Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein Azungumza na Uongozi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar.


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, akizungumza na Uongozi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, wakati wa mkutano wa Utekelezaji wa Bajeti na Mpango Kazi kwa mwezi wa Julai 2018 hadi Juni 2019, kwa Wizara hiyo uliofanyika ukumbi wa Ikulu Zanzibar.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ametoa pongezi kwa uongozi wa Wizara ya Elimu na kueleza juhudi za makusudi zilizochukuliwa na Serikali katika kuhakikisha Bajeti ya Wizara yake zinaimarika ikiwemo Wizara hiyo ili kukuza sekta ya elimu nchini.

Hayo aliyasema leo, Ikulu mjini Zanzibar alipokutana na uongozi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali wakati ilipowasilisha utekelezaji wa Mpango Kazi wa Julai  2018 hadi Juni 2019 sambamba na Mpango Kazi wa mwaka 2019/2020.

Dk. Shein alitumia fursa hiyo kutoa pongezi zake kwa kutekeleza vyema majukumu ya Wizara hiyo na kuwasilishwa vyema Mpango Kazi wake huku akisisitiza kuyatangaza mafanikio yaliopatikana katika Wizara hiyo.

Aidha, alieleza mafanikio yaliofikiwa katika kuendeleza na kukiimarisha Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), ambacho amesema hivi sasa kinatambulika duniani kote kutokana na mafanikio yaliopatikana na hatimae elimu imeimarika hapa Zanzibar.

Rais Dk. Shein aliongeza kuwa Chuo Kikuu hicho cha SUZA kimepata usajili kamili, huku hospitali ya Mnazi Mmoja nayo imepata hadhi ya kuwa hospitali ya mafunzo na kupata cheti maalum cha utambulisho.

Nae Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee aliipongeza kazi nzuri ya uwasilishaji iliyofanywa na Wizara hiyo na kusisitiza kuimarishwa kwa mashirikiano kati ya uongozi na wafanyakazi wa Wizara hiyo.

Mapema Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe.Riziki Pembe Juma katika taarifa yake alieleza utekelezaji wa malengo na vipaumbele ambavyo miongoni mwao ni ujenzi wa jengo jipya la Taasisi ya Karume ya sayansi na Teknolojia ambao umekamilika na Taasisi ya Maendeleo ya Utalii unaendelea na umefikia asilimia 90.

Aidha, alieleza kuwa ujenzi wa vituo vya Amali Daya na Makunduchi unaendelea vizuri ambapo ujenzi wa kituo cha Daya umefikia asilimia 65 na Makunduchi umefikia asilimia 55, pia, alieleza maendeleo ya ujenzi wa skuli mbali mbali za Unguja na Pemba.

Hivyo, Rais Dk. Shein alisisitiza haja ya kuengeza kasi katika ujenzi wa vituo vya amali vya Daya na Makunduchi ili kufikia malengo yaliyokusudiwa ikiwa ni pamoja na kumaliza kwa wakati uliokusudiwa.

Alieleza kuwa utoaji wa chakula kwa wanafunzi wa Skuli 27 za Msingi unaendelea Unguja na Pemba ambapo pia, jumla ya vituo 20 vya TUTU vimepatiwa jumla ya TZS 242,250,000 ikiwa ni fedha za ruzuku za kuendeshea vituo na skuli hizo.

Sambamba na hayo, Waziri Pembe alieleza kuwa jumla ya wanafunzi 1,720 wapya walipatiwa mikopo wakiwemo 1475 wa vyuo vya ndani na 245 kwa vyuo vya nje ya Tanzania huku akieleza kuwa Chuo cha Kilimo cha Kizimbani kimeunganishwa rasmina Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar mnamo Juni 24, 2019.

Pamoja na hayo, Waziri huyo alieleza baadhi ya changamoto zinazoikabili Wizara hiyo ambazo hata hivyo juhudi za makusudi zinaendelea kuchukuliwa na serikali kwa lengo la kuzitafutia ufumbuzi.

Mshauri wa Rais Pemba Dk. Mauwa Abeid Daftari alisisitiza haja kwa Wizara hiyo kuyatangaza mafanikio yaliyopatikana katika Wizara hiyo kwani imefanya mambo makubwa huku akiipongeza Wizara hiyo kwa uwasilishaji wa Mpango Kazi wao huo.

Nae Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dk. Idrissa Muslim Hija alieleza Mpango Kazi wa Wizara hiyo huku akitumia fursa hiyo kumpongeza Rais Dk. Shein kwa uongozi wake na kuipongeza Serikali kwa kuipa fedha za kutosha Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali huku akipongeza mashirikiano kutoka kwa wafanyakazi wa Wizara hiyo.

Aidha, aliahidi kulifanyia kazi suala la wanafunziwa Zanzibar wanaosoma nje ya Zanzibar ambao huja nchini kufanya tafiti mbali mbali kwa lengo la kuwasaidia ili kutekeleza vyema zoezi lao hilo.

Aidha, kwa upande wa Skauti uongozi wa Wizara hiyo ulieleza azma ya kuwarejesha vijana kuwa na maadili na uzalendo ikiwa ni pamoja na kurejesha na kuanza vikundi vya Skauti katika skuli za Zanzibar.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.