Habari za Punde

Msaada wa Huduma za Kisheria wapokelewa kwa mikono miwili




Na Raya Hamad - WKS

Ø   Wananchi waridhishwa na utaratibu
Ø  Wasema ni hatua muafaka kukomesha udhalilishaji

HATUA ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ya kuanzisha Utaratibu wa Utoaji wa Huduma za Msaada wa Kisheria na Kurahisisha Upatikanaji wa Haki kwa wenye mahitaji imepokelewa kwa mikono miwili na wananchi walio wengi, hasa wale wanyonge ambao hali zao za kipato ni duni au wenye uelewa mdogo wa taaluma ya masuala ya sheria.

Hali hiyo imebainika muda mfupi tangu Serikali kupitisha na kuanza kutekeleza Sheria  ya Msaada wa Kisheria, iliyowezesha kuanzishwa Idara ya Msaada wa Kisheria, iliyo chini ya Wizara ya Katiba na Sheria, ambapo wananchi wengi wameizungumzia hatua hiyo kuwa ni msaada mkubwa na wa kipekee kwa wananchi walio wengi Unguja na Pemba.

Zuwena Othman mkaazi wa Bumbwini Makoba anaielezea hatua ya kuanzishwa msaada wa kisheria na upatikanaji wa haki kwa wale wasiokuwa na uwezo imekuja katika wakati muafaka ambapo jamii imebadilika kwa kuongezeka watu wasiokuwa na huruma wala imani kwa wengine.

Zuwena anasema hivi sasa sehemu zote iwe mjini au vijijini watu wengi wamekuwa wajanja na kuna matukio mengi ya watu kudhulumiwa na wanaoathirika zaidi ni wale wasiokuwa na kitu, elimu au watu wakuwasimamia kuweza kupigania haki zao mbele ya Mahakama na vyombo vyengine vya kutoa haki.

“Kwa hatua hii Serikali imefanya jambo zuri na la maana… Ni mambo ya kawaida sasa kujitokeza wajanja kuwahadaa wanyonge kuwaibia ardhi  nyumba, na hata baadhi ya wanaume kwa mfano kwa kujiona wana nguvu hutelekeza familia na kuwaacha watoto katika shida kubwa wakijua mwanamke hana pakukimbilia”, alisema Zuwena.

Kwa mtazamo wake iwapo Serikali itakuwa na utaratibu mzuri wa kuwawezesha wananachi 
wasiokuwa na uwezo au ndio walengwa wa msaada huo, kuweza kuwafikia watoaji wa huduma hizo, hata hivyo vitendo vya watu kudhulumiana kwa njia za hadaa vitapungua kwa kiasi kikubwa.

Kwa mujibu wa Sheria hiyo inayojuilikana kama Sheria ya Msaada wa Kisheria ya 2018, huduma za kisheria zinazotolewa ni utoaji wa ushauri, msaada wa uwakilishi wa kisheria na taarifa ambapo watakaonufaika ni watu ambao hawana uwezo wa kulipia huduma hizo za kisheria
Hatua za utoaji huduma hizo zimeanza baada ya kuundwa Idara ya Msaada wa Kisheria na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe Dkt Ali Mohamed Shein kwa kumteuwa Bi Hanifa Ramadhan Said kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Msaada wa Kisheria
 Idara ambayo inatekeleza majukumu yake kwa mashirikiano ya hali ya juu na taasisi mbali mbali za Umma zikiwemo Mahakama, Polisi na Chuo cha Mafunzo, vile vile, Idara inafanya mashirikiano makubwa na watoaji wa huduma za msaada wa kisheria na watu binafsi.
Mara baada ya kuundwa kwa Idara, utekelezaji wa majukumu yake umeanza kwa uzinduzi rasmi wa Idara hio ambapo uliwakutanisha baadhi ya watoa huduma za Msaada wa Kisheria pamoja na wanufaika wa huduma za msaada wa kisheria.
Katika uzinduzi huo Mkurugenzi Hanifa amesema kuwa uwepo wa Idara ya Msaada wa Kisheria Zanzibar ni kufungua ukurasa mpya katika kuhakikisha kuanzisha haki na wajibu kwa watoaji wa msaada wa huduma za kisheria kwa vigezo na viwango ili kwenda sambamba na vigezo vya kimataifa vya utoaji wa msaada wa kisheria.
 Anabainisha na kusema kuwa Katiba yetu ya Zanzibar ya mwaka 1984 inatambua na inahakikisha haki na inajumuisha suala la msaada wa kisheria kama msingi wa haki za binadamu kwa watu wote. Hivyo, ni wajibu wa watoaji wa msaada wa kisheria kuifuata miongozo ili kuweza kuisaidia jamii kupata msaada wa kisheria kwa ufanisi na kwa wakati.
“Niwaombe kama Watoa huduma za msaada wa kisheria msiishie hapa na juhudi zenu ambazo mmekuwa mkizifanya kwa muda wa siku nyingi, na muendelee na moyo huo huo katika kuwajengea uwezo wananchi katika kufahamu haki zao za msingi na wanapata huduma ipasavyo”. Alisisitiza  Hanifa
Mkurugenzi Hanifa amesema Idara ya Msaada wa Kisheria inathamini kazi kubwa inayofanywa na Wasaidizi wetu wa Kisheria na watoa huduma wengine wa msaada wa kisheria katika nchi.
Pia ametoa shukrani za dhati kwa Jeshi la Polisi kwa kazi ya utoaji wa msaada wa kisheria kupitia madawati ya kijinsia na njia nyengine ambazo zinasaidia kwa namana moja au nyengine kusaidia jamii.
Aidha, amewataka watoa huduma za Msaada wa Kisheria kuendeleza mashirikiano na kuahidi kuitunza Idara na kutekeleza kwa vitendo Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa ustawi bora katika kuhakikisha kila mtu anaestahiki kupata msaada wa kisheria anapata kwa kiwango kilicho bora na kwa wakati.
Sheria hiyo inazingatia maadili ya jamii na taratibu za kulinda faragha ya mtu wakati wa kumsaidia kupata huduma za kisheria na haki nyenginezo, ambapo imeeleza kuwa watu wenye kupatiwa huduma hizo watapatiwa kwa mazingira ya usiri.
Ikizingatiwa kuwa miongoni mwa wateja watakaoweza kupatiwa huduma hizo ni makundi maalum, wakiwemo watoto, mayatima, wazee, watu wenye kuishi na virusi vya ukimwi, mambo yanayohusu migogoro ya ardhi, urithi, unyanyasaji wa kijinsia, uangalizi na huduma za watoto pamoja na masuala ya uvunjifu wa haki za binaadamu
Sheria hii inakuja wakati Zanzibar ikikabiliwa na changamoto ya kukithiri kwa vitendo vya udhalilishwaji watoto, wanawake, watu wenye ulemavu pamoja na wimbi la talaka linalosababisha watoto kuingia katika mtihani mkubwa kimalezi, ambapo mara nyingi wazazi wa upande mmoja wa mwanamke ndiye anayebeba jukumu la ulezi na matunzo.
Ashura Suleiman mkaazi wa Kijichi Unguja, kwa maoni yake kuja kwa sheria hiyo kutawapa ahueni baadhi ya wazazi na wana familia ambao watoto wao hasa wasichana wadogo hupatiwa ujauzito na kukatiwa ndoto zao za kimaisha, huku wazazi hao wakipewa ushauri mbaya na baadhi ya wanajamii au mara nyengine hata wasijue la kufanya.
“Kuja kwa sheria hiyo ya msaada wa Kisheria itakuwa ni kimbilio la wazazi na familia zilizokumbwa na masahiba ya kudhalilishiwa watoto au wanafamilia, huko wataweza kusaidiwa na kushauriwa vizuri na kujua la kufanya lenye faida kwao”, alisema.
Katika kufanikisha utoaji wa huduma za kisheria kwa ufanisi wa hali ya juu umewekwa utaratibu maalum kwa watoaji wa msaada huo, ikiwemo taasisi au mtu anayetoa huduma hizo kuhakikishwa uwezo wake wa kufanikisha kazi hiyo, ili kuepuka ubabaishaji na utoaji wa huduma muafaka.
Kwa maana hiyo sheria hiyo inahitaji mtu, jumuiya au taasisi hiyo kwanza isajiliwe rasmi na Idara ya Msaada wa Kisheria, ambapo walioanishwa kuwa watakuwa watoaji wa huduma hizo ni pamoja na Mawakili, Wanasheria, Mavakili pamoja na wasaidizi wa sheria. 
Bila shaka hatua hiyo imechukuliwa kuhakikisha kwamba wanaotoa huduma za kisheria na haki kwa wananchi ni watu wenye weledi na uzoefu usionashaka yoyote, hasa ikizingatiwa kuwa baadhi ya watu wamekuwa na tabia ya kujivisha sifa za kitaaluma au kazi ambazo hawajazisomea au kuzifanya, lengo lao likiwa ni kujipatia vipato kwa njia ya udanganyifu.
Sheria hiyo ya Msaada wa Kisheria na inayorahisisha upatikanaji wa Haki imeliona hilo, na kuchukua hatua za kudhibiti hali hiyo isitokee, ambapo kwa mujibu wa sheria hiyo, mtu yoyote ambaye atafanya kazi kama mtoa msaada wa kisheria bila ya cheti cha usajili kinachotolewa na Mkurugenzi au kujifanya kama mtoa msaada wa kisheria wakati cheti cha usajili kimesitishwa au kwa makusudi kumzuia mtu asiombe msaada wa kisheria atakuwa anatenda kosa kisheria
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe Khamis Juma Mwalim katika kikao kilichopita wakati akiwasilisha bajeti ya Wizara hio alisema kuwa Wizara imejipanga na imefanya ziara ya mafunzo kuhusu Msaada wa Kisheria na kuwapatia vitendea kazi ili watekeleze majukumu yao kwa ufanisi.
Hivyo Waziri Khamis amewaomba watoaji wa huduma za msaada wa kisheria nchini na wanufaika wa msaada wa kisheria kuielewa vizuri na kuipa ushirikiano Idara mpya ya huduma za msaada wa kisheria ili kuhakikisha wanawasaidia wananchi wa taifa hili kuweza kupata haki zao kama ilivyokusudiwa.
Kwa upande wake, Hamduni Makame ambaye ni mkaazi wa Machui Wilaya ya Kati Unguja, akizungumzia utaratibu huo wa kuwasaidia kisheria wanaanchi wasiokuwa na uwezo anasema kuwa kwa hatua hiyo Serikali inastahili kupongezwa kwa sababu wamo wananchi wengi wanyonge wenye vilio vya muda mrefu, lakini hawana pa kuvipeleka kutokana na unyonge wao.
Ameeleza kuwa jambo la muhimu kwa Taasisi inayohusika na Utoaji wa Huduma za Msaada wa Kisheria kuhakikisha wasiokuwa na uwezo ndio wanaonufaika na utaratibu huo. Hivyo, ameomba kufanywa kila liwezekanalo kuwazuia wale wenye uwezo wa kujisimamia na kuendesha kesi na kupata haki zao wenyewe kutoingia katika utaratibu huo na kuwazuia walengwa.
“Wapo wajanja ambao wana uwezo mkubwa lakini hujiigiza na kujipatia huduma ambazo wahawastahili na hivyo kuwazuia wale wanaostahili kupata huduma hizo. Kwa kuwa Serikali imedhamiria kuwasaidia wasiokuwa na uwezo wa kusimamia haki zao mbele ya sheria ni matumaini yangu kwamba wajanja hao hawatapewa nafasi”, alisema Makame.
Amesema kwamba wamo wananchi wengi ambao uwezo wao na mwamko wa kupigania haki zao ni mdogo, huku baadhi ya wananchi hao wanashindwa na hata nauli ya kuwawezesha kufika mahakamani, hivyo uamuzi huo ni jambo la kupongezwa kwa sababu umelenga hasa kuwakomboa wenye mahitaji.
Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Zanzibar ndugu George Joseph Kazi anasema kuwa jamii ielewe  kuwa azma ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar nikuahakikisha wananchi wote wanapata huduma stahiki za msaada wa sheria kutoka kwa watoaji wa huduma za msaada wa kisheria ambao  wanasifa zinazoitajika kwa  mujibu wa sheria 
“tulifanikiwa kupata Sera ya Msaada wa Kisheria kutokana na jitahada kubwa ya Serikali yetu kwa kushirikiana na wahusika mbali mbali wa maendeleo na mkiwemo na nyinyi watoaji wa huduma za msaada wa Kisheria. Hatimae mwaka 2018 tuliweza kupata Sheria na mwezi Agosti, 2019 tulipata Kanuni za Msaada wa Kisheria zilizotangazwa Rasmi katika Gazeti la Serikali na kupelekea watoaji wa huduma ya msaada wa kutambulika rasmi.
George amewasisitiza watendaji wa Idara ya Msaada wa Kisheria kuwa waadilifu wakati wakitekeleza wajibu wao na kukumbushia majukumu yao kuwa ni kutoa miongozo ya kisera kwa watoaji wa msaada wa kisheria, kusajili watoaji wa msaada wa kisheria, kumtaka mtoa msaada wa kisheria kutoa huduma ya msaada wa kisheria kwa mtu asiekuwa na uwezo
Pia Kuratibu, kufuatilia na kutathmini kazi za watoaji wa msaada wa kisheria na kutoa maelekezo ya jumla ya utekelezaji unaofaa wa program za msaada wa kisheria katika kiwango kilichowekwa na ubora wa huduma za msaada wa kisheria na Kumshauri Waziri kuhusu sera na mambo mengine muhimu yanayohusu kuimarisha utaoaji wa msaada wa kisheria.
Katibu George ameongeza kusema kuwa Idara ijikite zaidi katika kufanya tathmini na kuandaa taarifa za ufatiliaji na tathmini ya masuala ya msaada wa kisheria ikiwa ni pamoja na kufanya tafiti ya changamoto za utoaji na upatikanaji wa huduma za msaada wa kisheria.
Ni wakati muafaka sasa kwa watoaji wa huduma wa msaada wa kisheria kuzielewa vizuri kanuni kwa lengo la kuweza kufikisha elimu kwa walengwa ambao ni wataka huduma wa msaada wa kisheria  huku ikizingatiwa kuwa Serikali  ya Mapinduzi Zanzibar kupitia Wizara ya Katiba na Sheria Zanzibar  imefanikiwa kuwana miongozo mbali mbali ikiwemo Sera, Sheria, Kanuni na Mpango wa Utekelezaji inayosimamia sekta nzima ya msaada wa Kisheria.
Kwa kufahamu kuwa kwa miaka mingi iliopita kwa upande wa Zanzibar kulikuwa hakuna mfumo rasmi wa kitaasisi unaosimamia huduma za msaada wa kisheria hivyo kulikosekana Sera au Sheria ambayo ingeweza kusimamia vizuri na kwa ufanisi huduma za msaada wa Sheria.
Kila mmoja atimize wajibu wake katika kuhakikisha jamii inapata msaada wa kisheria ili tuwe na jamii yenye kuelewa sheria na kuweza kudumisha utawala wa sheria, watowaji wa msaada wa kisheria hawana budi kuipa mashirikiano Idara hii ili iweze kufikia malengo yake hatua ambayo ni utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.