Habari za Punde

Waumini wa Dini ya Kiislam Wamepaswa Kutathimini Kwa Kina Baada ya Kumalizika Kwa Mfungo wa Mwezi wa Ramadhani

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Kushoto akisalimiana na Viongozi wa Dini pamoja na Serikali wa Wilaya ya Kaskazini B alipofika katika Msikiti wa Ijumaa wa Kiombamvua kwa ajili ya Ibada ya Sala ya Iddi El Fitri.
Balozi Seif pamoja na Waumini mbali mbali wakifuatilia Hotuba ya Iddi El Fitri iliyotolewa na Sheikh Ahmed Ashkina Ali hayupo pichani kwenye Msikiti wa Ijumwa wa Kiombamvua.
Waumini mbali mbali wa Kiombamvua na Vitongoji vyake wakiwa makini kufuatilia Hotuba ya sala ya Iddi El Fitri iliyotolewa na Sheikh Ahmed Ashkina Ali hayupo pichani kwenye Msikiti wa Ijumaa wa Kiombamvua.
Balozi Seif Ali Iddi akiagana na baadhi ya Viongozi wa Dini na Serikali ya Wilaya ya Kaskazini “B”  baada ya kutekeleza Ibara ya Sala ya Iddi El Fitri hapo Msikiti wa Ijumaa wa Kiombamvua.
Picha na – OMPR – ZNZ.
Na.Othman Khamis.OMPR.
Waumini wa Dini ya Kiislamu Nchini wanapaswa kufanya tathmini ya kina baada ya kumalizika kwa mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan ili utekelezaji wa ibada zinazowajibikia katika safari yao ya ucha Mungu isiwe na dosari wala wasi wasi wa nafsi.
Kauli hiyo imetolewa na Sheikh Ahmed Ashkina Ali wakati akitoa Hutba ya Ibada ya Sala ya Iddi El Fitri mbele ya Waumini wa Dini ya Kiislamu akiwemo pia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi iliyofanyika katika Msikiti wa Ijumaa wa Kiomba Mvua Wilaya ya Kaskazini “B”.
Sheikh Ahmed Ashkina Ali alisema Mwezi Mtukufu wa Ramadhan lazima uwe kigezo kizuri cha kuendelezwa katika miezi mengine inayofuata kwa vile kimeshibisha Waumini kupata chakula ikiwemo usomaji wa kitabu Kitukufu cha Quran kitendo kilichokwenda sambamba na masuala ya utoaji wa sadaka.
Alisema ucha Mungu wa moyo umekuwa ukisisitizwa kuwemo ndani ya vifua vya Waumini utakaowawezesha kufikia daraja ya juu inayomsafishia njia Muumini kuwa na maisha mema kwenye safari yake ya milele.
Sheikh Ahmed Ashkina Ali aliwaeleza Waumini hao wa Dini ya Kiislamu kwamba Iddi zote mbili, ile ya Fitri na Hajj ni siku Maalum zilizowekwa na Mwenyezi Muungu kwa lengo la kuwapa furaha na bashasha Waja wale bila ya kujali fukara, Maskini au Tajiri baada ya kukamilisha Ibada zao.
Hata hivyo Sheikh Ashkina alisema Iddi hizo zina mnasaba Maalum unaowapa Waja kutafakari uwezo wa Muumba wao ambao unawajibisha kutekeleza vyema na kwa dhati Ibada zao za kumcha Muumba huyo.
“ Iddi El Fitri hufanyika baada ya kumalizika kwa Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan wakati Iddi El Hajj inafanyika baada ya kumalizika kwa Masiku Kumi bora ndani ya Mfunguo Tatu”. Alisisitiza Sheikh Ashkina.
Akigusia ugonjwa wa Homa Kali, Kukohowa pamoja na kupumua kwa tabu kunakosababishwa na Virusi vya Corona Sheikh Ahmed Ashkina Ali aliwakumbusha Waumini pamoja na Wananchi kwa jumla kuendelea kuchukuwa tahadhari kubwa ya kujikinga na Maradhi hayo.
Alisema mitihani ya maradhi ya kuambukiza ambayo ni rehema kwa Wacha Mungu imewahi kuwakumba pia Waumini mbali mbali waliopita na wakati huo tahadhari zilichukuliwa ikiwa ni pamoja na kuwekwa kwa Karantini ya kutoingia au kutoka kwenye eneo lilioathirika na Maambukizi husika.
Alibainisha kwamba maamuzi hayo yalifanywa na Viongozi wa Dini na Tawala zilizopita kwa kuzingatia umuhimu wa kuwaepusha Waumini kuambukizwa na maradhi mapya ambayo yangewaletea usumbufu wa kutoendelea na Ibada na Maisha yao ya kila siku.
Sala ya Iddi El Fitri zimefanyika katika Misiki mbali mbali ya Ijumaa katika utaratibu wa kuzingatia Kinga dhidi ya Marasdhi ya Corona iliyopelekea kusitishwa kwa Sala ya Iddi Kitaifa pamoja na Baraza la Iddi kwa Mwaka huu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.