Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Ali Mohamed Shein kulia Mhe.Mohammed Ali Musabah,Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara na Wenyeviwanda wa Ras Al Khaimah na Waziri wa Ardhi Maji Nyumba na Nishati Zanzibar Mhe.Salama Aboud Talib, wakimasiliza Meneja wa Mamlaka ya Maendeleo ya Utalii wa Serikali ya Ras Al Khaimah Bi.Navritu Rai na Viongozi wa Kampuni za Uwekezaji, Jumuiya ya Wafanyabiashara na Wenye Viwanda pamoja na Mamlaka za Vitega Uchumi wa Ras Al Khaimah, hafla hiyo imefanyika katika Ukumbi wa Hotel ya Waldorf Astoria Ras Al Khaimah)
VIONGOZI wa Kampuni za Uwekezaji, Jumuiya ya Wafanyabiashara na Wenye Viwanda pamoja na Mamlaka za Vitega Uchumi za Ras Al Khaimah wameeleza azma yao ya kushirikiana na kuiunga Zanzibar ili izidi kupiga hatua katika kujiletea maendeleo endelevu.
Maelezo hayo waliyatoa wakati walipofanya
uwasilishaji wa shughuli zao za kimaendeleo za nchi hiyo kwa Rais wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein pamoja na Ujumbe
wake huko katika ukumbi wa Hoteli ya Waldorf Astoria, mjini Ras Al Khaimah.
Miongoni mwa viongozi hao ni pamoja na viongozi
wa Jumuiya Wafanyabiashara na wenye Viwanda wa Ras Al Khaimah ambapo Msaidizi Mkurugenzi Mkuu wa Jumuiya
hiyo Bi Eiman Darwish Alhayyas alieleza ukubwa wa Jumuiya hiyo yenye wanachama wapatao
139 pamoja na kazi inazozifanya.
Bi Eiman Darwish aliongoza kuwa Jumuiya yao hiyo
ina uzoefu wa miaka 52 katika kuwasaidia
wafanyabiashara pamoja na Mashirika na Makampuni ya biashara ambayo tayari yameweza
kupata mafanikio makubwa na kuweza kuimarisha na kukuza uchumi wa nchini hiyo.
Alisema kuwa shughuli za Jumuiya yao zimeipelekea
Ras Al Khaimah kuwa ni nchi inayoongoza kwenye uzalishaji wa viwanda katika
nchi za Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), hivyo walieleza haja kwa Zanzibar
kupata kuitumia fursa hiyo.
Uongozi huo waliikaribisha Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar kushirikiana katika maeneo mbali mbali yakiwemo maeneo mengine
mapya ya biashara yanayohusiana na usalama wa chakula, viwanda, utalii pamoja
na kilimo.
Ahmed Numan ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Masoko
na Mawasiliano katika Mamlaka ya Vitega Uchumi ya Ras Al Khaimah ( RAKEZ)
ambapo katika maelezo yake alieleza kuwa Ras Al Khaimah ni nchi inayotambulika
ulimwenguni katika masuala ya uwekezaji.
Alieleza kuwa katika nchi za Umoja wa Falme za
Kiarabu (UAE), Mamlaka hiyo ya (RAKEZ) ni moja kati ya Mamlaka ya Vitega Uchumi
inayokuwa kwa haraka sana na matunda yake yanaonekana ambapo tayari inamiliki
Kampuni 40500 za uwekezaji.
Aidha, Mkurugenzi huyo alieleza kuwa (RAKEZ)
inachangia asilimia 25 za Pato la Taifa la nchi hiyo ambazo zinatokana na
uzalishaji wa viwanda.
Akiwasilisha mada yake juu ya Mamlaka ya
Maendeleo ya Utalii ya Ras Al Khaimah Bi Navritu Rai yeye kwa upande wake
alieleza maendeleo ya Utalii ya Ras Al Khaimah sambamba na hatua
zinazochukuliwa ili kuuendeleza zaidi utalii.
Alieleza kuwa idadi ya watu wa nchi hiyo ni
345000 ambapo wanajivunia rasilimali walizonazo ambazo ndizo zinazoendeshea
utalii ambazo ni milima, fukwe, jangwa, chemchem za asili na mikoko ambavyo hivyo
ndivyo vivutio vyao vikubwa vya utalii.
Alieleza kuwa lengo lao ifikapo mwaka 2025 waweze
kuingiza watalii milioni 2.9 ambapo kwa hivi
sasa tayari wanapokea watalii milioni 1.2 wakiwa na lengo la kufikisha watalii
1.5 mwishoni mwa mwaka 2021.
Alisema kuwa njia kubwa wanazozitumia katika
kukuza utalii wao ni kubuni vivutio vipya kwa mfano shamba la lulu ambalo wafanyaji
shughuli za kutafuta lulu huzisarifu katika mapambo ya vitu mbali mbali ambavyo
ni vivutio vikuu vya watalii sambamba na upandaji wa mikoko ambayo ndege
hufanya makaazi yao ambayo pia, ni vivutio vya watalii.
Aliongeza kuwa Ras Al Khaimah ina bustani ya miti
ya asili ambayo imekuwa ni kivutio kimoja wapo kikubwa cha watalii.
Pia, kuwepo kwa michezo mbali mbali nayo imekuwa kivutio
cha watalii hasa michezo ya kuruka majabalini huku akieleza azma ya miradi
mingine wanayokusudia kuanzishwa ni kuanzisha utalii kwa michezo ya watoto.
Aidha, walieleza azma yao ya kuanzisha Chuo maalum
kwa ajili ya kuwafundisha watu njia tofauti za kujiokoa na majanga mbali mbali.
Pamoja na hayo, viongozi hao walieleza kuwa mbali
ya kuanzisha vivutio mbali mbali vinavyotokana na rasilimali walizonazo za
utalii pia, wanachukua juhudi za makusudi katika kuutangaza utalii wao kwa
kufanya maonyesho pamoja na wao kushiriki katika maonyesho katika nchi mbali
mbali ulimwenguni.
Pia, walieleza namna wanavyoendeleza miji mipya
ya kisasa inayotokana na kufukia bahari
kikiwemo kisiwa cha kitalii cha Marjan ambacho ni nembo muhimu katika maendeleo
ya Ras Al Khaimah ambacho kinapokea watalii 17200 kwa mwaka na bado wapo wageni
ambao hukosa nafasi kwa uhaba wa nafsi za makaazi.
Mkuu wa Utawala wa Kisiwa cha Marijani Abdulla Al
Abdool alieleza kuwa maendeleo katika kisiwa hicho yataendelea kukua kwani
tayari kuna wawekezaji kadhaa wa ndani na nje ya Ras Al Khaimah ambao
wameonesha nia ya kutaka kuekeza miradi mbali mbali.
Kwa upande wa Mamlaka ya Bandari ya Ras Al
Khaimah ni Shirika ambalo lina uzoefu mkubwa wa uendeshaji wa hsughuli za
baharini ikiwemo bandari ambapo huduma zao za mambo ya bahari ni ya daraja la
kwanza.
Bandari za Ras Al Khaimah zimekuwa kiunganishi
muhimu kwa nchi za Unoja wa Falme za Kiarabu (UAE) ambapo pia, ni miongoi mwa
vituo vinavyosambaza saruji na vifaa vyengine ujenzi katika nchi za Ghuba
ambayo ina Vyelezo 14 vya kufanyia matengenezo ya meli zinazoharibika.
Mkuu wa Mamlaka hiyo Adrian Pearson alieleza kuwa
shughuli zote za bandari katika nchi hiyo zinaendeshwa na wawekezaji wa kigeni
kwa asilimia mia moja.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein nae kwa upande wake alitumia fursa hiyo kutoa
pongezi kwa uongozi wa Kampuni, Jumuiya ya Wafanyabiashara na Mamlaka za Ras Al Khaimah na kuisifu azma
ya kuwepo kwa mashirikiano kati ya pande mbili hizo.
Nao viongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
walieleza kufarajika kwao na maelezo ya uwasilishaji wa shughuli za maendeleo
yaliofikiwa na Ras Al Khaimah na kuuliza masuala kwa ajili ya kupata ufafanuzi
zaidi juu ya mambo mbali mbali kwa lengo la lujifufunza sambamba na kwenda kuyafanyia
kazi zaidi nyumbani hatua kwa hatua.
Viongozi hao walipongeza mafanikio yaliofikiwa na
Ras Khaimah pamoja na mbinu wanazotumia katika kuendeleza siri ya mafanikio yao
kwenye maendeleo wanayoyapata hasa katika sekta ya uwekezaji na utalii ambazo
zimekuwa zikiimarika kila uchao.
Sambamba na hayo, viongozi hao walieleza kuwa miongoni
mwa maendeleo yaliyokwisha fikiwa na Ras Al Khaimah tayari Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar kwa upande wake imeshaanza kuchukua hatua za utekelezaji wa
mipango yake mbali mbali pamoja na mikakati maalum kwa kushirikiana na
wawekezaji wa ndani na nje ya nchi ili kuyafikia maendeleo kama hayo.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment