Habari za Punde

Zanzibar Itaendelea Kuthamini Uhusiano na Ushirikiano na China.


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (kulia) akizungumza na  Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha  Kikomunisti cha China (CPC) Nd,Guo Yezhou (kushoto) wakati alipofika Ikulu Mjini Zanzibar leo akiwa na Ujumbe wake,[Picha na Ikulu] 25/10/2019.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa Zanzibar itaendelea kuthamini uhusiano na ushirikiano uliopo kati yake na Jamhuri ya Watu wa China sambamba na Chama chake cha Kikomunisti cha (CPC).

Rais Dk. Shein ametoa kauli hiyo leo Ikulu mjini Zanzibar wakati alipofanya mazungumzo na Naibu Waziri  wa Mambo ya Nje na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Kikomunisti cha China (CPC), Guo Yezhou.

Katika mazungumzo hayo, Rais Dk. Shein alisema kuwa huwezi kuyataja maendeleo ya Zanzibar bila ya kuihusisha Jamhuri ya Watu wa China kupitia Chama Cha Kikomunisti cha China (CPC), hiyo ni kutokana na uhusiano na ushirikiano mwema na wa kihistoria.

Rais Dk. Shein alisema kuwa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China imeifanyia mambo mengi Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwemo Zanzibar kwa uungaji mkono wake katika kuimarisha sekta za maendeleo.

Akitoa ushuhuda jinsi ya Jamhuri ya Watu wa China ilivyoisaidia Zanzibar katika kuimarisha sekta za maendeleo ikiwemo afya, elimu, viwanda, kilimo, sekta ya habari, miundombinu, michezo na mengineyo Rais Dk. Shein alisema kuwa nchi hiyo ni marafiki wa kweli kwani imeanza ushirikiano mara tu baada ya Mapinduzi matukufu ya Januari 12, 1964.

Aliongeza kuwa mbali ya Serikali ya China kusaidia sekta hizo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa kiwanda cha Sukari Mahonda, Kiwanda cha Sigareti Maruhubi, Viwanda vyenginevyo pia, nchi hiyo imeleta Mapinduzi makubwa katika sekta ya elimu kwa kutoa nafasi nyingi za masomo nchini mwake.

Alieleza kuwa kubwa kuliko yote hayo ni ukarabati mkubwa wa Hospitali ya Abdalla Mazee Mkoani Pemba, Ukarabati wa uwanja wa Mao Zedong pamoja na ujenzi wa uwanja wa ndege Terminal III.

Aidha, Rais Dk. Shein alimueleza kiongozi huyo haja ya kukuza ushirikiano uliopo kati ya  Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama Cha Kikomunisti cha China (CPC) pamoja na Serikali mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kama ulivyofanywa na waasisi wake Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Mwenyekiti Mao Zedong.
Alieleza kuwa ushirikiano huo ulianza tokea mwanzo wa vyama vya ASP, TANU na hatimae kuja kwa CCM na kueleza urafiki mzuri uliooneshwa na viongozi wa pande mbili hizo kwa kutembeleana ambao umekuwa ukiendelezwa hadi hivi leo.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein alitumia fursa hiyo kutoa shukurani zake kwa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kupitia Chama cha Kikomunisti cha China (CPC)  kusaidia ujenzi wa Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Julius Nyerere kinachojengwa Wilaya ya Kibaha Mkoni Pwani.

Dk. Shein alitoa pongezi na salamu kwa Rais wa Jamhuri ya Watu wa China na Mwenyekiti wa (CPC) Xi Jinping kwa kuendelea kuiunga mkono Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwemo Zanzibar.

Rais Dk. Shein alisema kwamba hatua ya ujenzi wa chuo hicho kupitia Chama cha Kikoministi cha China (CPC) ambacho ndicho kinachojenga zinaendeleza uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo baina ya Jamhuri ya Watu wa China na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Nae Naibu Waziri wa Mambo ya Nje ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Kikomunisti cha China (CPC) Guo Yezhou alitoa pongezi kwa mapokezi mazuri aliyoyapata yeye na ujumbe wake tokea walipowasili nchini Tanzania.

Alisema kuwa miongoni mwa lengo la ujio wake ni kuendeleza uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya Jamhuri ya Watu wa China na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwemo Zanzibar huku na yeye akitumia fursa hiyo kutoa salamu za Rais Xi Jinping kwa Rais Dk. Shein.

Naibu Waziri huyo wa Mambo ya Nje ambaye pia, ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha (CPC), alimueleza Rais Dk. Shein kuwa chuo hicho ni kwa ajili ya kutoa mafunzo ya uongozi kwa nchi sita zenye vyama vya ukombozi vilivyoshirikiana na (CPC) ambavyo ni (CCM), (ANC), (ZANU-PF), (FRELIMO), (MPLA) na (SWAPO) cha Namibia.

Kiongozi huyo alimueleza Rais Dk. Shein kuwa kutokana na China kuthamini juhudi za Tanzania ilizozichukua katika kuiunga mkono nchi hiyo ndipo Rais Xi Jinping alitoa tunzo kwa Waziri Mkuu Mstaafu Dk. Salim Ahmed Salim hivi karibuni ikiwa ni kutambua mchango wake mkubwa katika kuiwezesha China kuwa mwanachama wa Umoja wa Mataifa (UN).

Pia, Kiongozi huyo alimuhakikishia Rais Dk. Shein kuwa China itaendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha miradi mbali mbali ya maendeleo na kupongeza miradi ambayo tayari imeshakamilika huku akisisitiza kuwa bado nchi hiyo itaendeleza hatua zake za kuisaidia Zanzibar ikiwemo kuleta wataalamu wakiwemo madaktari kutoka Jimbo la Jingsu.

Alisisitiza kuwa Chama cha (CCP) kitaendeleza uhusiano na ushirikiano wake na Chama Cha Mapinduzi kwani vyama hivyo vina historia kubwa ambayo kuna kila sababu ya kuiimarisha ambapo katika ujumbe wake alifuatana na Balozi mdogo wa China Xie Xiaowu ambapo pia, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Abdalla Juma Mabodi alishiriki.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.