Habari za Punde

Balozi Seif afika nyumbani kwa Rais Mstaafu Benjamin Mkapa kuhani


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akitia saini kitabu cha Maombolezo kufuatia Kifo cha Rais wa Awamu ya Tatu Tanzania Mzee Benjamin William Mkapa Nyumbani kwa Marehemu Mtaa wa Masaki Jijini Dar es salaam.
Balozi Seif na Mkewe Mama Asha Suleiman Iddi wakimfariji na kumpa pole Mke wa Rais Mstaafu wa Tanzania Mama Anna Mkapa Nyumbani kwake Masaki Mjini Dar es salaam.

Picha na – OMPR – ZNZ.


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba watendaji wa Umma waliojikubalisha kuingia katika Fani ya Diplomasia ni vyema wakazingatia kusoma Kitabu cha Rais wa Awamu ya Tatu ya Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Bendjamin William Mkapa ili kufanikisha malengo yao katikia Fani yao.

Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati akizungumza na Vyombo mbali mbali vya Habari Nchini mara baada ya kuweka saini Kitabu cha maombezo kufuatia Kifo cha Ghafla cha Rais Mstaafu WA Awamu ya Tatu Mzee Bendjamin William Mkapa na kumpa pole Mkewe Mama Ana Mkapa hapo Nyumbani kwao Mtaa wa Masaki Jijini Dar es salaam.

Alisema Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania imepata sifa kubwa katika masuala ya Kidiplomasia kufuatia Mchango mkubwa uliotolewa na Marehemu Mzee Bendjamin William Mkapa wakati akiwa Waziri wa Mambo ya Nje  na Ushirikiano wa Kimataifa wa Tanzania na baadae kushika wadhifa wa Urais wa Awamu ya Tatu.

Balozi Seif aliwaeleza Wanahabari hao kwamba Mzee Mkapa alikuwa ni Kiongozi Muadilifu, Mcheshi aliyekuwa akizingatia Hekima na busara zilizomuongoza kuwa muungwana kwa kutoa Elimu kwa Watu wote waliokuwa karibu naye.

“ Mimi nimemfahamu Mzee Mkapa wakati akiwa Mwanadiplomasia wa Tananzia wakati nikiwa Afisa wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Tanzania na baadae Balozi Kamili. Hapo ndipo nilipojuwa na kufahamu umahiri wake katika Kazi Mzee Mkapa”. Alisisitiza Balozi Seif.

Akimpa pole Mke wa Marehemu Mzee Mkapa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohamed Shein, Viongozi, Wananchi wa Zanzibar na yeye binafsi wamepokea kwa mshtuko kifo hicho cha Mzee Mkapa usiku wa kuamkia  Ijumaa.

Alisema Watanzania, Familia, Marafiki na hata Viongozi walimpenda sana Kiongozi huyo mkongwe katika pia Fani ya Habari kutokana na mchango wake mkubwa kwa Jamii lakini Mwenyezi Muungu alimpenda zaidi.

Balozi Seif aliwataka wafiwa na jamaa wa karibu wa Marehemu kuwa na moyo wa subra katika kipindi hichi kigumu cha msiba na huku wakielewa kwamba msiba huo ni wa Watanzania wote.

Mzee Bendjamin William Mkapa alizaliwa mnamo Tarehe  12 Novemba Mwaka 1938 na kushika nafasi ya Urais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kuanzia Mwaka 1995 hadi 2005.

Mrehemu Mzee Mkapa  aliyehitimu Shahada ya Chuo Kikuu cha Makerere Nchini Uganda ameacha kizuka Mmoja na Watoto Wawili.

Mwenyezi Muungu ailaze roho ya Marehemu Mzee Mkapa  mahali pema Amin.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.