Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein Akishiriki Katika Maziko ya Jaji wa Mahkama Kuu Zanzibar Marehemu Mkusa Sepetu Yaliofanyika Kijiji Kwao Mbuzini Wilaya ya Magharibi "A" Unguja leo.Kil

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Ali Mohamed Shein na (kulia kwa Rais ) Rais Mstaaf wa Zanzibar Mhe. Dkt. Amani Karume na (kushoto kwa Rais) Jaji Mkuu wa Zanzibar Mhe. Omar Othman Makungu na Viongozi wengi na Wananchi wakiitikia dua ya kuuombea mwili wa Marehemu Jaji wa Mahkama Kuu Zanzibar Jiji Mkusa Sepetu baada ya kumaliza Sala ya Maiti iliofanyika katika Msikiti wa Ijumaa Mbuzini Wilaya ya Maghareibi"A" Unguja yaliofanyika leo 16-2-2020 katika makaburi ya Kijiji chao Mbuzini Unguja.


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein  leo ameongoza mazishi ya marehemu Jaji Mkusa Isaac Sepetu yaliyofanyika kijijini kwao Mbuzini, Wilaya ya Magharibi ‘A’, Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Viongozi mbali mbali wa vyama vya siasa na serikali, sekta binafsi pamoja na wananchi, ndugu na jamaa walihudhuria  katika mazishi hayo akiwemo Rais Mstaafu wa Zanzibar wa Awamu ya Sita Dk. Amani Abeid Karume, Spika wa Baraza la Wawakilishi Zubeir Ali Maulid, Jaji Mkuu wa Zanzibar Omar Othman Makungu, Jaji wa Mahakama ya Rufaa Tanzania Mbarouk Salim Mbarouk.

Wengine ni Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee,  Mwanasgeria Mkuu wa Zanzibar Said Hassan Said, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Abdalla Juma Mabodi, Mawaziri na viongozi wengine wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mapema Alhaj Dk. Shein aliungana na viongozi, ndugu, jamaa, marafiki na wananchi mbali mbali katika dua ya Hitma pamoja na sala ya kumsalia Marehemu Jaji Mkusa Isaac Sepetu katika Msikiti wa Ijumaa Mbuzini, Wilaya ya Magharibi A, Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Akisoma Wasfu wa Marehemu Jaji Mkusa Isaac Sepetu, Mrajis wa Mahkama Kuu Zanzibar Mohamed Ali Mohamed alieleza kuwa Marehemu  Jaji Mkusa Isaac Sepetu alizaliwa tarehe 12 Machi, 1974 Zanzibar.

Alisema kuwa Marehemu alipata elimu ya Msingi na Sekondari huko Urusi mnamo mwaka 1982 hadi mwaka 1992.

Kwa upande wa elimu ya Juu alieleza kuwa Marehemu amesoma Shahada ya Kwanza ya Sheria (LLB) mwaka 1993 hadi mwaka 1997 huko Urusi.

Maisha yake katika Utumishi wa Umma yalianza mwaka 2001 hadi mwaka 2002 alipoajiriwa kuwa Afisa Sheria wa Wizara ya Fedha na Uchumi Zanzibar.

Mwaka 2002 hadi 2004 aliteuliwa kuwa Hakimu wa Mkoa katika Mahkama ya Vuga na mwaka na mwaka 2004 hadi 2006 aliteuliwa kuwa Hakimu wa Mkoa Dhamana katika Mahkama ya Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Aidha, wasfu huo ulieleza kuwa mnamo mwaka 2006 hadi 2009 aliendelea kuwa Hakimu wa Mkoa Dhamana wa Mahkama ya Mkoa wa Kusini Unguja iliyopo  Mwera na mnamo mwaka 2009 hadi mwaka 2010 aliendelea kuwa Hakimu Dhamana Mahkama ya Mkoa Vuga.

Mwaka 2010 hadi 2020 aliteuliwa kuwa Jaji wa Mahkama Kuu Zanzibar.

Katika nyadhifa nyengine za Uteuzi Marehemu Jaji Mkusa mnamo mwaka 2014 hadi 2020 aliteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi ya Mahkama Zanzibar na tarehe 10 Disemba 2014 hadi 20 Januari 2015 aliteuliwa kuwa Kaimu Jaji Mkuu wa Zanzibar

Pia, mnamo tarehe 12, Disemba 2016 hadi Januari 16 mwaka 2017 aliteuliwa kuwa Kaimu Jaji Mkuu wa Zanzibar ambapo pia,  mnamo Disemba 8, 2017 hadi Januari 17 mwaka 2018 aliteuliwa kuwa Kaimu Jaji Mkuu wa Zanzibar.

Akiendelea kusoma wasfu huo Mrajis wa Mahkama Kuu Zanzibar Mohamed Ali Mohamed aliongeza kuwa mnamo Machi 22, mwaka 2019 Marehemu Jaji Mkusa aliteuliwa  kuwa Mjumbe wa Kamati ya Uongozi ya Mahkama na mnamo Disemba 12 mwaka 2019 hadi Januari 20 mwaka 2020 aliteuliwa tena kuwa Kaimu Jaji Mkuu wa Zanzibar.

Marehemu Jaji Mkusa Isaac Sepetu ameacha Wajane wawili na watoto watatu Mwenyezi Mungu amlaze mahala pema Peponi. Amin.

Wakati huo huo mara baada ya mazishi, Alhaj Dk. Shein alifika nyumbani kwa familia ya marehemu Jaji Mkusa hapo hapo Mbuzini na kuipa pole familia na wafiwa wote na kumuomba Mwenyezi Mungu awape subira katika kipindi hiki kigumu cha msiba.

Rajab Mkasaba, Ikulu
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.