Habari za Punde

Uzinduzi wa Boti Mpya ya Fast Ferries Kati ya Zanzibar na Dar es Salaam Inatarajiwa Kuaza Safari Yake ya Kwanza Kesho.Saa moja Asubuhi.

Na Kijakazi Abdalla  Maelezo Zanzibar. 17/01/2020
KAMPUNI ya Zanzibar Fast Ferries imezindua boti  mpya (Zanzibar 1) itayofanya kazi katika bandari ya Zanzibar na Dar-es-salam ambapo itaanza safari yake,siku ya jumamosi kutoka Zanzibar kwenda Dar-es-salam.
Akizungumza na Waandishi wa Habari katika Hoteli ya Golden Tulip Malindi Makamu Mwenyekiti wa Kampuni hiyo Salim Hassan Turkey amesema boti hiyo itapunguza tatizo la usafiri kwa abiria.
Amesema inapofika majira ya saa kumi na moja jioni kuna kuwa na tatizo la usafiri na baadhi ya Wafanyabiashara  wanakuwa hawajamaliza majukumu yao hivyo kuanza safari kwa boti hiyo kuwarahishia na kupata usafiri wa uhakika.
Aidha amesema boti hiyo ni ya kisasa na imezingatia mahitaji maalum ya abiria ikiwemo watu wenye ulemavu ili kuwaondoshea usumbufu waliokuwa wanaupata wakati wanaposafiri.
Hata hivyo amesema katika kuunga mkono juhudi za Serikali la kupunguza tatizo la usafiri hapa nchini kampuni hiyo inampango wa kuleta Boti nyengine mpya ,inayotarajiwa kuwasili mwezi wa tatu mwaka huu na kufanya safari kati ya visiwa vya Unguja na Pemba.
Mbali na hayo Turkey ameipongeza mikakati iliowekwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuweka Sheria madhubuti ya kusimamia usafiri wa Baharini jambo ambalo litapelekea kukuza uchumi wa nchi.
Boti ya Zanzibar one inayomilikiwa na kampuni ya Zanzibar Fast Ferries imegharimu sh. Bilioni 21 hadi kukamilika kwake,inatarajiwa kuchukuwa abiria 500 kwa wakati mmoja na itafanya safari kati ya Dar-es-salam na Zanzibar mara 4 kwa siku.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.