Habari za Punde

Waandishi Watakiwa Kutumia Lugha ya Kiswahili Fasaha Wanapoandia Habari.


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, akihutubia na kuufungua Mkutano Mkuu wa Wanachama wa Muungano wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), uliofanyika katika ukumbi wa mkutano wa Sheikh Idrisa Abdulwakil Kikwajuni Zanzibar.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amewataka waandishi wa habari nchini, kuondokana na utamaduni wa kufanyakazi kwa mazoweya, kwani sio sifa ya uandishi na utoaji mzuri wa habari.

Dk. Shein amesema hayo katika ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Muungano wa Klabu za Waandishi wa Habari (UTPC), uliofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdulwakil, Kikwajuni mjini hapa.

Alisema kuna umuhimu kwa waandishi kubadilika kwa kuzingatia kuwa taaluma ya habari inahitaji mawazo mapya, ubunifu na ushindani wenye tija.

Alisema ili mawazo mapya yaweze kupatikana, kunahitajika ufuatiliaji na utafutaji wa habari kutoka katika vianzio vinavyoaminika pamoja na kufanyiwa utafiti.

“Habari bora sio tu ile ambayo inavutia wateja kuisoma, bali ni lazima iwe ya ukweli na inayoandikwa kwa lugha sahihi inayokubalika”, alisema.

Dk, Shein aliwataka waandishi wa habari hususan wa magazeti kuwa makini na kutoegeme zaidi katika biashara na badala yake kuangalia sifa na ubora wa habari zinazohitaji kuchapishwa.

“……nilazima muwe makini katika magazeti msielemee kwenye biashara zaidi kuliko kuangalia sifa za ubora wa habari”, alisema.

Alisema wananchi wanapaswa kuelewa changamoto zinazoikabili Serikali katika utekelezaji wake wa kazi, hususan pale malengo yasipofikiwa, hivyo akavikumbusha vyombo vya habari wajibu wao wa kutoa habari kwa jamii.

Aidha, Dk. Shein alisema kunahitajika matumizi sahihi na mazuri ya lugha katika uandishi, ili taarifa ziweze kukubalika bila kuleta hitilafu baina ya mtoa habari na mahali pa uzuri wa habari yenyewe.

“Nataka msisitize juu ya kutumia lugha kwa ufasaha katika kusema na kuzungumza, namna ya kuchaguwa maneno mazuri katika maandishi”, alisema.

Alibainisha kuwa katika uanadishi kalamu inaweza kuwa nyenzo nzuri yenye kuinua hadhi ya mwandishi na kuleta tija iwapo atatumia kwa uangalifu, lakini pia inaweza kumuweka mwandishi katika nafasi asiyoridhia, pale asipoitumia vyema.

Aliwataka waadishi wa habari kufanyakazi zao kwa weledi na kuzingatia maadili yanayokubalika katika taaluma hiyo, bila ya kukiuka mila, silka na utamaduni kwa kuzingatia matumizi bora ya kalamu zao na ulimi.

Katika hatua nyengine, Dk. Shein alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekuwa ikichukuwa kila juhudi kuimarisha sekta ya habari kwa kuviimarisha vyombo vya habari vya Serikali kwa kuvipatia vifaa vya kisasa pamoja na mafunzo kwa watendaji wake.

Alisema kuna mabadiliko makubwa yaliofanyika katika Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) kwa kuzifanyia matengenezo studio pamoja na kuziwekea vifaa vipya vya kisasa vinavyoendana na mahitaji ya mfumo wa kidigitali.

Alisema Serikali imetayarisha mazingira mazuri na yenye hadhi Shirika la Magazeti kwa kulipatia vifaa vipya vya ofisi pamoja na kununua mtambo mpya wa uchapaji, hivyo kuliwezesha kuchapishwa hapa Zanzibar.

Aidha, Dk. Shein alikumbusha dhima kubwa iliyonayo vyombo vya habari kwa jamii, kwa kusema kuwa vinaijengea nguvu na uwezo jamii katika kuchangia maendeleo ya familia na Taifa kwa ujumla.

Alisema vyombo vya habari ni mkombozi wa jamii, na kubainisha kuwa watu wanaoishi bila kupata habari na kukosa kujua kinachoendelea katika Taifa, huwa wamo kizani.

Alisema kwa kuzingatia umuhimu wa jambo hilo, Serikali imeweka kifungu maalum katika Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, ikiwa ni hatua ya kuviwezesha vyombo hivyo kufanya kazi za kebila bughudha.

Alieleza kuwa kuna Jumuiya kadhaa za waandishi wa habari hapa nchini zinazofanya kazi kwa uhuru, miongoni mwao ni pamoja na ZPC,TAMWA, Pemba Press Club, WAHAMAZA na kadhalika.

Aidha, alisema kwa kutambuwa umuhimu wa habari, jukumu la waandishi wa habari limepewa uzito na kuelezwa vizuri katika mipango mikuu ya maendeleo, sambamba na kubainishwa katika Ilani ya Uchaguzi Mkuu wa 2015- 2020.

Rais Dk. Shein alivipongeza vyombo vya habari vya Serikali na binafsi nchini, kwa ushirikiano mkubwa na Serikali na kuvitaka kuendelezwe kwa kuyatangaza maendeleo mbali mbali yanayofanyika.

Hata hivyo Dk. Shein alisema kuna upungufu katika utoaji na usambazaji wa habari, hususan katika mambo mazuri yanayofanywa na Serikali, hivyo akawataka waandishi kuongeza juhudi sambamba na kuwataka watendaji wa Serikali kuwa tayari kuelezea mafanikio na changa moto zinazowakabili.

“Baadhi ya wakati wananchi huripoti kuilaumu Serikali kwa sababu hawajui jinsi gani Serikali yao inavyopanga na inavyotekeleza mipango yake kwa maslahi yao”, alisema.

Alisisitiza vyombo vya habari kupitia UTPC kuendelea kuyatangaza maendeleo na mambo mazuri yanayofanyika nchini, akitolea mfano ongezeko la Pato la Taifa na juhudi za Serikali katika kukuza uchumi wake.

Vile vile Dk. Shein aliwataka waandishi wa habari kuchangamkia fursa za kufanyakazi katika vyombo mbali mbali vya Kimataifa ikiwemo vya redio na magazeti, hatua aliyosema itafanikiwa tu kwa kujiimarisha na kuwa weledi katika kuandika na kuzungumza lugha ya Kiswahili kwa ufasaha.

“Na kuhimizeni mchangamkie fursa mbali mbali za ajira, wakati huu ambapo vyombo vya habari vinavyotumia lugha ya Kiswahili vimekuwa vikiongezeka na lugha hiyo kuzidi kukua”, alisema.

Alisema vyombo vya habari vinajukumu la kuendelea kuikuza na kuieneza lugha ya Kiswahili Ulimwenguni kwa kutumia lugha fasaha, na kubainisha kuwa Mjini Unguja ndio mahala inapopatikana.

Alisema mkutano wa wakuu wa Nchi za SADC uliofanhika hivi karibuni umeridhia kiswahili kuwa lugha ya Jumuiya, hivyo ni jukumu la waandishi wa habari kusisitiza utumiaji wa Kiswahili fasaha na kuepuka matumizi ya maneno yasio rasmi.

Aidha, Dk. Shein aliridhia ombi la UTPC la kusaidia maendeleo ya vyombo vya habari Zanzibar, akibainisha hatua ya Serikali ya kuthamini mchango mkubwa wa vyombo hivyo na kubainisha kuwa vitafanyakazi zake kwa uhuru.

Mapema, Waziri wa Habari, Utalii na Mambo ya Kale, Mahamoud Thabit Kombo alisema uamuzi wa UTPC kufanya mkutano wake mkuu Zanzibar ni uthibitisho kwa kiasi gani Jumuiya hiyo inavyolenga kuimarisha Muungano.

Alisema UTPC imefanya kazi kubwa ya kuunganisha Klabu za habari katika Mikoa yote, hivyo akaiomba Jumuiya hiyo kuangalia uwezekano wa kufanyia Pemba mkutano mkuu ujao, pamoja na gharama kubwa za uandaaji.

Nae, Balozi wa Sweden Nchini Tanzania, Mhe.Anders Sjoberg aliipongeza UTPC kwa kuwa kichocheo cha maendeleo ya kiuchumi nchini.

Aliipongeza kwa kuendeleza na kusimamia dhana ya kuwepo uhuru wa kujieleza na kupata habari pamoja na kusaidia mapambano dhidi ya rushwa nchini.

Aidha, Rais wa UTPC Ndg.Deogratias Nsokola, alisema kumekuwepo mafanikio makubwa kwa wadau wa habari nchini, kutokana na juhudi kubwa zinazochukuliwa na Jumuiya hiyo, hususan katika suala la upatikanaji wa mafunzo.

Alisema kwa nyakati tofauti Jumuiya hiyo ilifanikiwa kuvipatia fedha, vifaa, mafunzo kwa wanachama na asasi za kiraia.

Aliomba serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Bunge kuiangalia na kuifanyia marekebisho sheria ya makosa ya Mtandao pamoja na ile ya Huduma za vyombo vya habari, kwa mantiki kuwa inamapungufu.

Aidha, alitowa wito kwa wamiliki wa vyombo vya habari nchini kuwalipa wafanyakazi wao kwa wakati sambamba na kuwapatia stahiki zao ,ili kuepuka kutumika vibaya.

Abdi Shamna, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777476982. Fax: 024 2231822 
 E-mail: abdya062@gmail.com


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.