Habari za Punde

ZEC Itawapatia Wapiga Kura Vitambu;lisho Vipya Vya Kupigia Kura Zanzibar.

Na JaalaMakame Haji-ZEC
Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar itawapatia vitambulisho vipya vya kupigia kura Wapiga Kura wote walioandikishwa na kuhakikiwa taarifa zao katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ambavyo vitawawezesha kushiriki kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

Mkurugenzi wa Uchaguzi Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ZEC Ndg.Thabit Idarous Faina alitoa kauli hiyo baada ya kutembelea vituo vya Uandikishaji vya Wilaya ya Mjini kwa lengo la kuangalia mwenendo wa utoaji huduma kwa wananchi wanaofika vituoni kwa ajili ya kuandikishwa na kuhakikiwa taarifa zao.

Mkurugenzi Faina alisema kukamilika kwa zoezi la uandikishaji kwa mara ya pili ni hatua ambayo itaifanya Tume kuweka wazi Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kabla ya ugawaji wa Vitambulisho vipya vya kupigia Kura.

Mkurugenzi wa Uchaguzi alisema Tume imepata mafanikio makubwa ya kukamilisha zoezi la uandikishaji kutokana ushirikiano walioupata kutoka kwa vyombo vya ulinzi na usalama, viongozi wa vyama vya siasa na Serikali pamoja na wananchi wote wa Zanzibar kuwa tayari na kushiriki katika zoezi hilo.

Nao wananchi waliofika katika vituo vya uandikishaji waliipongeza Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kwa kuweka utaratibu mzuri wa uandikishaji katika vituo vya uandikishaji na kuwaomba viongozi wa Tume hiyo kuendelea kuwawekea mazingira mazuri katika hatua zote za uchaguzi ili uchaguzi huo ufanyike kwa uhuru na uwazi.

Wananchi hao waliomba Tume kuendelea kuwaandalia mazingira mazuri ambayo yatawawezesha kushiriki katika uchaguzi Mkuu bila usumbufu wowote na kuwataka wananchi wenzao kutodharau fursa wanazopatiwa na viongozi wao katika majimbo ya Uchaguzi.

Kazi ya Uandikishaji na uhakiki wa taarifa za Wapiga Kura kwa mara ya pili iliyofanyika kwa kuwapa fursa ya kuandikishwa na kuhakikiwa taarifa zao wananchi waliokosa huduma hizo kwa mara ya kwanza imeanza tarehe 30/5/2020 katika Mkoa wa Kaskazini Pemba na imekamilika leo tarehe 12/6/2020 katika Wilaya ya Mjini.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.