Habari za Punde

Tume ya Utangazaji Zanzibar yawaonya wanaotoa taarifa potofu mitandaoniKatibu Mtendaji Tume ya Utangazaji Zanzibar Omar Said akitoa taarifa ya kukemea matumizi mabaya ya  mitandao ya kijamii kusambaza taarifa potofu za ugonjwa wa Corona na kuwatia taharuki wananchi huko katika Ukumbi wa Wizara Habari,Utalii na Mambo ya Kale Kikwajuni .Mjini Zanzibar.

PICHA NA KHADIJA KHAMIS IDARA YA HABARI MAELEZO ZANZIBAR  
Na Issa Mzee                   Maelezo               

Tume ya Utangazaji Zanzibar imetoa onyo kwa watumiaji wa mitanado ya kijamii ambao wanajihusisha na utoaji wa taarifa potofu za ugonjwa wa corona na kuwatia taharuki wananchi.
Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari Katibu Mtendaji  Tume ya Utangazaji Zanzibar Omar Said Amer  alisema wapo baadhi ya watu ambao wanajihusisha na utoaji na usambazaji wa taarifa kwa njia aya mtandao ambazo hazina ukweli wowote.
 Amesema  wapo baadhi ya watu ambao pia wanatumia fursa  kwa kuwazushia  viongozi wa Serikali akiwemo Waziri wa Habari Utalii na Mambo ya kale,jambo ambalo si kweli na ni kinyume na utaratibu.
Aidha alitoa mfano wa muendelezo wa matukio hayo kufuatia kijana mmoja aliyejirekodi mtandaoni ya kuwa ameambukizwa ugonjwa wa corona ilihali kijana huyo hakuwa na ugonjwa huo jambo lililozua taharuki miongoni mwa wanajamii waliokaribu nae.
“Tume ya utanagazaji ipo karibu na watumiaji wa mitandao ya kijamii,ieleweke wazi kuwa kanuni na sheria za Utangazaji zipo palepale,Tume ya Utangazaji inasisitiza kwamba ipo macho na inafuatilia kwa karibu matukio hayo” alisema Katibu
Amesema  Tume ya Utanagazaji Zanzibar kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi na Mamlaka ya Mawasiliano(TCRA) wameweza kuwakamata wahusika waliosambaza taarifa za uongo kupitia mitandaoni.
Alisema kuwa tume ya Utangazaji inatoa onyo kali kwa wenye tabia na desturi za kutangaza habari za uzushi na zisizofanyiwa utafiti wa kitaalamu,kinyume na hapo Tume ya Utangazaji haitasita kuchukua hatua za kisheria.
Pia Katibu huyo amesema onyo hilo pia linaelekezwa kwa wale wote wanaopokea taarifa na kuamua kusambaza kwa njia ya ujumbe wa simu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.