RAIS
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein,
akiitikia dua ya kumuombea Marehemu Mzee Haji Nassib Haji Nyanya na (kushoto
kwa Rais) Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mwanamwema Shein na Wanafamilia
wakiitikia dua, alipofika kutowa mkono wa pole kwa Familia ya marehemu nyumbani
kwake Bububu kwa Nyanya
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, ametoa mkono wa pole kwa familia ya
Marehemu Mzee Haji Nasibu Haji Nyanya aliyefariki dunia alfajiri ya kuamkia Jumamosi
ya Julai 11, 2020 huko Jijini Dodoma.
Rais Dk. Shein alifika nyumbani kwa marehemu haji Nasibu Nyanya
mara tu baada ya kurejea Jijini Dodoma ambako alishiriki katika vikao mbali
mbali vya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Akiwa nyumbani kwa Marehemu Haji Nasibu Haji Nyanya huko Bububu,
Rais Dk. Shein aliwapa mkono wa pole wanafamilia wote akiwemo mjane wa Marehemu
Bi Zainab Nyanya na kuwataka kuwa na subira katika kipindi hichi kigumu cha
msiba.
Rais Dk. Shein akiwa amefuatana na Mama Mwanamwema Shein aliitaka
familia hiyo kumuombea dua Marehemu Haji Nasibu Haji Nyanya ambaye alikuwa ni
mwanasiasa mkongwe na mfanyabiashara wa muda mrefu.
Katika salamu zake hizo za pole, Rais Dk. Shein alieleza jinsi
alivyoguswa na kifo cha Mzee Nyanya ambacho kilitokea huko Jijini Dodoma na
kueleza jinsi walivyokuwa pamoja na Marehemu kabla ya kumfika umauti.
Nayo familia ya Mzee Nyanya ilitoa shukurani kwa Rais Dk. Shein
kwa kushirikiana nao bega kwa bega katika msiba huo yeye pamoja na Mama Shein ikiwa
ni pamoja na kwenda kuwapa mkono wa pole mara tu baada ya kurudi safari.
Marehemu Mzee Nyanya atakumbukwa katika harakati mbali mbali za
kisiasa, kiuchumi na kijamii hapa nchini ambapo mnamo Januari 8 mwaka huu 2020 Rais Dk. Shein
alimtunuku Nishani ya Mapinduzi kwa Viongozi na Wananchi Wenye Sifa Maalum huko
katika viwanja vya Ikulu Jijini Zanzibar.
Marehemu ameacha mjane, mtoto mmoja na wajukuu wanne,
MwenyeziMungu ailaze roho yake mahala pema peponi, Amin.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024
2231822
E-mail:
rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment