Habari za Punde

Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA Yaendesha Semina Kwa Makampuni ya Watembeza Watalii Zanzibar.

Afisa Elimu ya mlipa kodi TRA Ofisi ya Zanzibar Abdallah Seif akionesha Kitabu cha Makadirio ya Bajet ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar mwaka 2019-20 kwa washiriki wa Semina iliyohusu utozaji wa Kodi na uwasilishaji waTaarifa za Mapato kwa Kampuni za utembezaji Watalii Zanzibar iliyofanyika Raha leo mjini Zanzibar. Kulia ni Afisa mwandamizi Elimu ya mlipa kodi TRA Shuweikha S. Khalfan. 
Mmoja wa wawakilishi wa Kampuni za utembezaji Watalii Zanzibar Salim Salim akihangia katika Semina iliyoendeshwa na TRA Ofisi ya Zanzibar huko Raha leo mjini Zanzibar kuhusu utozaji wa Kodi na uwasilishaji waTaarifa za Mapato kwa Kampuni za utembezaji Watalii Zanzibar  
Mwakilishi wa Kampuni ya Coral Tour Khamis Makame akichangia katika Semina ya utozaji wa Kodi na uwasilishaji wa Taarifa za Mapato kwa Kampuni za utembezaji Watalii Zanzibar iliyofanyika Raha leo mjini Zanzibar.

Na. Faki Mjaka-Maelezo Zanzibar 
Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA Ofisi ya Zanzibar imezitaka Kampuni za utembezaji Watalii Zanzibar kusajili Kampuni zao na kulipa Kodi kwa wakati ili kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza.

Kwa kufanya hivyo kutawarahisishia kufanya kazi zao na kuwaondoshea usumbufu ikiwemo kulipa faini ya kuchelewesha Kodi hizo.

Wito huo umetolewa na Afisa mwandamizi Elimu ya mlipa kodi TRA Shuweikha S. Khalfan wakati akiwasilisha mada katika Semina ya utozaji wa Kodi na uwasilishaji wa Taarifa za Mapato kwa Kampuni za utembezaji Watalii Zanzibar iliyofanyika Raha leo mjini Zanzibar.

Amesema Sheria ya Kodi ya mapato ya mwaka 2004 ibara 4(1) inamtaka kila mtu ambaye anapata kipato kulipa kodi kwa mujibu wa sheria.

Amesema lengo la Semina hiyo ni kuendelea kutoa elimu kwa kila kundi ambalo lina wajibu wa kulipa Kodi ili kuziba mianya ya upoteaji wa mapato nchini.

Shuweikha amesema TRA inategemea sana wafanyabiashara katika kufanikisha malengo yaliyowekwa ili kuindeleza miradi mbali mbali ya maendeleo na huduma za kijamii nchini.

Wakichangia katika Semina hiyo Wawakilishi wa Kampuni hizo waliiomba TRA kufanya utafiti wa kina kubaini mapato wanayoingiza kabla ya maamuzi ya kutakiwa kulipa Kodi.

“Hakuna ambaye anakataa kulipa Kodi lakini lazima TRA wafanye Research ya kina hasa maeneo tunayofanyia kazi ili wabaini kipato chetu maana ukweli biashara ya kutembeza watalii imekuwa ngumu sana” Alisema Mwakilishi wa Kampuni ya Coral Tour Khamis Makame

Khamis amesema Kampuni za kuendesha utalii zinapitia wakati mgumu hivyo ni vyema kuwe na mikutano ya kuelimishana mara kwa mara kwa lengo la kuongeza uelewa kwa wadau.

“Tunahitaji pia kila mtu kujua Kampuni yake inanufaika vipi na Kodi inayoitoa hasa ikizingatiwa kuwa Kampuni inaweza kupita hata miezi sita bila hata kupata mgeni wa kufanya naye kazi” Alisema Khamis.

Kwa upande wake Salim Salim amesema biashara hiyo imekuwa ngumu kutokana na kuwepo kwa Tozo nyingi zinazotolewa bila kuangalia kipato halisi wanachoingiza kwa mwaka.

Hivyo alishauri Semina zinazofuata TRA wawashirikishe Wadau wengine wa Kodi kama vile ZRB na Halmashauri ili kuwa na msimamo wa pamoja kuhusu ulipaji wa Kodi.

Kwa upande wake Afisa Elimu ya Mlipa Kodi kutoka TRA Abd Seif amesema maoni yaliyotolewa yatafanyiwa kazi ili kuhakikisha Makampuni hayo ya kiutalii yanashirikiana vyema kulipa kodi bila tatizo.

Amesema wataendelea kutoa elimu kwa makundi yote ili kuziba mianya ya ulipaji Kodi nchini.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.