Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge Kazi, Vijana Ajira na Wenye Ulemavu,
Jenista Mhagama akiwa katika picha ya pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Selemani Jafo, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma,
Dkt. Binilith Mahenge (kulia) pamoja na Katibu Mtendaji wa Baraza la Biashara la
Taifa, Dkt. Godwill Wanga (kushoto) baada ya uzinduzi wa Muongozo wa
majadiliano kati ya sekta ya Umma na Binafsi katika ngazi ya Mikoa na Wilaya
uliofanyika leo jijini Dodoma.
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge Kazi, Vijana Ajira na Wenye Ulemavu,
Jenista Mhagama (kulia) akimkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt. Rehema
Nchimbi kitabu cha Muongozo wa Majadiliano kati ya sekta ya Umma na Binafsi
katika ngazi za Mikoa na Wilaya.Amepokea kitabu hicho kwa niaba ya Wakuu wa
Mikoa na Wilaya zote nchi nzima.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera,
Bunge Kazi, Vijana Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama (kulia) akikabidhiwa
kitabu cha Muongozo wa Majadiliano kati ya sekta ya Umma na Binafsi katika
ngazi za Mikoa na Wilaya na Katibu Mtendaji wa Baraza la Biashara la Taifa, Dkt.
Godwill Wanga (kushoto). Makabidhiano hayo yamefanyika leo jijini Dodoma wakati
wa uzinduzi wa muongozo huo.
Waziri wa Nchi, Ofisi
ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge Kazi, Vijana Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista
Mhagama amesema kuwa majadiliano ya mabaraza ya biashara yanayofanyika katika
ngazi ya Taifa, Mikoa na Wilaya yameendelea kusaidia uchumi wa nchi kuimarika.
Waziri Mhagama ameyazungumza
hayo leo Jijini Dodoma wakati akizindua Muongozo wa majadiliano kati ya sekta
ya Umma na Binafsi katika ngazi ya Mikoa na Wilaya uliofanyika jijini humo
ambapo amesema kuwa inawezekana mabaraza ya biashara yalikuwa hayafanyiki vizuri kwa sababu watu
walikuwa wanashindwa kutumia mazingira waliyonayo kujipanga kuendesha mabaraza
haya lakini, muongozo huo utasaidia watu kukutana kwa ajili ya majadiliano
yenye tija.
“Ili kuwa na utendaji
unaotukuka lazima tuwe na muongozo wa nini kifanyike, wakati gani, kwa
utaratibu upi na kwa rasilimali zipi, hatuwezi kuzungumza uchumi wa viwanda
wala utekelezaji wa Dira ya Maendeleo bila sekta binafsi hivyo kuna kila haja
ya kutengeneza mazingira wezeshi yatakayoifanya sekta ya umma isaidiane na
ishirikiane kwa karibu na sekta binafsi ili yaliyopangwa yaweze kutekelezwa”,
alisema Waziri Mhagama.
Waziri Mhagama
amesisitiza wahusika kutoa mrejesho wa majadiliano ya mabaraza ya biashara
katika ngazi za mikoa na wilaya kwani kama yatafanyika maamuzi na kujiwekea
malengo ambayo hayatekelezeki hakutakuwa na maana ya vikao hivyo.
Kwa upande wake
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Selemani
Jafo amesema kuwa muongozo huo ni kitendea kazi katika ngazi zetu za mikoa na
wilaya kitakachowezesha uendeshaji wa mabaraza haya ambayo kwa kiasi kikubwa
yataleta tija.
“Takwimu zinaonesha
kuwa kati ya Mikoa 26 ni mikoa 16 pekee ambayo ilifanya mabaraza hayo, sasa
muongozo umeshatolewa hivyo miongoni mwa taarifa za wakuu wa Mikoa zinazoletwa
TAMISEMI lazima taarifa ya Uendeshaji wa Mabaraza ya Biashara katika mikoa yenu iwepo”, alisema Waziri
Jafo.
Vile vile, Katibu
Mtendaji wa Baraza la Biashara la Taifa, Dkt. Godwill Wanga amesema Serikali
imeendelea kuboresha mazingira ya biashara kupitia majadiliano kati ya sekta
hizo mbili ambapo inasimamia kwa karibu majadiliano hayo kama njia muafaka ya
kufikia maridhiano yatakayoboresha uchumi na maendeleo endelevu ya nchi.
“TNBC tunatoa wito
kwa wadau wote kutumia majadiliano haya kuainisha matatizo ya miradi ya pamoja
kati ya sekta hizi mbili inayolenga kuimarisha mazingira ya biashara na
uwekezaji nchini”, alisema Dkt. Wanga.
Akiishkuru Serikali
ya Awamu ya Tano, Muwakilishi wa Mkurugenzi wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPFS),
Rehema Mbogi amesema kuwa Serikali imeonesha umakini katika masuala yanayohusu
majadiliano kati ya Sekta Binafsi na Umma katika ngazi zote kwani sekta binafsi
imekua ikishirikishwa katika mabaraza ya biashara pamoja na kupata nafasi za
kujadiliana masuala mbalimbali viongozi wa Serikali.
“Mnamo mwaka juzi
nilishiriki katika mkutano nchini Afrika Kusini uliohusu mfumo wa majadiliano
katika nchi za Kusini mwa Afrika nilifurahishwa kuona kwamba nimesimamishwa
kuelezwa kwamba nchi yetu Tanzania ina mfumo bora wa majadiliano unaoeleweka
kuanzia ngazi ya Taifa hivyo hii ni fursa nzuri ambayo tukiitumia vizuri
tunaweza kufika mbali katika nchi”, alisema Bi.Rehema.
No comments:
Post a Comment