Na Grace
Semfuko,Maelezo.
Yapi Merkez inajenga Reli ya SGR awamu ya kwanza kutoka Dar Es
Salaam hadi Morogoro ambayo ujenzi wake umefikia asilimia 56 na awamu ya pili
kutoka Morogoro hadi Makutupora Mkoani Singida ikiwa imefikia asilimia 52 zote
zikiwa na urefu wa zaidi ya kilomita 722 na zinajengwa kwa gharama ya fedha za
ndani shilingi Trilioni 7.2.
Hayo yalibainishwa na Waziri wa Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano
Mhandisi Isack Kamwelwe wakati akizindua Safari ya kwanza ya majaribio ya Treni
ya Wahandisi kwenye eneo la Soga lililopo Kibaha Mkoani Pwani.
Injinia Kamwelwe alisema mpango wa sasa wa Serikali ni kuwa na
Seti tano za Treni za SGR zitakazokuwa
na behewa nane za abiria, mpango ambao unalenga kuimarisha sekta ya usafirishaji wa reli.
“Ndugu zangu Watanzania, leo hii tumezindua majaribio ya njia ya
reli yetu, hii inamaana kwamba tupo katika mipango ya kuhakikisha reli
inakamilika kwa wakati, tumetembea kilomita 20 za majaribiop, reli ni salama kabisa,
haina kikwazo,sasa tumeanza mchakato wa kununua vichwa vya treni 22 na mabehewa
yake 60 ya Abiria na 1,430 ya Mizigo” alisema Waziri Kamwelwe.
Nae Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania TRC Masanja
Kadogosa amesema zoezi la majaribio ya awali ya treni ya wahandisi ni hatua
muhimu ya kuhakikisha reli hiyo inapitika bila kikwazo kwani inakagua na kuimarisha
miundombinu ya reli hiyo.
Alisema zoezi hilo la awali limekuja kufuatia kukamilika kwa
baadhi ya maeneo ya kupita treni kuanzia Soga Wilayani Kibaha Mkoani Pwani,
kuelekea Morogoro na kuongeza kuwa treni rasmi kwa ajili ya kupita reli hiyo
itawasili hivi karibuni.
Zoezi la majaribio ya uendeshaji wa Reli ya kihandisi
ulishuhudiwa na Waziri Kamwelwe, Maafisa wa Shirika la Reli Tanzania TRC pamoja
na Waandishi wa Habari ambao walitembea na treni hiyo kwa kilomita 20.
No comments:
Post a Comment