Habari za Punde

Vipindi vya masomo kuanzishwa wanafunzi kujifunza wakiwa majumbani


WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, imejipanga kuanzisha vipindi vya masomo kwa Wanafunzi wa Skuli za Serikali na Binafsi ili kuwasaidia Wanafunzi hao kujifunza wakiwa nyumbani katika kipindi hiki Dunia ikiwa katika janga la virusi vya Korona.

Vipindi hivyo vinatarajiwa kurushwa wiki ijayo katika vyombo mbalimbali vya habari vya Serikali, Binafsi,Redio jamii na Mitandao ya kijamii ambayo imesajiliwa na Wizara na Tume ya Utangazaji ili kuhakikisha Wanafunzi hawasahau masomo yao.

Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Mhe Simai Mohammed Said, ameyasema hayo wakati akizindua mkakati wa Elimu kwa Wamiliki wa Vyombo vya Habari, huko katika Kituo cha habari katika Elimu Kwarara ‘Education Media Center’.

Amesema tayari zaidi ya vipindi 20 vimeshaandaliwa kwa Wananfunzi wa Msingi, zaidi ya vipindi 88 kwa Wanafunzi wa Maandalizi na zaidi ya vipindi 88 kwa Wanafunzi wa Kidato cha kwanza hadi kidato cha nne.

Mhe Simai, amesema vipindi hivyo vitakuwa na muamko mbukwa kwa watoto wa kuweza kuvutiwa na kuacha kutumia mifumo ya kielimu iliyozoeleka ambao utawawezesha Wanafunzi kujifunza hata wakati yatakapomalizika maradhi hayo.

Hata hivyo, amesema vipindi hivyo kwa kiasi kikubwa vitawasaidia Wanafunzi hasa wa Maandalizi na Msingi kutosahau masomo baada ya kutumia muda mwingi kwa ajili ya kucheza.

Amefahamisha kuwa, vyombo vya habari vina nafasi kubwa ya kuunganisha nguvu zao katika kuwasaidia watoto kupata Elimu katika kipindi hiki ambapo kila nchi zimefunga Skuli na Vyuo vikuu ikiwemo Zanzibar kutokana na kuounguza kuenea kwa maambukizi ya maradhi ya Korona.

Hivyo, ameitaka Tume ya Utangazaji kuhakikisha wanalisimamia suala hilo ili kuona kila chombo kinarusha vipindi hivyo kwa maslahi ya watoto ambao ndio Taifa la kesho.

“Lengo letu ni kuona tunafanya vipindi ambavyo vitasaidia kufikisha malengo ya watoto wetu katika kipindi hiki kigumu cha Taifa letu tukiwa na mapambano ya ugonjwa huu,” amesisitiza Mhe Simai.

Pia amewaomba Wazazi kufuatilia ratiba ya vipindi hivyo kupitia vyombo vya habari na kuwahamasisha watoto waotilia juyafuatilia masomo hayo ili lengo lililokusudiwa liweze kufikiwa kwa haraka na kuleta mafanikio.

Sambamba na hayo, amewasisitiza wazazi na walezi kudhibiti watoto wao kuranda randa mitaani ili kuzuia maambukizi ya virusi hivyo ambayo hivi sasa kwa Tanzania yamefikia katika maambukizi ya wenyewe kwa wenyewe.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Utawala na Uendeshaji wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, mw Abdullah Mzee Abdullah, amesema ni vyema Vyombo vya habari kutilia mkazo suala hilo ambalo litawasaidia sana  watoto kama walivyoweza kufanikiwa kuelimisha kupitia kipindi cha Tutu.

Amesema, Elimu hiyo haitawahusu Wanafunzi wa Skuli za Serikali tu bali itawahusu pia Wanafunzi wote  waliokuwepo na Skuli za binafsi za Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

Nae, Katibu Mtendaji Tume ya Utangazaji Zanzibar, Omar Said, amesema ni jukumu la vyombo vya habari kuhakikisha vinatekeleza maagizo yote yanayotolewa na Serikali na kuviomba hivyo kuhakikisha vinatekeleza jukumu hilo kwa upendo na uzalendo katika kulitumikia Taifa lao katika kipindi hiki kwa kufuata sheria na kanuni zikizopo.

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzi ya Amali Zanzibar, imeunda kamati ya Kitaifa ya kushughulikia namna ya kutoa Elimu kwa Wanafunzi katika kipindi hiki cha mripuko wa Maradhi ya Korona COVID 19 hapa nchini.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.