Habari za Punde

Makamu Mwenyekjiti wa CCM Zanzibar Dk.Shein Azungumza na Wazee wa CCM Wilaya ya Mkoani Pemba


MAKAMU Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein ameeleza azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kununua boti mpya ili kuwasaidia wananchi wakiwemo wazee wanaoishi katika visiwa vidogo vidogo vya Unguja na Pemba waweze kuvuka kwa uhakika.
Dk. Shein aliyasema hayo wakati alipokutana na wazee wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa Wilaya ya Mkoani huko katika ukumbi wa Skuli ya Mohamed Juma Pindua, iliyopo Wilaya ya Mkoani, Mkoa wa Kusini Pemba.
Rais Dk. Shein alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tayari imeshaanza mchakato huo ambao utakapokamilika utawasaidiaa kwa kiasikikubwa wananchi wanaoishi visiwani.
Makamo Mwenyekiti huyo wa CCM Zanzibar alivitaja visiwa sita ambavyo vimelengwa kupata boti hizo mpya na za kisasa ili ziwe msaada mkubwa kwao katika kuwasaida kuwavusha kikiwemo Kisiwa Panza, Makongwe, Fundo, Uvinje, Kokota na Tumbatu.
Aidha, Rais Dk. Shein amesisitiza haja ya kufanya kazi pamoja na wazee kwani ni watu muhimu sana katika jamii ambao bado mchango wao unahitajikakatika maendeleo ya kisiasa, kiuchumi na kijamii.
Alisisitiza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inathamini na inazijali juhudi za wazee walizozichukua hadi kupelekea kupatikana uhuru wa Tanganyika na uhuru wa Zanzibar kupitia vyama vya ASP na TANU.
Katika hotuba yake aliyoitoa mbele ya wazee hao wa CCM pamoja na viongozi wengine wakuu wa chama hicho Rais Dk. Shein alisema kuwa wazee walichukua juhudi za kujitolea na ndio maana uhuru kwa Tanzania Bara na Zanzibar ukapatikana hivyo, falsafa hiyo ni lazima ikaendelezwa kwani ina tija katika kujiletea maendeleo.
Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein alisema kuwa CCM ndio chama kinachowatetea wanyonge hivyo, ni lazima kitegemee nguvu za wanachama wake katika kufikia malengo yao waliyoyakusudia ikiwa ni pamoja na kuendelea kuongoza Dola.
Nae Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Abdalla Juma Mabodi alisema kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) bado kinaendelea kuwatunza, kuwaenzi na kuwathamani wazee na ndio maana wameingizwa katika taratibu zote za chama hicho.
Aliongoza kuwa hikma za kuwaenzi wazee zimeanza kabda ya Mapinduzi chini ya Jemedaru Hayati Mzee Abeid Amani Karume na hadi hivi leo hikma na busara hizo zinaendelea kutumika ikiwa ni pamoja na kuwatuza wazee wote wa Unguja na Pemba tena bila ya ubaguzi.
Nao Wazee katika taarifa yao walimpongeza Rais Dk. Shein na kueleza kuwa kitendo cha kwenda kukutana nao ni kielelezo kuwa anawajali na kuthamini juhudi zao ama mchango wao ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Aidha, wazee hao wa Mkoani walimpongeza Rais Dk. Shein kwa jinsi alivyoweza kudumisha amani na utulivu nchini jambo ambalo limemfanya aweze kutekeleza kwa ufanisi mkubwa maendeleo endelevu nchini.
Wakijataja baadhi ya maendeleo hayo ni pamoja na ujenzi wa barabara zenye viwango, upandishaji wa bei za karafuu, fedha za kila mwezi kwa wazee wa umri wa miaka 70 ambao miongoni mwao wanafaidika, ongezeko la fedha kwa wastaafu na uwekaji wa umeme na maji salama katika visiwa vya Unguja na Pemba na mengineyo.
Wazee hao pia, walitumia fursa hiyo kumpongeza Rais Dk. Shein kwa kuendelea kuyaenzi Mapinduzi matukufu ya Zanzibar kwa vitendo kwa kuendeleza kwa kasi matunda yake kama vile kuendeleza huduma za afya na elimu bure kwa wananachi.
Sambamba na hayo, nao wazee wa Makongwe walitoa pongezi zao za pekee kwa Rais Dk. Shein kwa kuwapelekea umeme katika kisiwa hicho ambapo hivi sasa wananchi wa kisiwa hicho wamekuwa wakifaidika na huduma hiyo muhimu katika maisha ya mwananadamu ikiwa ni pamoja na kufanya biashara zao kwa ufanisi mkubwa.
 Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.