Habari za Punde

Uazishwaji wa Programu ya Lugha ya Kiswahili Utasaidia Kuongeza Fursa za Ajira Kwa Vijana wa Zanzibar.


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA) Mhe.Dk.Ali Mohamed Shein akihutubia wakati wa hafla ya Mahafali ya 15 ya Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA) yaliofanyika katika Ukumbi wa Dk. Ali Mohamed Shein Tunguu Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja. 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amesema ni muhimu kwa programu ya Ufundishaji wa Kiswahili kama lugha ya pili (TEKSOL), ikaanzishwa katika ngazi ya stashahada na shahada, ili vijana wengi zaidi waweze kujifunza namna ya ufundishaji wa lugha hiyo.

Dk. Shein amesema hayo katika sherehe za mahafali ya 15 kwa Wahitimu wa mwaka wa masomo 2018/2019 ya Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA), zilizofanyika katika Ukumbi wa Dk.Ali Mohamed Shein Campus ya Tunguu, Mkoa wa Kusini Unguja.

Dk. Shein ambae pia ni Mkuu wa Chuo hicho alisema uanzishaji wa Programu ya Ufundishaji wa Kiswahili kama lugha ya pili, utasaidia kuongeza fursa za ajira kwa vijana wa Zanzibar kwenda kufundisha Kiswahili ndani na nje ya nchi; wakati huu ambapo nchi mbali mbali duniani zimeanza kufundisha lugha hiyo katika vyuo Vikuu.

“Kwa hivyo, sisi ambao lugha ya Kiswahili ndio lugha yetu mama, lazima tuwe mbele na tuamini kuwa tuna uwezo mkubwa zaidi wa kufundisha Kiswahili fasaha, kwani ndicho kilichotulea na kutukuza na vile vile, tunaujua utamaduni wake”, alisema.

Aliwataka  Wahitimu  wa masomo hayo kufanya  kila juhudi kutafuta  fursa za kwenda kufundisha Kiswahili katika nchi mbali mbali duniani, ikiwemo za Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).

Aidha, aliwataka wahitimu kuchukua  hatua ya kuwasiliana na taasisi zinazohusika pamoja na kufuatilia katika mitandao, ili kuhakikisha wananufaika  na fursa hizo.

Alieleza kuwa katika hafla ya ufunguzi wa Kongamano la Kimataifa la Kiswahili lililofanyika hivi karibuni, alifurahia hatua ya kukabidhiwa idadi kubwa ya tasnifu za wataalamu waliohitimu katika fani za lugha ya Kiswahili katika ngazi ya Shahada ya Uzamivu na Shahada ya Uzamili kutoka vyuo vikuu mbalimbali  nchini, ikiwemo SUZA.

Alisema kuwepo kwa hazina kubwa ya wataalamu wenye shahada za juu katika Kiswahili, ikiwemo Tasnifu 17 za Uzamivu (PhD) na 95 za Uzamili (Masters),  kunapaswa kwenda sambamba na maandalizi ya kuanzisha Skuli ya Tafsiri na Ukalimani, akibainisha  hatua hiyo italiwezesha Taifa kuandaa wataalamu waliobobea wa fani za tafsiri na ukalimani  katika masuala ya mawasiliano ikiwemo mikutano ya Kimataifa.

Aidha, alitaka juhudi zifanyike kuimarisha Skuli ya Kiswahili na Lugha za Kigeni ili  ifikie kuwa Kitivo Kikuu na kuifanya Zanzibar kuwa  Kituo Bora,  “Center of Exellence”.

“Ni muhimu tuongeze vifaa na vivutio vyengine ili kuwafanya wageni wanaotaka kujifunza lugha ya Kiswahili washawishike kujiunga na taasisi hiyo,  tuandae mipango imara, tuwe na mikakati madhubuti pamoja na kutafuta nyenzo, kwani wazee walisema mti hawendi ila kwa nyenzo” alisema.

Katika hatua za kukiimarisha chuo hicho, Dk. Shein alisema uanzishaji wa programu mbali mbali umezingatia mahitaji ya mipango ya maendeleo na soko la ajira, hatua inayokwenda sambamba na uanzishaji wa Skuli mpya ya Utibabu wa Meno, na kubainisha kuwa  ni jambo linalofurahisha.

Alisema kwa mnasaba na jambo hilo, Serikali imeamua kuanzisha Taasisi ya Masomo ya Ubaharia pamoja na kukiunganisha Chuo hicho na Skuli ya Kilimo, kwa  kuzingatia upungufu mkubwa wa madaktari wa meno pamoja na kuzindeleza taaluma za uuguzi na ukunga.

Aidha, alisema kuanza kwa mafunzo ya Shahada ya Udaktari wa Meno na Shahada ya Uuguzi na Ukunga katika mwaka huu wa masomo ni hatua nyengine muhimu ya maendeleo katika kuimarisha huduma za afya nchini.

Alieleza kupatikana kwa wataalamu wa fani hiyo kutasaidia sana katika kukabiliana na matatizo ya maradhi ya meno yanayowasumbua wananchi.

Vile vile,alisema wataalamu wa fani ya uuguzi na ukunga watatoa mchango mkubwa katika kuinua huduma hizo na kufanikisha  utekelezaji wa malengo ya serikali katika kukabiliana na vifo vya mama wajawazito na watoto wakati wa kujifungua.

Dk. Shein aliitaka SUZA kuandaa utaratibu wa kutathmini mitaala yake na kuangalia ubora wa wahitimu wake, katika kuyamudu majukumu yao kulingana na masomo waliyojifunza wakati wakiwa chuoni.

Alisema chuo kinapaswa kuendelea kubuni programu za masomo ambazo zitapunguza wahitimu kutegemea zaidi ajira kutoka Serikalini na badala yake kuweza kujiajiri wao wenyewe.

Alisema Serikali itaendelea kufanya kila linalowezekana kuwasaidia vijana wanaohitimu, ili waweze kuitumia elimu waliyoipata kujiajiri pamoja na kuwapatia mikopo ili kuendeleza maisha yao. Aidha, alisema Serikali inaendelea na juhudi kukamilisha taratibu zitakazowezesha kuwa na fedha za kutosha ili kuwawezesha wananchi kiuchumi.

Rais Dk. Shein aliwakumbusha wahitimu hao kuwa  elimu ni bahari isiyo na mwisho, hivyo akawataka  wasitosheke na hatua waliyofikia kwa kutambua kuwa jamii ina matarajio makubwa kwao.“Ni vyema mkaitumia elimu yenu vyema kwa faida yenu na jamii, huku mkizingatia uadilifu, uzalendo, maadili mema na malezi mema tuloachiwa na wazee wetu”, alisema.
Aliwataka wahadhiri na wafanyakazi wa SUZA  kuendelea kutimiza wajibu wao  kwa kufanya kazi kwa bidii  ili kuhakikisha  wanafunzi wanahitimu wakiwa wamebobea na wenye nidhamu, sambamba na kuuhimiza Uongozi kusimamia Sheria ya Utumishi wa Umma namba 2 ya mwaka 2011.
Aidha, aliwataka wahadhiri  kuzingatia uwiano wa kiwango bora cha elimu na namna ya kutathmin uwezo wa watahiniwa, pamoja na utoaji wa alama za ufaulu kwa weledi ili kuepusha migongano, jambo ambalo litateremsha kiwango cha elimu inayotolewa.

Katika hatua nyengine, Dk. Shein aliwataka wahitimu wa ngazi ya Uzamivu (Phd), kufanya juhudi katika kufanya utafiti na kuandika makala za kitaaluma  pamoja na kuandika vitabu,  ili hatimae wafikie daraja la uprofesa. 

Alisema Serikali imekuwa ikitenga bajeti kubwa ya fedha  kugharamia huduma za elimu ikiwemo mishahara ya wahadhiri na wafanyakazi wa chuo pamoja na uimarishaji wa miundo mbinu ya elimu ikiwemo vitabu na ujenzi wa majengo ya kisasa na ubadilishaji wa sera, ili kuhakikisha  wanafunzi wanapata nyenzo bora za kujifunzia.

“Sasa hivi kujifunza kumerahisishwa na matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) hivyo, itumieni vizuri teknolojia hiyo, ili ikuzidishieni maarifa na ujuzi na wala msiitumie kwa mambo yasiyofaa”, alisema.
Alisema mabadiliko ni jambo la lazima katika maisha ya binadamu na mazingira yake na kubainisha jukumu la Serikali katika kuwaletea maendeleo watu wake, akibainisha SUZA ndio hazina na uti wa mgongo katika kufikia maendeleo ya Zanzibar.

Dk. Shein alitoa shukurani kwa viongozi, wahadhiri na wafanyakazi wote  waliofanya kazi nae  tangu alipokabidhiwa dhamana ya Mkuu wa Chuo hicho mwaka 2010, wakiwemo wale ambao wamefariki, kustaafu na wengine kukabidhiwa majukumu mengine.

Nae, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Riziki Pembe Juma alitoa pongezi kwa Serikali kwa mafanikio makubwa yaliofikiwa katika kukiendeleza Chuo hicho na hivyo kuwa chachu katika maendeleo ya kijamii na kuchumi.
Aidha, Makamo Mkuu wa SUZA, Zakia Abubakar alisema kuendelea kufanya vizuri kwa wahitimu wa kike ni jambo la kupongezwa linaloonyesha matumizi mazuri ya uwezo wao katika masomo.

Alisema katika mahafali ya mwaka huu, wahitimu wa kike wameendelea kufanya vyema kwa kupata asilimia 54 dhidi ya asilimia 46 za wanaume, huku mwanafunzi bora wa jumla akiwa mwanamke.
Alisema chuo hicho kinakabiliwa na changamoto mbali mbali, ikiwemo ya ukosefu wa dahalia, hususan katika Campus ya Tunguu inayohusisha ukosefu wa maeneo mbali mbali ya utoaji wa huduma kitaaluma kwa wanafunzi.
Alisema jumla ya wahitimu 1,719 kutoka fani mbambali wamefaulu na kutunukiwa vyeti, stashahada pamoja shahada, hatua inayokifanya chuo hicho kufikisha jumla ya wahitimu 12,000 katika kipindi cha miaka 15 sasa.
Katika mahafali hayo ambayo yalihudhuriwa na Viongozi mbali mbali wa Kitaifa, akiwemo Makamo wa Rais wa Jamuhuri ya Mauungano wa Tanzania Dk. Mohamed Gharib Bilali na Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd, Rais Dk. Shein alikabidhi zawadi kwa wanafunzi bora katika ngazi za cheti, Stashahada na Shahada.
Abdi Shamna, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777476982. Fax: 024 2231822 
 E-mail: abdya062@gmail.com

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.