Habari za Punde

WANANCHI WA WILAYA YA MAGU WATAKIWA KUCHANGAMKIA FURSA UJIO WA CHUO CHA MIPANGO


Kamishna Msaidizi wa Idara ya Bajeti ya Serikali Bw. Pius Mponzi akizungumza wakati wa makabidhiano ya eneo litakapojengwa Chuo cha Mipango ya Maendeleo vijijini – IRDP lililopo katika kitongoji cha Kitumba, Halmashauri ya Wilaya ya Magu, Mkoani Mwanza.
Wananchi wa Kitongoji cha Kitumba kilichopo-Kisesa- Halmashauri ya Wilaya ya Magu mkoani Mwanza wakifuatilia matukio mbalimbali wakati wa hafla ya makabidhiano ya eneo la ujenzi wa Chuo cha Mipango na Maendeleo Vijijini, Jijini Mwanza.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha na Mipango-Mwanza)


Na Ramadhani Kissimba na Saidina Msangi, WFM, Mwanza.

Wakazi wa Wilaya ya Magu mkoani Mwanza, wametakiwa kuchangamkia fursa mbalimbali zitakazotokana na ujenzi wa  Chuo cha Mipango na Maendeleo vijijini kitakachojengwa  
katika Halmashauri ya Wilaya hiyo.

Hayo yalisemwa na Kamishina msaidizi wa Idara ya Bajeti ya Serikali -Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Pius Mponzi  wakati akipokea kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Fedha 

na Mipango, Bw. Doto James eneo lenye ukubwa wa ekari 21  lililotolewa na Halmashauri ya Wilaya ya Magu kwa ajili ujenzi wa chuo cha Mipango na Maendeleo Vijijini Tawi la  
Kanda ya Ziwa.


Bw. Mponzi alisema ujenzi wa chuo hicho utafungua fursa nyingi za kiuchumi kwa wananchi wanaozunguka maeneo hayo, hivyo kuwataka kuchangamkia fursa hiyo kwa kuwekeza katika miradi ambayo itawasaidia kuongeza kipato na kuwaletea maendeleo.

‘’Chuo hiki kwa sasa kinadahiri wanafunzi zaidi ya 3,000 katika Kampasi ya Mwanza, hivyo ni fursa nzuri hasa kwa wajasiriamali wadogo kubuni na kuanzisha biashara zitakazowasaidia kuondokana na umasikini’’ alisema  Bw.Mponzi.

Aidha Bw. Mponzi aliitaka Menejimenti ya Chuo hicho kuhakikisha ujenzi wa chuo hicho unaanza maramoja na kuhakikisha malighafi zote zitakazotumika katika ujenzi huo zinatumika ipasavyo pasipo ufujaji wowote.

“Ninawaagiza pia wakandarasi mtakaojenga chuo hiki kuhakikisha mnawatumia vijana wanaozunguka eneo la mradi kufanya kazi za ujenzi ili kuwapatia ajira vijana wa Halmashauri ya Magu.

Awali akizungumza kabla ya makabidhiano ya eneo hilo, Mkuu wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini, Prof. Hozen Mayaya alisema uongozi wa chuo uliamua kuanzisha 
kituo cha mafunzo katika Kanda ya Ziwa -Mwanza ili kuongeza kasi ya kutimiza lengo la Serikali la kuwaandaa watalaam wa kupanga na kusimamia utekelezaji wa mipango ya maendeleo katika ngazi mbalimbali hapa nchini na kusogeza huduma za chuo karibu na wananchi na wadau wa maendeleo.

Prof.Mayaya alisema Kituo cha Kanda ya Ziwa tangu kuanzishwa kwake mwaka 2011 kimekuwa kikiendesha shughuli zake katika majengo ya kupangisha, hivyo kupatikana kwa eneo hilo kutaondoa changamoto hiyo na kituo kujiimarisha zaidi katika kuwapatia elimu vijana wa Kitanzania wenye sifa za kusoma katika Taasisi za elimu ya juu.


Aidha Prof. Mayaya alisema Chuo cha Mipango kimejizatiti kujenga chuo bora zaidi na cha mfano katika Kanda ya Ziwa na kwa kuanzia yatajengwa majengo mawili  yenye thamani 
ya shilingi bilioni 2.1 yatakayokuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 1,220.


Akiwashukuru uongozi wa Wizara ya Fedha na Mipango na Uongozi wa Chuo hicho, Mkuu wa Wilaya Magu Dkt. Philemon Sengati, , alisema ujenzi wa chuo hicho utasaidia kufungua fursa mbalimbali za uwekezaji katika Wilaya hiyo 

na kuwakaribisha wawekezaji wengine kuwekeza katika Halmashauri ya Wilaya ya Magu kwa kuwa maeneo ya kuwekeza yapo ya kutosha na yenye mandhari nzuri.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.