Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein akizungumza na Uongozi wa Wizara ya Vijana Utamaduni Sanaa na Michezo Zanzibar, wakati wa mkutano wa Utekelezaji wa Bajeti na Mpango Kazi wa Wizara hiyo kwa mwezi wa Julai hadi Juni 2019, uliofanyika katika ukumbi wa Ikulu Zanzibar.23-8-2019.
RAIS wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameupongeza
uongozi wa Wizara ya Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kuwapa mwanga wa
kimaisha vijana na kusisitiza haja ya kuwaenzi na kuwaendeleza.
Hayo aliyasema leo, Ikulu mjini Zanzibar
alipokutana na uongozi wa Wizara ya Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo wakati
ilipowasilisha Mpango Kazi wa Julai 2018
hadi Juni 2019 sambamba na Mpango Kazi wa Utekelezaji kwa mwaka 2019/2020.
Alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
imefanya kazi kubwa katika kuhakikisha vijana ambao ndio kundi kubwa inawawekea
mazingira mazuri ya kujiajiri sambamba na kuwapa mafunzo ya ujasiriamali.
Hivyo, Rais Dk. Shein alisisitiza haja kwa Wizara
hiyo kuendelea kuwasaidia vijana na kuwatunza kwani wana umuhimu mkubwa katika
jamii na ndio maana Serikali anayoiongoza inaendelea kuwawekea mikakati maalum
ya kuwaendeleza kimaisha.
Rais Dk. Shein alitoa pongezi kwa Wizara hiyo kwa
kuwasilisha vyema Mpango Kazi wao na kueleza kuwa vikao na utaratibu huo
umekuwa ukitatua mambo mbali mbali ambayo hatiamae kuleta tija.
Dk. Shein alieleza azma ya Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar ya kujenga uwanja mpya kwa ajili ya shughuli maalum za Serikali
zikiwemo sherehe za Mapinduzi.
Aidha, Rais Dk. Shein alieleza haja kwa Wizara
hiyo kuwa karibu sana na wasanii wa hapa nchini kwani wengi wao wanavipaji
vizuri na iwapo watawekewa mikakati maalumu ya kuwaimarisha watazidi kufanya
vizuri kitaifa na kimataifa.
Rais Dk. Shein alieleza kuwa tayari Kiswahili
kimeingizwa katika Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) hivyo, kuna
haja ya kukiendeleza na kukiimarisha hasa kwa Zanzibar kwani ndio chimbuko la
lugha hiyo na kusisitiza haja ya kukaa pamoja kati la Baraza la Kiswahili la
Zanzibar na uongozi wa vyombo vya habari vikiwemo vya Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar.
Nae Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee aliipongeza kazi nzuri ya uwasilishaji
iliyofanywa na Wizara hiyo huku akisisitiza haja kwa uongozi na wafanyakazi
kuendeleza mashirikiano.
Mapema Waziri wa Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo Balozi Ali Karume akiwasilisha
muhtasari wa utekelezaji mpango Kazi wa Wizara hiyo alipongeza jitihada
zilizochukuliwa za kuendeleza lugha ya Kiswahili ambapo kwa sasa imetangazwa
kuwa lugha ya nne rasmi itakayotumika katika mikutano ya (SADC).
Balozi Karume alieleza kuwa Wizara hiyo kupitia
Baraza la Kiswahili Zanzibar inachukua juhudi zikiwemo uanzishaji wa Kazi Data
ya wataalamu wa Kiswahili Zanzibar,Uchapishaji wa Makala za Kiswahili, vitabu
vya taaluma ya Kiswahili, lahaja pamoja na kuandaa makongamano ya Kiswahili.
Waziri huyo alieleza mafanikio ya wizara hiyo
ikiwa pamoja na kuyaunganisha Mabaraza ya Vijana kwenye fursa za uchumi,
kuongezeka idadi ya wanachama wa Baraza la Vijana na kufikia 3,276 pamoja na
kuwapatia vijana mafunzo ya kilimo, ufugaji, elimu ya ujasiriamali na uzalendo
kupenda nchi yao.
Aidha, alieleza kuwa Wizara imefanikiwa kuvipatia
vifaa vya muziki kikundi cha taarabu cha Taifa ambapo hapo awali vifaa vingi
vilivyokuwa vikitumiwa na kikundi hicho vilikuwa ni vya kukodi na kuazimwa
kutoka vilabu mbali mbali vya taarabu.
Katika kuhakikisha utamaduni, mila, silka za
wazanzibari zinaenziwa, zinaendelezwa kwa manufaa ya Taifa, Wizara kwa
kushirikiana na kikundi cha Taifa cha Maigizo na Kikundi cha Culture imeandaa maigizo maalumu
yatakayoelezea utamaduni halisi wa Mzanzibari.
Aliongeza kuwa jumla ya kazi za Sanaa 31 zikiwemo
nyimbo, maigizo, tenzi, mashairi,kasida pamoja na vipindi vya kuelimisha jamii
zikiwemo matangazo na hadithi fupi vimerekodiwa kupitia studio ya Filamu na
Muziki Rahaleo.
Pia, alieleza kuwa Wizara imefanikiwa kukamilisha
Sera ya Michezo na kuvisaidia vyama vya michezo kuandaa na kushiriki katika
mashindano mbalimbali ya kitaifa na kimataifa pamoja na kuandaa tamasha la
mazoezi ya viungo kitaifa.
Uongozi huo pia ulieleza mafanikio ya kukamilisha
matengenezo makubwa ya kiwanja cha MaoZedong na matengenezo madogo kwa kiwanja
cha Gombani na Amaan Stadium ambapo kwa upande wa viwanja vya Wilaya ya Kusini
Pemba vya “Kangani” na Kaskazini “Kishindeni” vimo katika hatua za uwekaji lami
katika sehemu ya kukimbilia.
Aidha, uongozi huo ulieleza jitihada wanazoendelea
kuzichukua katika kudhibiti filamu zisizo na maadili huku wakieleza juhudi
wanazozichukua katika kuhakikisha Kiswahili kinatumikakwa fasaha na usahihi
katika vyombo vya habari pamoja na jamii nzima kwa jumla.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment