Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein akipokea Matembezi ya Maandamano na Maonesho ya Amsha Amsha ya Vikosi vya Ulinzi na Usalama vya SMT na SMZ , katika viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Zanzibar.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amesema jukumu la kudumisha amani na
usalama wa nchi ni la wananchi wote na sio la vyombo vya ulinzi na Usalama
pekee.
Dk. Shein amesema hayo viwanja vya Mnazimmoja mjini hapa,
baada ya kupokea matembezi ‘amsha amsha’, yaliyowashirikisha Makamanda na
wapiganaji wa vikosi vya Ulinzi na Usalama pamoja na Idara maalum za Serikali
ya Mapinduzi Zanzibar.
Amesema kila mwananchi ana jukumu la kudumisha amani iliopo
nchini pamoja na kulinda na kuyaenzi kikamilifu Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964.
Alisema hatua ya wakuu wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama ya kuanzisha
aina hiyo ya matembezi, inafaa
kupongezwa kwani inafanikisha dhamira ya kuwajengea ari wapinaji pamoja na kuwajengea
matumaini wananchi ya kuendelea kuiamini Serikali yao.
Alisema dhana ya kudumisha usalama wa nchi inatokana na Sera
ya chama cha Afro Shirazi Party (ASP) iliyowekwa baada ya Mapinduzi ya 1964, na
kusema dhana hiyo ni endelevu na haitokuwa na
mbadala.
Dk. Shein alisema baada ya Mapinduzi ya 1964, Zanzibar
ilianzisha Jeshi la Ukombozi (JLU) na baada ya Muungano wa Tanzania, Jeshi la
wananchi wa Tanzania liliundwa, lengo kuu likiwa ni kudumisha ulinzi na
usalama ndani na nje ya mipaka yake.
Alisema Wakoloni mbali na kutunza usalama katika kipindi cha
Utawala wao, uamuzi wao haukuwa wa kisera, wakati ambapo hivi sasa kila kikosi
kina sheria na kuongozwa kwa taratibu, hali inayovifanya vikosi hivyo kuwa na
nidhamu ya hali ya juu.
Alisema Serikali zote mbili za Jamuhuri ya Muungano wa
Tanzania (SMT) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) ziko salama, zikitoa
fursa kwa watu mbali mbali duniani kuja nchini na kufanya yale wanayoyapenda,
ikiwemo utalii, ‘honey moon’ na mapumziko.
Aidha, alisema utulivu na usalama wa kutosha uliopo hapa
nchini, imekuwa kivutio kikubwa cha kuvutia watalii kuja kwa wingi nchini, na
kusema kumekuwepo ongezeko la ujio wao kutoka 520,000 mwaka uliopita
(2017/2018) hadi kufikia 540,000 mwaka
huu.
Alieleza kuwa Utalii umekuwa na tija kubwa kwa maendeleo ya
kiuchumi pamoja na kuleta ustawi bora wa
wananchi wa Zanzibar.
Katika hatua nyengine, Rais Dk. Shein alikemea tabia ya baadhi
ya watu ya kujifanya wababe na kuidharau Serikali na kusema kila jambo lina mipaka yake,
akibainisha usawa uliopo kwa kila mwananchi mbele ya sheria.
Alisema Serikali zote mbili za SMT na SMZ zinaendeshwa kwa
misingi ya sheria, chini ya usimamizi wa vyombo vilivyowekwa ambavyo
hufanyakazi kwa misingi ya katiba na sheria.
Aliwataka wale wote waliojiandaa kufanya vituko kwa kisingizo
cha uchaguzi mkuu mwaka huu kuacha mara moja na kubainisha kuwa Zanzibar ni
nchi ya Mapinduzi iliopinduliwa ili wananchi waweze kuishi kwa amani na
usalama.
Alisema siasa isiwe sababu ya watu kufanya fujo na kusema
uchaguzi unaendeshwa kwa misingi ya sheria, akibainisha azma ya Serikali ya
kuwashughulikiya wale wote watakaojihusisha na uvunjifu wa amani.
Alieleza kuwa vyombo vya ulinzi viko makini na vinajuwa wajibu
wao na kufafanua kuwa hakutakuwepo na mtu atakaeonewa katika ushughulikiaji wa
jambo hilo.
Aidha, Dk. Shein aliwakumbusha wapiganaji hao kuwa suala la
ulinzi na kuitetea nchi halina mbadala, akiahidi Serikali zote mbili kuendelea
kubaki salama kwa vile zimejidhatiti kulinda mipaka yake ardhini na baharini.
Alieleza kuwa wapiganaji hao wana wajibu wa kulinda nchi na
kusema yeyote atakaekuja kwa dhamira ya kuchochea machafuko, taratibu za kisheria
zitachukuliwa.
Aliwataka wananchi wote kuishi na kuendelea kufanya shughuli
zao bila khofu, kwani vyombo vyao viko imara kuwalinda nyakati zote.
Nae, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa, Serikali
za mitaa na Idara maalum za SMZ, Haji Omar Kheir aliwashukuru makamanda na
wapiganaji wa Vikosi hivyo kwa kushiriki
vyema na kufanikisha matembezi hayo.
Aidha, alisema zoezi la namna hiyo ambalo pia limefanyika
kisiwani Pemba, litaendelea kufanyika mara kwa mara ili kuwaweka sawa wapiganaji .
Mapema, Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya
Halmashauri ya sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa, Brigedia Jenerali Fadhil Omar
Nondo, alisema lengo la ‘amsha amsha’ ni kujenga ari na uwezo miongoni mwa
vikosi hivyo pamoja na kuwajengea wananchi matumaini juu ya kuwepo kwa vikosi
vyao makini.
Alisema zoezi hilo lililoratibiwa na wakuu wa Vikosi vya
Ulinzi na Usalama hufanyika kila mwaka, ambapo katika miaka iliyopita
lilifanyika kwa mfumo wa ‘root march’ na kufanyiwa mabadiliko mwaka huu, na
kuwa katika mfumo wa ‘amsha amsha’.
Alisema zoezi hilo limewasharikisha wapiganaji kutoka JWTZ,
Polisi, Uhamiaji, KMKM, Mafunzo, JKU,KVZ na Zimamoto
linalenga kuyaenzi, kuyalinda na kuyatetea Mapinduzi ya 1964.
Aidha, alisema zoezi hilo lililoongozwa na kikundi cha JWTZ
chini ya Kamanda Kanali Said Khamis lilitokana na njia kuu tatu tofauti (roots)
zilizoanzia Mtoni na kuwakutanisha wapiganaji wote eneo la Ziwani, na kuendelea
na matembezi hayo hadi Uwanja wa Mnazi mmoja, yakifuatiwa na vyombo mbali mbali
vya usafiri pamoja na vifaa vinavyotumiwa na wapiganaji hao.
Abdi Shamna, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777476982. Fax: 024 2231822
E-mail:
abdya062@gmail.com
No comments:
Post a Comment