Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (kulia) akizungumza na Uongozi wa Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora katika kikao cha utekelezaji wa Mpango kazi kwa kipindi cha Julai-Disemba 2019 katika ukumbi wa Ikulu Mjini Zanzibar,(kushoto) Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Nd,Yakout Hassan Yakout.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali
Mohamed Shein amesema viongozi wote wa
Serikali wana wajibu wa kusajili taarifa za mali na madeni kwa uwazi, ikiwa ni
hatua muhimu katika kukamilisha dhana ya utawala bora.
Dk. Shein amesema hayo Ikulu jijini Zanzibar, wakati akipokea
taarifa ya utekelezaji wa mpango kazi kwa Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na
Utawala Bora kwa kipindi cha kuanzia Julai hadi Disemba 2019/2020.
Alisema ni wajibu wa viongozi wote nchini kubainisha kwa
usahihi na kwa uwazi mali na madeni waliyonayo, na kueleza kuwa hakuna sababu
ya viongozi kuficha mali zao.
Alipongeza uongozi wa
Tume ya Maadili na Viongozi wa umma kwa kutambua dhima kubwa
iliyokabidhiwa na Taifa pamoja na kutekeleza vyema majukumu yao, ambayo yanawahusisha
viongozi wote wa umma.
Aidha, aliipongeza Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa
kufanya kazi zake kuambatana na misingi ya haki na demokrasia na kutoa fursa ya
kujieleza kwa viongozi wanaotuhumiwa.
Alisema ana matumaini makubwa
ofisi hiyo itaweza kupata mafanikio makubwa katika siku za usoni
kutokana na kasi kubwa ya utendaji kazi inayochukuliwa na watendaji wake.
Katika hatua nyengine,
Dk. Shein aliutaka uongozi wa
Chuo cha Utawala wa Umma (IPA) kuendelea kutekeleza malengo ya utoaji wa
mafunzo kwa watumishi wa umma na wananchi mbali mbali ili kuwajengea uwezo, sambamba
na kuliwezesha Taifa kuwa na wigo mpana
wa wataalamu.
Alipongeza juhudi zinazofanywa na uongozi wa chuo hicho katika utoaji wa taaluma kupitia viwango
tofauti vya elimu.
Nae, Katibu Mkuu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu
Kiongozi, Dk. Abdulhamid Yahya Mzee aliipongeza Uongozi wa Ofisi ya Rais,
Utumishi wa Umma na Utawala bora kwa juhudi kubwa wanazoendelea kuchukuwa katika
kusimamia na kupanga vyema maslahi na stahiki mbali mbali za watumishi wa umma,
hatua iliyowezesha kuleta utulivu mkubwa kwao.
Alishauri Ofisi hiyo kuharakisha utoaji wa matokeo kwa
wananchi na wanavyuo wanaofanya usaili wa nafasi mabali mbali za kazi, akibainisha
kuwepo kwa utaratibu unaochukuwa muda mrefu hivi sasa hadi kukamilisha mchakati wa ajira kwa watumishi
wapya.
Alisema baadhi ya nyakati hali hiyo imekuwa ikiipotezea
Serikali watumishi wenye sifa na viwango bora vya elimu baada ya wananchi hao kuchukuliwa
na taasisi nyengine binafsi au kujiunga na taasisi zilizoko Tanzania Bara kutokana na ucheleweshaji huo.
Aidha, Dk. Abdulhamid aliushauri uongozi wa Ofisi hiyo
kuzingatia kwa kina changamoto ya kuwepo
kwa makundi ya watumishi kutoka baadhi ay Idara/taasisi za Serikali wanaokwenda
mafunzoni na baadae kubadili kada, jambo alilosema limekuwa likiziathiri idara/taasisi wanazotoka.
Mapema, kwa niaba akiwasilisha taarifa ya utekelezaji ya
Mpango kazi ya Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala bora kwa kipindi cha
Julai hadi Disemba, 2019/2020, Waziri Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi, Issa Haji Ussi ‘Gavu’ alisema Wizara hiyo imepata mafanikio makubwa
katika utekelezaji wa mpango huo kupitia programu mbali mbali.
Alisema mafanikio hayo yamefikiwa kutokana na upatikanaji wa fedha
wa shilingi 6,587,048,945/ ikiwa sawa ni asilimia 93 ya fedha zilizokadiriwa
kutumika katika kipindi hicho.
Alisema miongoni mwa mafanikio hayo ni pamoja na kuandaa
miongozo ya usimamizi wa TEHAMA katika taasisi ya udhibiti wa viwango na kutoa
ushauri wa kitaalamu katika aunzishaji wa mfumo wa Elektronik katika shughuli za
uendeshaji na utoaji wa mizigo bandarini.
Alisema Wizara ilifanya mapitio ya sheria ya Utumishi wa umma
ya mwaka 2011 na kuandaa mapendekezo ya marekebisho ya sheria hiyo pamoja na
kanuni zake.
Aidha, alisema ilifanikiwa kuingiza taarifa za awali za
viongozi katika mfumo wa kielektronik wa kusajili taarifa za mali na madeni ya
viongozi.
Sambamba na hayo Waziri Gavu
alisema Wizara hiyo ilitowa elimu ya uelewa kwa maafisa utumishi na
mamlaka, mashirika na taasisi zinazojitegemea kuhusu muongozo wa fomu ya
upimaji utendaji kazi pamoja na fomu ya upandishwa vyeo kwa watumishi wa umma.
Vile vile, alisema Wizara ilifanikiwa kukamilisha ripoti ya
hali ya rushwa na uhujumu uchumi ya mwaka 2019.
Alieleza kuwa katika kipindi hicho Wizara ilikusanya jumla ya
shilingi 53,363,982/ kutokana na ada ya ukaguzi wa Hesabu za mashirika na
taasisi mbali mbali, ikiwa sawa na asilimia 59 ya makadirio.
Aidha, Mwenyekiti wa Tume ya Maadili ya Viongozi wa umma Asaa
Ahmad Rashid alisema kumekuwepo uwasilishaji mzuri wa taarifa za mali na madeni
ya viongozi wa umma na kubainisha kuwa hadi Disemba, 2019 jumla ya viongozi
2,300 walikuwa wamewasilisha taarifa zao katika Ofisi hiyo.
Hata hivyo, alisema kuna baadhi ya viongozi huchelewa
kuwasilisha taarifa zao kwa wakati, sambamba na viongozi wengi hususan wale
ambao hawako katika ngazi za uteuzi, ikiwemo wahasibu na wakaguzi wa ndani ambao hushindwa kabisa kuwasilisha taarifa zao.
Abdi Shamna, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777476982. Fax: 024 2231822
E-mail:
abdya062@gmail.com
No comments:
Post a Comment