Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh. Saleh Omar Kabi akisoma Dua Maalum ya kumuombea Rais wa Kwanza wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Marehemu Mzee Abeid Amani Karume, ilifanyika katika viwanja vya kaburi la marehemu Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui Jijini Zanzibar.
RAIS wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein leo amejumuika na viongozi wa Serikali pamoja na viongozi wa madhehebu
mbali mbali ya Dini katika dua ya kumbukumbu ya muasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar,
marehemu mzee Abeid Amani Karume.
Hafla hiyo ilifanyika kwenye Kaburi la
kiongozi huyo liliopo Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui, ambapo viongozi wa madhehebu
mbali mbali ya dini walipata fursa ya kumuombea dua marehemu.
Akifungua dua ya kiislamu, Mufti wa
Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kaabi alimtakia malazi mema kiongozi huyo na kusema
wakati wa uhai wake akiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi, Marehemu alizingatia umuhimu wa kuweka hali sawa za wananchi wake
pamoja na kuhakikisha wanaishi katika makaazi bora.
Alimuomba Mwenyezi Mungu kuinusuru
Zanzibar na dunia kwa ujumla ili kuondokana na maradhi ya Corona yaliosambaa
Ulimwenguni.
Nae, Kiongozi wa Kanisa la Anglicana
Zanzibar, Askofu Michael Henry Hafidh alimtakia msamaha, rehema na amani
kiongozi huyo katika malazi yake, sambamba na kumuomba Mwenyezi Mungu
kubainisha njia ya kuondokana na ugonjwa wa Corona ulioikumba Dunia.
Aidha, Kiongozi wa jamii ya Kihindu
Yoges Pirocit alitumia fursa hiyo kumuombea dua na kumtakia rehma kiongozi
huyo.
Dua ya kumbukumbu ya Marehemu Abeid
Amani Karume, ambayo kwa kawaida hufanyika kila kifikapo April 7 ya kila mwaka,
ilihudhuriwa na viongozi mbali mbali wa Serikali, akiwemo Waziri Mkuu wa
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Majaliwa Kassimu Majaliwa, Viongozi
wakuu wa Kitaifa wastaafu akiwemo Dk. Amani Abeid Karume pamoja na baadhi ya
Mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Wengine waliohudhuria dua hiyo ni
Kiongozi wa Mabalozi wadogo waliopo Zanzibar George Augostino, Mwakilishi wa
Familia ya Marehemu Balozi Ali Karume, Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu
Mkuu Kiongozi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee, Jaji Mkuu wa Zanzibar Omar Othman
Makungu na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Abdalla Juma Sadalla ‘Mabodi’.
Aidha, wengine ni pamoja na Kamanda Brigedia JWTZ Zanzibar Fadhil
Omar Nondo, Kamishna wa Polisi Zanzibar Mohamed Hassan, Mwenyekiti Idara Maalum
SMZ, Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Hassan Khatibu pamoja na Wawakilishi wa
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pamoja na Viongozi mbali mbali wa
vyombo vya Ulinzi na Usalama vya SMZ na SMT.
Dua ya kumbukumbu ya Marehemu mzee
Abeid Amani Karume mwaka huu imehusisha washiriki wachache, ikiwa tofauti na
ilivyozoeleka ambapo wananchi na waumini
walipata fursa ya kushiriki na kusoma khitma, hatua hii ikiwa ni juhudi za
kukabiliana na maambukizo ya virusi ya Corona vinavyoendelea kusambaa duniani
kote.
Abdi Shamna,
Ikulu Zanzibar
Postal
Address: 2422 Tel.:0777476982. Fax: 024 2231822
E-mail: abdya062@gmail.com
No comments:
Post a Comment