Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, akizungumza na Uongozi wa Wizara ya Kazi Uwezeshaji Wazee Wanawake na Watoto Zanzibar, wakati wa kuwasilisha Taarifa ya Utekelezaji Mpango Kazi kwa mwezi wa Julai hadi Disemba 2019 / 2020, uliofanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, amesema kuwa kuwepo kwa
mazingira ya muhali katika jamii kumeweza kuchangia kwa kiasi kikubwa
kudhorotesha mienendo ya kesi za udhalilishaji wa wanawake na watoto.
Hayo aliyasema leo, Ikulu Jijini Zanzibar alipokutana
na uongozi wa Wizara ya Kazi, Uwezeshaji, Wanawake na Watoto wakati ilipowasilisha
taarifa ya utekelezaji wa Mpango Kazi kwa
kipindi cha Julai hadi Disemba katika mwaka wa fedha 2019/2020.
Rais Dk. Shein alieleza haja ya kuachana na muhali
katika kuzitafutia ufumbuzi kesi za udhalilishaji wa wanawake na watoto na
kusisitiza umuhimu wa kusimamia sheria na kutaka sheria kuchukua mkondo wake
ili kuondoa malakamiko katika jamii.
Alieleza kuwa juhudi za makusudi zimechukuliwa na
Serikali ikiwa ni pamoja na kuunda Kamati Maalum ya kupambana na vitendo vya
ushalilishaji wa wanawake na watoto hivyo kuna kila sababu ya kuchukuliwa hatua
za kisheria kwa wanaofanya vitendo vya udhalilishaji huo.
Rais Dk. Shein alisisitiza haja ya kuendelezwa
mikakati iliyowekwa na Serikali kupitia Wizara hiyo ili kuhakikisha yale yote
yaliopangwa yanafanyiwa kazi na hatimae kupata matokeo yaliyokusudiwa.
Alifahamisha kuwa kuna kila sababu ya kupambana na
vitendo vya udhalilishaji wa wanawake na watoto kwa kufuata sheria zilizowekwa
na kuitaka Wizara hiyo isichoke na isivunjike moyo katika kukabiliana na
vitendo hivyo kwani ni miongoni mwa kazi iliyokabidhiwa kusimamia hayo.
Alisema kuwa mambo hayo yanahitaji nguvu za pamoja
kwani hayo ni mapambano makubwa yanayofanywa na watu ambao wamekosa haya
kutokana na kufanya vitendo hivyo vya kinyama.
Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein aliitaka Wizara
hiyo kufanya kazi kwa pamoja, kuendelea kushirikiana, kuongeza uzalendo kwenye
kazi zao pamoja na kuwa waadilifu, waaminifu na watiifu sambamba na kuwa
wabunifu katika kazi.
Aidha, Rais Dk. Shein alieleza umuhimu wa kuundwa
kwa Sheria ya Wazee ambayo Serikali imeamua kuiunda kwa makusudi ambapo mbali
ya mambo mengine pia, Sheria ndani yake yamo masuala ya Pencheni ya Jamii
yatakuwemo hatua ambayo itaondosha wasi wasi mkubwa wa wazee juu ya kuendelea
kwa Pencheni yao hiyo.
Nae Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Idd
aliipongeza Wizara hiyo na kueleza haja ya kutafutwa njia za kuondosha
udhalilishaji huku akipongeza hatua zinazochukuliwa na Wizara hiyo katika
kufuatilia mikopo wanayoitoa kwa wananchi.
Nae Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee aliipongeza kazi nzuri ya utayarishaji na uwasilishaji
iliyofanywa na Wizara hiyo na kuutaka uongozi wa Wizara hiyo kuendelea
kushirikiana.
Mapema Waziri wa Kazi, Uwezeshaji Wazee, Wanawake
na Watoto Maudline Cyrus Castico akisoma utangulizi wa taarifa hiyo kwa niaba
ya Wizara anayoiongoza ilimpongeza Rais Dk. Shein kwa kutekeleza vyema Ilani ya
Uchaguzi ya CCM.
Aidha, Waziri Castico alieleza kuwa Dira ya Wizara hiyo ni kuwa na jamii ya
Wazanzibari yenye ajira za staha, ubunifu na uwezo wa kukabiliana na umasikini,
inayotoa haki na fursa sawa kwa watu wa makundi yote.
Waziri Castico alileza kuwa Dira hiyo inatekelezwa kwa kuimarisha upatikanaji wa
kazi na ajira zenye staha, kukuza usawa wa kijinsia na kuwawezesha
wanawake, vijana, wazee na watoto kwa
kusimamia utekelezaji wa sheria na kanuni za kazi.
Aliongeza kuwa Wizara hiyo imeanzishwa kwa lengo
la kusimamia utekelezaji wa sheria na miongozo ya kazi, kuratibu upatikanaji wa
ajira za staha hasa kwa vijana, kuimarisha program za kuwawezesha wananchi
kiuchumi na kuimarisha haki, ustawi na maendeleo ya wanawake, watoto, wazee na
wanaoishi katika mazingira magumu.
Aidha, Waziri huyo alieleza majukumu yaliyotekelezwa
na Wizara yake kwa kipindi cha miezi sita ikiwa ni pamoja na kuunga umeme wa
jua katika nyumba 150 katika kijiji cha Makoongwe Pemba na Mbuyu Tende Unguja
kupitia mradi wa “Barefoot Zanzibar”
Pia, kwa maelezo ya Waziri Castico Wizara imeweza
kutunisha Mfuko wa Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi kwa ongezeko la TZS Milioni 161 ambapo ni sawa na asilimia 230 ya
lengo walilojipangia kwa miaezi 6.
Nao viongozi wa Wizara hiyo walieleza mafanikio
yaliopatikana katika Wizara hiyo na kueleza mikakati yao waliyoiweka katika
kuhakikisha wanafikia malengo ya kuwatumikia wazee, wanawake pamoja na watoto huku wakisisitiza
kuimarisha mashirikiano waliyonayo.
Aidha, walipongeza utaratibu wa mikutano hiyo
ambayo walisema imeweza kusaidia utendaji wa kazi zao na kutumia fursa hiyo
kumpongeza Rais Dk. Shein kwa jinsi anavyowaongoza.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment