Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu, kwa Waandisahi wa Habari na Wataalmu wa Afya Kutoka
Wizara ya Afya (Hawapo pichani) kuhusu Mkutano wa Mawaziri wa Afya na Ukimwi
kwa nchi za SADC, utakaofanyika kuanzia Novemba 04 hadi 08, 2019 katika ukumbi
wa Banki Kuu ya Tanzania Jijini Dar es Salaam, kushoto ni Mkurugenzi Msaidizi
Idara ya Habari-MAELEZO(Uratibu-Mawasiliano Serikalini) Bi. Zamaradi Kawawa wa
(kwanza) na Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dkt. Zainabu Chaula.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu akifafanua jambo kwa Waandishi wa Habari (Hawapo
pichani) kuhusu Mkutano wa Mawaziri wa Afya na Ukimwi kwa nchi za SADC,
utakaofanyika kuanzia Novemba 04 hadi 08, 2019 katika ukumbi wa Banki Kuu ya
Tanzania Jijini Dar es Salaam.
Na.Paschal
Dotto-MAELEZO.29-10-2019.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatarajiwa kuwa
mwenyeji wa Mkutano wa Mawaziri wa Sekta ya Afya na UKIMWI kutoka Nchi
Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) unaotarajiwa
kufanyika nchini kuanzia Novemba 04 hadi
08, 2019, katika Ukumbi wa Mikutano wa
Benki Kuu ya Tanzania jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika Mkutano na Waandishi wa Habari, Waziri wa
Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe.Ummy Mwalimu amesema
kuwa Mkutano huo utafunguliwa rasmi na
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu
Hassan, huku kauli mbiu yake ikiwa ni “Ushirikiano wa nchi za SADC ni nguzo kuu
kufikia Maendeleo Endelevu ya Sekta ya Afya na Mapambano dhidi ya UKIMWI.
Mhe. Ummy amesema kuwa katika Mkutano huo ambao kwa kiasi
kikukubwa utawakutanisha Mawaziri wa Afya na Watendaji Wakuu wa Idara za Afya
kutoka Nchi Wanachama wa SADC takribani 200 utakuwa na lengo la kujadili
masuala mbalimbali yanayoikumba sekta ya Afya Ukanda huo wa Afrika.
“Mkutano wa Mawaziri wa Sekta ya Afya na
UKIMWI unalenga kuangalia hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa Itifaki ya
Afya ya SADC ya mwaka 1999 na Mpango Mkakati wa Kanda kuhusu masuala ya Afya,
na pia kutakuwepo na ajenda za kuwezesha ujenzi mpya wa Sekta ya Afya kwa Nchi
Wanachama”, Alisema Waziri Ummy.
Alizitaja ajenda hizo kuwa ni pamoja na Magonjwa ya kuambukiza
yanayoziathiri nchi za SADC kama vile Kifua Kikuu, Malaria na UKIMWI; Masuala
ya lishe hususani uongezaji virutibisho na lishe ya makuzi kwa watoto, uzito
uliopitiliza na viribatumbo na huduma ya Lishe wakati wa majanga
Ajenda nyingine ni uimarishwaji wa Mifumo ya Afya ikiwemo
uimarishaji wa upatikanaji wa dawa, na upatikanaji wa takwimu za afya,
rasilimali watu, rasilimali fedha na Masuala ya ununuzi wa pamoja wa dawa na
vitendanishi ili kuongeza ufanisi na kupunguza gharama za manunuzi kwa nchi
wanachama, na hiyo itasaidia kuimarishwa kwa Sekta ya Afya huku Tanzania ikiwa
mbele kwenye masuala ya ununuzi wa dawa baada ya Bohari Kuu ya Dawa(MSD)
kuchaguliwa kuwa mzabuni katika ununuzi
wa dawa kwa nchi za SADC.
Aidha Waziri Ummy alisema kuwa katika kuimarisha afya ya Mama
na Mtoto suala la kuimarisha huduma za Afya kwa uzazi salama pamoja na chanjo
ya mtoto ni suala lingine ambalo linazikumba nchi hizo, kwa hiyo mjadala
utajikita katika suala hilo ili kulinda
Afya ya Mama na Mtoto hilo.
Kwa upande wa magonjwa ya mlipuko, majanga ya dharura
ikiwemo magonjwa ya milipuko kama vile
Ebola ambayo tayari yanazikumba nchi wanachama kama vile Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Uganda masuala haya yatajadiliwa kwenye mkutano
ili kupata ufumbuzi zaidi.
“Wizara yangu ikiwa ni Mwenyekiti wa Mkutano huu itasimamia
hoja zake katika masuala mbalimbali ya afya ikiwa ni pamoja na kuzishauri nchi
wanachama kuwekeza katika afya bora ambayo ndiyo msingi wa maendeleo na ukuaji
wa uchumi; nchi wanachama kuendelea kukabiliana na magonjwa yanayozuilika na
nchi wanachama kuwa na huduma za afya zenye usawa kwa watu wote”, Alisema
Waziri Ummy.
Mbali na kushiriki Mkutano huo, Mawaziri watapata fursa ya
kufanya ziara katika maeneo ya kimkakati ikiwemo; Kiwannda cha Viuadudu vya
Malaria cha Labiofam kilichopo Wilayani Kibaha, Mkoani Pwani tarehe 8 Novemba
2019, lengo la ziara hiyo ikiwa ni
kuzindua rasmi siku ya Malaria ya SADC na Kampeni ya Kitaifa ya Kupambana na
Malaria inayojulikana kama “Zero Malaria Starts with me” pamoja na kukitangaza kiwanda hicho kwenye nchi wanachama wa SADC
ili kupata soko la dawa zinazozalishwa kiwandani hapo, pia watatembelea Bohari
Kuu ya Dawa (MSD) kufuatia ushindi wake wa zabuni ya ununuzi, utunzaji,na
Usambazaji dawa na vifaa Tiba wa Nchi wanachama wa SADC.
No comments:
Post a Comment