Habari za Punde

Wakazi Zaidi ya 1000 Kanda ya Ziwa Wanufaika na Huduma ya Upasuaji Bure

Dakta Catherine Mung’ong’o Rais wa Chama Cha Madaktari wa Upasuaji Tanzania akizungumza na Wanahabari  katika Hospitali ya Rufaa Bugando jijini Mwanza  hivi karibuni.
Madaktari wakiendelea na zoezi la Opereshi kwa wagonjwa wakati wa siku ya kuhitimisha zoezi la huduma ya upasuaji kwa wagonjwa wanaosubiri kwa muda mrefu toka Kanda ya Ziwa hivi karibuni.Zoezi hilo la siku tano limefanyika kwa ushirikiano baina ya Chama cha Madaktari wa Upasuaji Tanzania na Madaktari wa Hospitali ya Rufaa ya Bungando.
Madaktari wakiendelea kuwashauri wananchi kuhusiana na afya zao katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando jijini Mwanza hivi karibuni.
Dakta Catherine Mung’ong’o Rais wa Chama Cha Madaktari wa Upasuaji Tanzania akizungumza na Wanahabari  katika Hospitali ya Rufaa Bugando jijini Mwanza  hivi karibuni.  (Na: Mpiga Picha Wetu)

Na: Mwandishi Wetu
Zaidi ya wakazi 1000 wa Kanda ya Ziwa wamenufaika na matibabu bure hasa kwa upande wa upasuaji unaofanywa na Chama cha Madaktari wa Upasuaji Tanzania. 

Hayo yamebainishwa na Rais wa Chama cha Madaktari wa Upasuaji Tanzania, Dkt. Catherine Mung’ong’o wakati wa siku ya kuhitimisha zoezi la upasuaji lililofanyika kwa siku tano kuanzia tarehe 03 hadi 07 Juni 2019 katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando jijini Mwanza.

Alisema kuwa lengo la upasuaji huo ni kupunguza idadi ya wahitaji wa huduma ya upasuaji kwa wagonjwa wanaosubiri kwa muda mrefu toka Kanda ya Ziwa, nakuongeza kuwa zoezi hilo limefanyika kwa ushirikiano baina ya Chama hicho,  Madaktari wa Hospitali ya Rufaa ya Bungando na Madaktari wengine.

Dkt. Mung’ong’o  amesema kuwa huduma hii ya upasuaji inayotolewa na Chama cha Madaktari wa Upasuaji Tanzania imekuwa ikifanyika kila mwaka katika mikoa mingine huku ni ikiwa ni mara ya kwanza katika mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Kwa upande wake Kiongozi wa Chama hicho Kanda ya Ziwa ambaye ni Daktari Bingwa wa Upasuaji toka Hospitali ya Rufaa Bugando, Dkt. Olivia Kimario amesema kuwa zoezi hilo ni utaratibu uliowekwa na Chama cha Madaktari hao ambapo mwaka huu wamehudumia katika mikoa ya Mwanza , Shinyanga , Mara na Geita.

Katika hatua nyingine Dkt. Mung’ong’o amesema kuwa baada ya kukamilisha zoezi hilo la upasuaji kwa wagonjwa wanaosubiri kwa muda mrefu Chama hicho kitatoa huduma bure za upasuaji kwa wagonjwa wenye matatizo ya Mdomo Sungura litakalofanyika tarehe 10 na 11 Juni 2019 bila ya malipo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.