwa siku anauza wastani wa pea tatu za viatu na nguo zisizozidi mbili.
Alisema kwa uzoefu uliopo katika kipindi kama hicho wanunuzi huwa wengi na wafanyabiashara wamekuwa wakiuza bidhaa hizo kwa kiwango kikubwa ikilinganishwa na miezi mengine.
Mfanyabiashara aliejitambulisha kwa jina la Said Abrahman (34) Saateni alisema, kwamba hali ya biashara sio nzuri hadi sasa pamoja na kuwepo kwa unafuu wa bei kwa baadhi ya nguo.
Nao baadhi ya wateja wa bidhaa hizo walisema sababu kubwa inayochangia kujitokeza hali hiyo, watu wengi wamekuwa na mwamko wa kununua bidhaa Tanzania Bara na wengine wamekuwa wakikopa kwa wafanyabiashara wengine ili kuondokana na ulipaji wa fedha taslimu.
Mmoja ya wateja hao, Khadija Juma Simai alisema, kitendo cha ununuzi wa nguo hivi sasa wengi wanatumia kwa njia ya mkopo na wengine kutokana na kufuata unafuu wa bei  huwenda kununua Tanzania Bara.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.