Habari za Punde

Vikundi Vya Vijana Wakabidhiwa Vifaa Kwa Mahitaji na Matarajio ya Vikundi Hivyo Kuongeza Kipato.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi pamoja na baadhi ya Viongozi wa Serikali wakiangalia vifaa viliomo ndani ya Programu ya Ajira kwa Vijana wakipata maelezo kutoka kwa Katibu Mkuu Wizara ya Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo Nd. Omar Hassan Omar {King}
Katibu Mkuu Wizara ya Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo Nd. Omar Hassan Omar akimuonyesha Balozi Seif baadhi ya Vifaa vitakavyotumiwa na Vijana katika Miradi ya Kilimo cha Umwagiliaji.
Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar.Mhe.Balozi Seif akiangalia bidhaa za Wajasiriamali Vijana kwenye Maonyesho yao kabla ya Kuzinduliwa kwa Programu ya Ajira kwa Vijana uje ya Ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdulwakil Kikwajuni.
Kikundi cha Sanaa na Utamaduni kikitoa burdani kwenye hafla ya uzinduzi wa Programu ya Ajira kwa Vijana iliyofanyika katika Ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdulwakil Kikwajuni.
Katibu Mkuu Wizara ya Vijana, Utamaduni,  sanaa na Michezo Nd. Omar Hassan Omar {King} akitoa Taarifa ya Kitaalamu juu ya hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa Programu ya Ajira kwa Vijana iliyozindauliwa rasmi.
Waziri wa Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo Balozi Ali Karume akitoa salamu za kumkaribisha Mgeni rasmi kuzindua rasmi  Programu ya Ajira kwa Vijana katika Ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdulwakil Kikwajuni.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizindua Programu ya Ajira kwa Vijana na ugawaji wa Vifaa kwa Vikundi vya Kiuchumi vya Vijana ngazi ya Wilaya hapo Ukumbi wa Sheikh Idissa Abdulwakil.
Baadhi ya Vijana watakaohusika na Programu ya Ajira kwa Vjana wakifuatilia kwa makini baadhi ya matukio ya uzinduzi wa Programu hiyo hapo Ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdulwakil Kikwajuni.
Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini “B” Nd. Rajab Ali Rajab Kulia akipokea baadhi ya vifaa vilivyomo ndani ya Programu ya Ajira kwa Vijana kwa ajili ya Vikundi vya Wilaya yake kutoka kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akimkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Kusini Nd. Idrissa Kitwana vifaa vilivyomo ndani ya Programu ya Ajira kwa Vijana kwa ajili ya Vikundi vya Wilaya yake.
                                                  Picha na – OMPR – ZNZ.
Na.Othman Khamis OMPR. 
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Wizara inayosimamia masuala ya Vijana  inapaswa kuratibu na kusimamia vyema masuala ya maendeleo yao ili kubaini vilivyo changamoto za upatikanaji wa Ajira unaozingatia zaidi ujuzi, vipaji pamoja na juhudi zao katika Taaluma.
Alisema jukumu la Wizara ya Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo ni kuhakikisha mahitaji na matarajio ya Vijana Kisekta yanajitosheleza katika Miongozo inayokwenda sambamba na Utekelezaji wa Agenda ya Maendeleo Endelevu ya Dunia kufikia Mwaka 2030.
Akizindua Programu ya Ajira kwa Vijana na ugawaji wa Vifaa kwa Vikundi vya Kiuchumi vya Vijana ngazi ya Wilaya hapo Ukumbi wa Sheikh Idissa Abdulwakil Kikwajuni Balozi Seif Ali Iddi alisema ili Kijana aweze kuuzika hana budi kujikita zaidi katika kutafuta Elimu na Ujuzi kulingana na soko la ajira liliyopo.
Balozi Seif alisema Serikali Kuu sasa iko katika hatua ya kuandaa Miongozo mipya ya Maendeleo ngazi ya Taifa ikiwemo Dira ya Mwaka 2025, Muelekeo wa Sera ya CCM kufikia Mwaka 2030 na Ilani ya Uchaguzi ya kufikia Mwaka 2025 lengo likiwa kuongeza Uchumi wa Taifa kupitia nguvu kazi ya Vijana.
Alisema utekelezaji wa Programu ya Ajira kwa Vijana ni miongoni mwa jitihada za Serikali kutimiza dhamira yake ya kukuza ujuzi kwa Vijana wanaokadiriwa kufikia asilimia 36.2% kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makaazi ya Mwaka 2012 ili kuchochea Maendeleo na ujenzi wa Uchumi wa Viwanda kufikia Uchumi wa Kati.
Balozi Seif alitanabahisha kwamba Serikali inaielewa vyema changamoto kubwa ya ufinyu wa ajira kwa Vijana kupitia hali halisi inayoonekana wazi mitaani pamoja na tafiti mbali mbali zilizofanywa na Wataalamu wa Takwimu Kitaifa na Kisekta ndani na nje ya Nchi.
Alifahamisha kwamba kwa mujibu wa Utafiti wa Nguvu Kazi wa Zanzibar wa Mwaka 2014 umeonyesha wazi kwamba kiwango cha ukosefu wa Ajira miongoni mwa Vijana wenye umri wa  Miaka 15 hadi 25 kilifikia asilimia 2.3% ya Vijana wote Nchini.
“ Kupitia Miongozo mbali mbali ya Kitaifa na Kisekta, Serikali imetoa maelekezo ya kulifanyia kazi suala hili kwa kutoa Matamko, Mikakati na maelekezo ya utekelezaji wa Programu mbali mbali ”. Alisisitiza Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwaomba Vijana kujenga matumaini makubwa  kutokana na kuanzishwa kwa Programu hiyo ya kudumu yenye kutafsirika kwa vitendo dhana ya Vijana kujiajiri kwa mustakabali wa Maendeleo ya Taifa.
Balozi Seif Ali Iddi alifahamisha kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inathamini  juhudi za Taasisi, Washirika mbali mbali wa ndani na nje ya Nchi ikiwemo Sekta Binafsi na Vijana wenyewe katika kulifanyia kazi suala la ukosefu wa ajira kwa Vijana.
“ Ni matumaini ya Serikali kuendelea kuunganisha nguvu za pamoja katika kulifikia suala la upatikanaji wa ajira kwa Vijana kwani waswahili walisema:- kinga na kinga moto ukawaka”. Alisema Balozi Seif.
Aliwahakikishia Washirikia hao wa Maendeleo na Taasisi Binafsi kwamba Serikali itaendelea kushirikiana nao katika kutatua changamoto za Vijana ili kufikia maendeleo ya Vijana na kuwa na nguvu kazi yenye tija Nchini sambamba na kumpa fursa Kijana wa Zanzibar kushiriki kikamilifu katika kuleta maendeleo.
Akigusia Makundi ya Vijana waliopatiwa zana, vitu na vifaa vitakavyokuwa chachu kwa Maendeleo yao Kiuchumi Balozi Seif aliwanasihi Vijana hao kuhakikisha kwamba wanaitumia fursa waliyopewa ya kukabidhiwa vifaa hivyo kwa lengo la kujikwamua na tatizo la ajira.
Akitoa Taarifa ya Kitaalamu juu ya hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa Programu ya Ajira kwa Vijana Katibu Mkuu Wizara ya Vijana, Utamaduni,  sanaa na Michezo Nd. Omar Hassan Omar {King} alisema Programu hiyo ni Mfumo wa jitihada za Serikali za kuwajengea uwezo wa kujitegemea Vijana Nchini.
Nd. Omar alisema jumla ya Vijana Elfu 3,051 katika Visiwa vya Unguja na Pemba watafaidika na Programu hiyo ya Ajira kwa Vijana katika Miradi ya Kilimo, Viwanda Vidogo vidogo pamoja na ujasiri Amali ambapo Serikali Kuu tayari imetenga jumla ya Shilingi Bilioni 12 zinazoratibiwa na Wizara ya Vijana.
Alisema kiwango hicho cha Fedha zilizotolewa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  kwa Awamu tofauti zinakwenda sambamba na zile Fedha  zilizoahidiwa na Mashirika na Taasisi za Kimatakifa zipatazo Shilingi Bilioni 46 katika kuunga mkono jitihada za Serikali za kuwajengea mazingira bora  ya Ajira Vijana.
Nd. Omar alifahamisha kwamba Wizara ya Vijana kwa kushirikiana na Taasisi mbali mbali Nchini tayari imeshajipanga sio tu kuwapatia vifaa Vijana hao bali itaandaa mafunzo, kuwapatia fursa za zitakazowezesha kupata soko kwa bidhaa watakazozalisha kwenye Miradi yao.
“ Programu hiyo haiko katika kuwapatia Vifaa tuu Vijana  bali pia itasaidia mafunzo, fursa za ajira sambamba na kuwatafutia soko la bidhaa watakazozalisha kwenye miradi yao”. Alisisitiza Nd. Omar Hassan Omar.
Katibu Mkuu  huyo wa Wizara ya Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo alifafanua wazi kwamba katika Programu hiyo Jumla ya Vijana 660 watajikita katika Miradi ya Ufundi, Vijana 400 kushiriki katika Sekta ya Kilimo na Vijana 150 katika Kazi za Sanaa zitazojumuisha Uchoraji, Muziki,Mapishi, Upambaji na Michezo.
Nd. Omar alisisitiza kwamba katika kuunga mkono Sekta ya Kilimo  ambao ndio inayotegemewa na kundi kubwa la Wananchi Mjini na Vijijini kupitia Programu hiyo Green House 19 zitajengwa na uchibwaji wa Visima 32 vya Maji  Unguja na Pemba lengo likiwa kuwanyooshea njia Vijana walioamua kujikita katika Sekta hiyo muhimu.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo alimshukuru na kumpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali  Mohamed Shein pamoja na wasaidizi wake kwa moyo anaoendelea kuchukuwa wa kujikubalisha kuwatumikia Wananchi wake Mijini na Vijijini Unguja na Pemba.
Mapema Waziri wa Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo Balozi Ali Karume aliwakumbusha Vijana kuzingatia na kuthamini fursa wanazopewa na Taifa na hata Taasisi za Kimataifa katika kujengewa mazingira bora ili waweze kujitegemea badala ya kusubiri Ajira zinazoendelea kuwa finyu katika maeneo tofauti ya Kazi.
Balozi Karume alisema Serikali kupitia Wizara anayoisimamia itaendelea kuwaunga mkono Vijana wote Visiwani Zanzibar na Tanzania kwa ujumla katika kuona changamoto zinazowakabili zinaondoka au kupunguwa kabisa ili wawe na utulivu wa kukabiliana na harakati zao za Kimaisha za kila siku.
Akitoa Shukrani kwa Niaba ya Vijana na Vikundi vya Vijana vya Ujasiri Amali Mwakilishi wa Vijana hao Nd. Hassan Said Hamad  kwa niaba yao ameishukuru na kuipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya Rais Dr. Ali Mohamed Shein kwa kuwajali Vijana ambao ndio nguvu kazi ya Taifa.
Nd. Said alisema Kundi laVijana kupitia Programu ya Ajira kwa Vijana tayari wameanza Mafunzo ya Miezi Sita chini ya Usimamizi wa Walimu kutoka Vyuo vya Amali na Chuo cha Ufundi cha Polisi na wanatarajia kumaliza Mafunzo yao Mwezi wa April  Mwka huu wa 2020 baada ya Mitihani yao wakiwa na furaha ya kuingia katika soko la Ajira kupitia Sekta za Ujasiri Amali.
Mapema Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alikagua Maonyesho ya Kazi na Bidhaa za Wajasiri Amali Vijana kutoka Chuo cha Mamlaka ya Mafunzo ya Amali Mkokotoni, Kituo cha Mafunzo ya Amali Mwanakwerekwe pamoja na Chuo cha Ushoni cha Polisi Ziwani.
Katika Maonyesho hayo Balozi Seif alifurahishwa na kuridhika na hatua ya Ubunifu iliyofanywa na Vijana hao ikionyesha mwanzo mzuri wa muelekeo wao wa kujikita katika firsa za Kujitegemea kiajira.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.