Habari za Punde

Ufunguzi wa Tamasha la Sita la Biashara katika Viwanja vya Maisara Wilaya ya Mjini Unguja

 Spika wa Baraza la Wawakilishi Zubeiri Ali Maulid akikata utepe kuashiria Ufunguzi wa Tamasha la Sita la Biashara katika Viwanja vya Maisara Wilaya ya Mjini Unguja.Ikiwa ni Shamra shamra za miaka 56 ya Mapinduzi ya Zanzibar.Kushoto ni Waziri wa Biashara na Viwanda Balozi Amina Salum Ali na Kulia Naibu Waziri wa Biashara na Viwanda Hassan Khamis Hafidh .

 Spika wa Baraza la Wawakilishi Zubeiri Ali Maulid akipata maelezo kutoka kwa Maafisa wa IkuluMwatima Rashid Issa na Juma Haji Juma wakati akitembelea Banda hilo katika Tamasha la sita la Biashara linalofanyika Maisara Wilaya ya Mjini Unguja .Ikiwa ni Shamra shamra za miaka 56 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Spika wa Baraza la Wawakilishi Zubeiri Ali Maulid akipata maelezo kutoka kwa Mjasiria mali Bi Atu wa kikundi cha Atu Product kutoka Dodoma wakati akitembelea Banda hilo katika Tamasha la sita la Biashara linalofanyika Maisara Wilaya ya Mjini Unguja .Ikiwa ni Shamra shamra za miaka 56 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

PICHA NA YUSSUF SIMAI/MAELEZO ZANZIBAR

Na Miza Kona /Suhaila Pongwa Maelezo Zanzibar   07/01/2020

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema itaendelea kuwaunganisha wafanyabiashara kupitia matamasha ya biashara ili kuweza kupata masoko ya kimataifa na kupelekea kukua kwa  kasi uchumi wa nchi

Akifungua Tamasha la Sita la Biashara Zanzibar Spika wa Baraza la Wakilishi Mhe. Zuberi Ali Maulid amesema ni vyema wafanya biashara kufanya biashara kiushindani  zenye kukidhi viwango ili kufikia uchumi wa kati na kuleta mafanikio zaidi.

Amesema  Serikali inaendelea na juhudi za kuimarisha viwanda vidogo vidogo ili kuweza kutasaidia kasi ya ukuaji wa uchumi na kupunguza tatizo la ajira nchini.

 Mhe. Spika amewataka wafanyabiashara pamoja na wajasiri amali kuitumia vyema fursa hiyo adhimu ya kutangaza na kuuza bidhaa  ili wakuze biashara zao kwa vile ni moja kati ya sekta muhimu ya kukuza uchumi na kutoa ajira kwa Taifa.

Aidha ameeleza kuwa changamoto kubwa inayowakabili wafanyabiashara ni ukosefu wa viwango katika bidhaa, urasimu na ukosefu wa leseni za biashara pamoja na uzalisha usokidhi viwango ambao huzorotesha maendeleo ya biashara.

 Akizungumza katika Tamasha hilo Waziri wa Biashara na Viwanda Balozi Amina Salum Ali amesema matamasha kama hayo husaidia kuzitangaza biashara zinazo zalishwa nchini kuweza kutambulika katika masoko ha kimataifa pamoja na kupata soko la uhakika .

Mhe. Amina amefahamisha kuwa Tamasha hilo kutakuwa na uzinduzi wa Klinik ya biashara ambayo itarahisisha upatikanaji wa huduma za biashara na kutatua changamoto zinazowakabili wafanyabiashara na kupata ushauri katika uendeshaji wa biashara  pamoja na kuonesha ubunufu wa vipaji katika bidhaa zao.

Balozi Amina ameeleza kuwa Tamasha la Biashara ni chachu ya ajira kwa vijana hivyo Wizara yake imejipanga kuboresha maonyesho ya biashara ili yawe endelevu na kuleta tija zaidi .

“Nawaomba wafanyabiashara pamoja na vijana kuitumia nafasi hii kwa umuhimu wa kipekee ili kuweza kuzitangaza bidhaa”, alieleza Waziri Amina.  


Tamasha hilo la sita linafanyika katika viwanja vya Maisara ambalo limehidhuriwa na wafanyabiashara zaidi ya 300 kutoka nchi mbali mbali ikiwemo Ruwanda, Burundi na Kenya ikiwa ni shamra shamra za kutimiza miaka 56 ya Mapinduzi Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.