Habari za Punde

TAMASHA la tatu la Utalii na Michezo lafikia tamati

KIJANA Ali Khamis Abdalla akiwa nje ya gari yake baada ya kuibuka mshindi wa kwanza katika bonanza la Utalii, lililofikia tamati katika fukwe za Vumawimbi Wilaya ya Micheweni.
KIJANA Ali Khamis Abdalla akiwa ambaye ni mshindi wa kwanza katika bonanza la utalii Pemba

KIJANA Ali Khamis Abdalla (Wanne katika picha) Kutoka Tumbe Wilaya ya Micheweni, ambaye ameweza kujinyakulia Gari yenye Thamani ya Milioni 7 baada ya kuibuka mshindi wa kwanza katika mashindano ya Traithoni, ikiwa ni bonanza la Tatu utalii Kisiwani Pemba.
GARI ambayo amekabidhiwa bingwa wa bonza la utalii Kiswani Pemba
(Picha na Abdi Suleiman - Pemba.)

Na.Abdi Suleiman na Said Abdulrahman -Pemba.
TAMASHA la tatu la Utalii na Michezo Kisiwani Pemba, limefikia tamati kwa michezo mbali mbali ikiwemo trithon, mchezo wa kuogolea na resi za ngalawa, huko katika fukwe za vumawimbi wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kusini Pemba.

Mtamasha hilo liliweza kuvuta hisia za mashabiki wengi katika kisiwa hicho, hali iliyopelekea kuujaza ufukwe wa vumawimbi, huku likiwashirikisha wanamichezo wapatao 500 kutoka Zanzibar na Tanzania bara.

Baadhi ya wananchi wa wilaya ya micheweni walishindwa kuzuwia hisia zao, baada ya kumuona kijana wao Ali Khamis Abdalla kutoka Tumbe, kuongoza katika mbio za baskeli na kujinyakulia gari, huku wakishindwa kuamini kilichotokea.

Tamasha hilo ambalo limefungwa na Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Mgeni Hassan Juma, ambapo washindi mbali mbali waliweza kuzawadiwa zawadi

Washindi hao waliweza kuzawadi mbali mbali zikiwemo fedha taslimu, baskeli, Honda aina ya boxer na sunlj, huku mshindi wa mashindano hayo akijinyakulia Gari.

Kwa upande wa michezo ambayo ilishindaniwa na kutolewa zawadi katika ufungaji huo, ni pamoja na resi za baskeli, mpira wa miguu, resi za ngawala, uogeleaji, dufu pamoja na mbio za trithon.

Kwa upande mbio za trithon ambazo ziliwashirikisha vijana kutoka Unguja na Pemba, zikiwashirikisha washiriki 51, ambapo mshindi wa Kwanza ni kijana Ali Khamis Abdalla kutoka Tumbe Wilaya ya Micheweni, alijinyakulia gari aina Vtz pamoja na kikombe.

Mshindi wa pili wa mbio hizo ni Khamis Juma Khamis kutoka Dimani Unguja, ambapo yeye alijinyakulia Honda huku nafasi ya tatu ilichukuliwa na kijana Hassan Ame Tajo kutoka Dimani nae akajinyakulia Honda aina boxer, huku washiriki 10 wa mwanzo wakiahidiwa kila mmoja kuzawadiwa shilingi 50,000/.

Kwa upande upigaji dufu, mshindi wa Kwanza kilikuwa ni chuo Cha Almadrasatul Nurul-Islamiyya kutoka Micheweni ambapo kimejinyakulia kitita Cha shilingi 3000,000/ taslimu, nafasi ya pili ikichukuliwa na Almadrasatul Munir Islamiyya kutoka Kangani Mkoani Pemba ambapo nacho kikajinyakulia kitita Cha shilingi 2000,000/ huku nafasi ya tatu ilichukuliwa na Almadrasatul Thamaratul Jannar ya Fundo ikajipatia shilingi 1000,000/ huku walimu wa madrasa hizo walizawadiwa baskeli kila mmoja.

Kwa upande wa Mashindano ya uogeleaji mshindi wa Kwanza alikuwa ni Hamad Mattar Abdalla ambae alijinyakulia kitita Cha shilingi 1000,000/ pamoja na kikombe, mshindi wa pili ni Faki Omar Faki nae akajinyakulia shilingi 700,000/ na mshindi wa tatu alikuwa ni Ali Hamad Shaame akijichukulia kitita Cha shilingi 500,000/, ambapo katika mchezo huo waogoleaji wapatao 71 walishiriki Mashindano hayo.

Ama kwa upande resi za ngalawa zilizoshirikisha ngalawa 12, nafasi ya kwanza ikichukuliwa na Simba Salim Issa kutoka Mnarani Makangale ambae alijipatia kitita Cha shilingi 1000,000/ na kikombe, nafasi ya pili ikichukuliwa na Said Khamis Rashid alijipatia kitita Cha shilingi 700,000/ na mshindi wa tatu ni Ali Shaame kutoka Mnarani akajinyakulia shilingi 500,000/ huku washiriki waliosalia wakiahidiwa shilingi 100,000/.

Kwa upande wa mbio za marathon upande wa wanaume nafasi ya kwanza ilichukuliwa na kijana Nelson Mbuya kutoka JKU ambae alijipatia kitita Cha shilingi 800,000/, nafasi ya pili ikachukuliwa na Ali Malik Mohammed na kujinyakulia shilingi 700,000/ na nafasi ya tatu ilichukuliwa na Mohammed Ramadhani Mgeni kutoka KMKM ambae alijipatia kitita Cha shilingi 400,000/.

Kwa wanawake ambapo washiriki walikuwa ni wawili tu mshindi wa Kwanza alikuwa ni Rosemary Gusta kutoka KMKM, ambae alijipatia kitita Cha shilingi 400,000/, huku nafasi iliyosalia ikichukuliwa na Asha Abdalla Khatib ambae na akipata shilingi 300,000/.

Kwa upande wa mchezo wa mpira wa miguu ambayo ilishirikisha vilabu 8 vya mchezo huo, mshindi ilikuwa ni timu ya Mwenge kutoka Wete, ilijipatia kikombe pamoja na fedha taslim shilingi 3000,000/, mshindi wa pili akizawadiwa fedha taslim shilingi 2000,000/, huku vilabu vilivyobakia wakiahidiwa mipira ya kuchezea kila timu.

Akitoa nasaha zake Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Mgeni Hassan Juma,  alisema Zanzibar ilikuwa na ndoto ya kuanzisha mashindano ya trithon jambo ambalo sasa limetimia kwa upande wa Kisiwa Cha Pemba.

Alisema kufanyikwa mashindano hayo ni kielelezo tosha cha kuibua vipaji vya wachezaji mbali mbali ya vijana, hali ambayo inaweza kuhamasisha vijana kujiingiza katika sekta ya utalii.
“Kwa sasa michezo ni ajira na imekuwa ikiajiri vijana wengi na kutoka sehemu mbali mbali duniani, hivyo vijana kutumia nafasi hii ya michezo kujitangaza kwenu”alisema.

Tamasha hilo ambalo lilifunguliwa rasmi na Rais Mtaafu wa awamu ya pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Alhaj Ali Hassan Mwinyi mwishoni mwa wiki iliyopita, ambapo hapo Jana limefungwa na Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Mgeni Hassan Juma, michezo mbali mbali iliweza kufanyika.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.