Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, Ametoa Msamaha Kwa Wanafunzi 19 wa Chuo Cha Mafunzo Zanzibar.



RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ametoa msamaha kwa wanafunzi kumi na tisa (19) ambao bado walikuwa wakiendelea kutumikia vyuo vya Mafunzo vya Unguja na Pemba ikiwa ni miongoni mwa shamra shamra za Sherehe za miaka 56 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee ilieleza kuwa kwa uwezo aliopewa chini ya kifungu cha 59 cha Katiba ya Zanzibar 1984, Rais Dk. Shein ameamuru kuwa kifungo kilichobaki cha wanafunzi walionufaika na msamaha huo, ambao bado wanaendelea kutumikia katika vyuo vya Mafunzo vya Unguja na Pemba kuwa kipindi hicho chote kinafutwa na kwamba wanafunzi hao waachiwe huru kuanzia leo tarehe 11 Januari 2020.

Taarifa hiyo, imeeleza kuwa, kwa kuwa Zanzibar itakuwa inasherehekea miaka 56 ya Mapinduzi ya Zanzibar hapo kesho tarehe 12 Januari 2020, na kwa kuwa Rais ameridhika kuwa kuna sababu za kutosha za kutumia uwezo wake huo katika sherehe hii, wanafunzi hao waachiwe huru.

Walionufaika na msamaha huo kwa Unguja ni Salum Kombo Juma, Rashid Abdalla Salum, Shaame Mussa Suleiman, Rajab Juma Suleiman, Mwinyi Abdalla Rajab, Faki Ramadhan Juma, Abdalla Said Khamis, Omar Khalfan Said, Abdulbaki Abdulaziz Muhammad, Mwinyi Maulid Haji, Said Ali Seif na Abdalla Ame Khamis.

Aidha, wengine walionufaika na msamaha huo kwa upande wa Pemba ni Fauzi Abdalla Said, Is-haka Saleh Ali, Hashim Moh’d Khamis, Ussi Juma Khamis, Juma Salum Moh’d, Moh’d Khamis Ali na Maulid Abdalla Seif.

Msamaha huo ambao hutolewa kila mwaka katika kipindi cha sherehe za Mapinduzi matukufu, huwahusisha wanafunzi ambao ni wazee sana, wenye maradhi sugu au wenye makosa madogo ambao wamebakisha muda mfupi wa kutumikia chuoni sambamba na  kuonesha nidhamu nzuri chuoni na kujutia makosa yao.

Wanafunzi wa Chuo cha Mafunzo, wenye makosa kama vile kuua kwa makusudi, wizi wa kutumia nguvu, wizi wa mali ya Umma, makosa ya kudhalilisha wanawake na watoto, makosa ya dawa za kulevya na wenye makosa mengi ya zamani kwa kawaida huwa hawapewi msamaha.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.