Habari za Punde

WAZIRI MHAGAMA AKUNWA NA UTATUZI WA MIGOGORO YA KAZI KWA NJIA YA USULUHISHI

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama akisisitiza umuhimu wa kutatua migogoro ya kikazi kwa kutumia njia ya Usuluhishi wakati kikao kazi cha Tathmini ya utekelezaji wa Majukumu ya Tume ya mjini Morogoro, tarehe 19 Desemba, 2019
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama akimpongeza mmoja wa watumishi wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi nchini, wakati kikao kazi cha Tathmini ya utekelezaji wa Majukumu ya Tume ya mjini Morogoro,
Baadhi ya washiriki wa kikao kazi cha Tathmini ya utekelezaji wa Majukumu ya Tume ya Usuluhishi na Uamuzi nchini,wakifuatilia  kikao kazi cha Tathmini ya utekelezaji wa Majukumu ya Tume ya mjini Morogoro, tarehe 19 Desemba, 2019, kikao hicho kimewajumuisha Wasuluhishi na  Waamuzi wa migogoro ya kikazi na wasaidizi wa Tume hiyo.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama ameipongeza Tume ya Usuluhishi na Uamuzi nchini kwa kutekeleza agizo lake alilolitoa mwaka jana kwa Tume hiyo, ambapo aliiagiza Tume hiyo  kuwa na mpango mkakati wa Kuhakikisha kuwa migogoro ya kazi nchini inatatuliwa kwa njia ya Usuluhishi bila kufika katika ngazi ya maamuzi, kutokana na utekelezaji wa agizo hilo asilimia 86.73 ya migogoro ya kazi 9,646 iliyosajiliwa nchini imetatuliwa kwa njia ya usuluhishi bila kufika kwenye ngazi maamuzi.

Waziri Mhagama ameyasema hayo leo, tarehe 19, Desemba 2019,  mjini Morogoro,  wakati akifungua kikao kazi cha Tathmini ya utekelezaji wa Majukumu ya Tume kilichowakutanisha Wasuluhishi na  Waamuzi wa migogoro ya kikazi na wasaidizi wa Tume hiyo. Aidha, amefafanua kuwa njia bora ya kutibu mahusiano ya kiajira yaliyotetereka ni kupitia kumaliza mashauri kwa njia ya usuluhishi.

“Nawapongeza Wasuluhishi na Waamuzi wa mashauri ya kikazi, jitahidini mfanye kazi kwa uadilifu, kwani hata kwenye mashauri yaliyohitaji kutatuliwa kwa njia ya maamuzi asilimia 78 ya mashauri 5,131 ya maamuzi yaliyosajiliwa yamepata maamuzi,mmefanya kazi nzuri kwa kuvuka nusu ya mashauri, pia  mmepunguza malalamiko ya watumishi kupata haki zao ambazo zimekuwa zikipotezwa  na baadhi ya wajanja katika sekta ya ajira bila kuwa na huruma kwa watanzania wenzao ”  Amesema Mhagama

Mhe. Mhagama ameeleza kuwa kitendo cha Tume hiyo kutekeleza agizo lake la kuanzisha kitengo cha Usuluhishi na kuteua Mkurugenzi anayeratibu Kitengo hicho kunadhihirisha dhamira ya Tume hiyo ya kuhakikisha migogoro ya kikazi haizalishwi kwa kuwa huchochea kutumika vibaya kwa rasilimali muda kati ya mwajiri na Mfanyakazi hali inayopelekea kuchelewesha Maendeleo.
    
“Serikali ya Awamu ya Tano imeendelea kutekeleza miradi ya Maendeleo ya Kiuchumi na Kijamii ikiwemo kujenga viwanda, kujenga reli ya kisasa, kujenga bwawa la Nyerere litakalozalisha Umeme, Utekelezaji wa Miradi hii maana yake kuna ajira zinazotengenezwa hivyo tutarajie na migogoro ya kazi pia kuzalishwa, kwa mantiki hiyo Tume haina budi kuendana pia na  kasi ya maendeleo ili kuifanya nchi yetu kuwa mahala salama ya uwekezaji na ufanyaji wa kazi ” Amesisitiza mhagama.

Aidha, Mhe. Mhagama ameitaka Tume hiyo kuendelea kufanya utafiti kwa sekta   zote zinazoongoza kwa migogoro ya kikazi ili kubaini chanzo cha migogoro hiyo na kuandaa Mkakati Maalum wa kuishughulikia, kwa kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu Kupitia Tume hiyo  imepewa jukumu la kutatua migogoro na kuweka msisitizo wa kuimaliza migogoro.

“Nimepitia ripoti yenu inaonesha bado sekta ya Ulinzi binafsi inaendelea kuwa kwenye kundi linaloongoza kwa migogoro, lakini sekta ya Hoteli pia kila mwaka ipo kwenye kundi hilo, lakini ziko sekta nyingine kama sekta ya Ujenzi kwa mwaka huu imeondoka lakini sekta ya  Viwanda imeingia kwenye sekta zinazoongoza za migogoro japo si kwa kiwango cha juu, kwa kuwa tumejipambanua tunajenga uchumi wa viwanda lazima muwe na mpango kazi ili kuweka mazingira wezeshi kwa Taifa letu” Amesisitiza Mhagama

Awali akiongea katika kikao kazi hicho, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi, Shanes Nungu alibainisha kuwa Tume hiyo iliamua kutelekeza maagizo ya Mhe. Waziri Mhagama kwa kuboresha Mkakati Wa Mpango kazi Wa Tume ambao umesaidia kuwa na  mpango mkakati kwenye mtazamo Wa kupunguza migogoro  na unaolenga kumaliza migogoro, lengo nikutaka kutatua migogoro na kuweka msisitizo wa kuimaliza migogoro kwenye  sekta  zinazoongoza kuwa na migogoro mahala  pa kazi.

 "Wasuluhishi na Waamuzi wa mashauri ya Kikazi kwa pamoja wamekuwa wanajitahidi kumaliza na kuipunguza migogoro ya kikazi, kwani tumefanikiwa kumaliza migogoro hiyo kwa asilimia 86 kwenye hatua ya Usuluhishi na asilimia 78 kwenye hatua ya Uamuzi kwa migogoro na mashauri yote yaliyosajiliwa," alieleza Nungu.   

Naye, mjumbe kutoka Shirika la Kazi Duniani (ILO) aliye mwakilisha wa Mkurugenzi wa Shirika la Kazi Duniani hapa nchini, Maridadi Marwa amefafanua kuwa ILO wanaunga mkono utatuzi wa migogoro uishie kwenye hatua ya Usuluhishi, kwani utatuzi kwa kuwa njia hiyo humaliza mgogoro kabisa kwani pande mbili zenye tofauti hukubaliana tofauti na hatua ya uamuzi ambapo mmoja huambiwa kashindwa hivyo ni bora kujikita katika utatuzi wa usuluhishi.
              
Tume ya Usuluhishi na Uamuzi  ipo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, ambapo  Kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Tume hiyo kimefanyika kwa mujibu wa Agizo la Rais Na.1 la mwaka 1970. Baraza hilo   huiwezesha Tume kuboresha Huduma na masuala ya utatuzi Wa migogoro ya kikazi kwa njia ya Usuluhishi na Uamuzi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.