Habari za Punde

Zanzibar Kutumia Drone Kumaliza Kabisa Malaria

Muongozaji ndege isiyo na rubani  kutoka Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA) akijiandaa kurusha ndege ya kunyunyiza dawa ya kuulia viluilui vya Malaria katika uzinduzi uliofanyika bonde la Cheju.

Na Khadija  Khamis-Maelezo  Zanzibar.
Juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuhakikisha maradhi ya Malaria kabisa zinaonyesha kuleta mafanikio baada kuzinduliwa kampeni ya unyunyizaji dawa katika maeneo yanayozalisha viluilui vya maradhi hayo kwa kutumia ndege isiyo na rubani (drone). 
Akizindua kazi za unyunyizaji dawa ya kuulia viluilui kwenye mashamba ya mpunga bonde la Cheju, Waziri wa Afya Zanzibar Hamad Rashid Mohamed amekipongeza Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA)  kwa kushirikiana na Kampuni ya DJI ya China kutumia Teknologia ya drone  kumaliza malaria Zanzibar .
Amesema ndege hiyo itarahisisha kuyafikia maeneo yote ya Zanzibar yatakayo onekana bado kunamazalia ya viluilui vya mbu wa Malaria hasa maeneo yanayotuwama maji wakati wa mvua yakiwemo mashamba ya mpunga.
Alisema malaria kwa Zanzibar yameondoka lakini wilaya ya kati bado malaria ipo kutokana na kuwa na maeneo mengi yenye mazalio ya viluilui katika mashamba ya mpunga  
Aidha aliwataka wananchi kutowa ushirikiano katika kazi za unyunyizaji wa dawa ya kuulia viluilui katika maeneo mbali mbali ili kupiga vita maradhi hayo.
"Wananchi muwe tayari kuwasaidia wataalamu wetu na kuzitunza ndege hizi ili ziweze kufanya kazi kwa mafanikio makubwa," alisisitiza Waziri wa Afya.  .
Alisema tumeomba msaada wa kupatiwa teknolojia ya  ndege isiyo na rubani hivyo jukumu la kuhakikisha chombo  hicho kinadumu na kufanyakazi kwa muda mrefu ni jukumu la wananchi wote .
Msaidizi Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Jamii Simai Moh’d Simai alisema hali ya malaria katika wilaya ya kati sio nzuri na takwimu za mwaka 2019 zinaonyesha jumla ya wagonjwa 41,223 waliochunguzwa 11,357 walionekana na malaria wagonjwa 262 waligunduliwa kuwa na vimalea vya malaria.
Alifahamisha kuwa vijiji vilivyoadhirika zaidi na ugonjwa huo ni Jumbi, Kiboje, Miwani, Ndijani, Mseweni,  Jendele, Mitakawani, Chwaka, Uzi,  N’gambwa,Cheju, Bambi na Tunguu .
Alieleza matarajio yake kuwa kutokana na mikakati iliopo kwa kushirikiana na Serikali kuu na kupatikana kwa ndege hiyo kazi ya kupambana na  viluilui vya malaria itakuwa rahisi.
Nae Yussuf Mo’hd  kutoka Chuo cha Taifa SUZA  alisema Teknologia  ya ndege isiyo Rubani  ( drone) ya unyunyizaji  dawa ya kuua viluilui vya malaria itarahisisha kufanya kazi kwa haraka katika eneo kubwa kwa muda mfupi kwani inauwezo wa kunyunyiza  zaidi ya hekta hamsini kwa siku .
Pia alisema kutumia teknelojia hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa kunusuru mpunga usiharibike kutokana na unyunyizaji  wa dawa kufanywa kwa utaalamu mkubwa.
Kampuni ya DJI ya nchini China imetoa ndege mbili za kunyunyiza dawa ya kuulia viluilui vya malaria na kazi hiyo inafanywa kwa pamoja na Taasisi ya Tanzania Flying Labs kwa kushirikiana na Idara ya Sayansi  ya Komputa na Tehama ya Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.