Habari za Punde

WATUMISHI WATAKIWA KUWEKA MALENGO YA USAJILI WA WATOTO

Na Hamida Kamchalla, TANGA.
WATUMISHI wa Serikali ngazi za Mkoa na Wailaya wametakiwa kuweka malengo mahususi katika kutekeleza na kufikia lengo la kusajili watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano kwa asilimia 100 ndani ya miezi mitatu.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga Bi.Jufica Omari alitoa wito huo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga Ndg.Martin Shigela wakati kwenye kikao cha hamasa kuhusu usajili wa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano kwa viongozi wa mkoa na wilaya kilichofanyika katika ukumbi wa jengo la mkuu wa mkoa Tanga.

Alisema kuwa pamoja na majukumu waliyonayo pia inawapasa kufanikisha utekelezaji wa mpango huo na ni lazima kuhakikisha wanaweka maazimio mahususi ambayo yatakuwa dira ya kufikia lengo la kusajili watoto wenye sifa hizo.

"Tafadhali viongozi wenzangu kuanzia sasa tukatumie fursa mbalimbali zilizopo kuhamasisha wananchi kupitia njia mbalimbali, nafahamu tuna majukumu mengi hasa kwa kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu na pia kusimamia wananchi katika majukumu ya uzalishaji mali lakini pia niwaombe jambo hili liwe kipaumbele katika ratiba zenu kutokana na umuhimu wake kwa Taifa" alisema.

Alisisitiza kwamba watumishi hususani wa halmashauri wajipange katika utekelezaji, usimamizi na ufuatiliaji kwani serikali inangiza fedha za utekelezaji ndani ya halmashauri zao hivyo wana jukumu la kuhakikisha matumizi sahihi ya rasilimali fedha na vifaa vitakavyotolewa katika utekelezaji wa mpango huo.

"Kwa niaba ya mkuu wa mkoa huu naunga mkono mpango huo, tafadhali sana RITA msisite kunishirikisha mara mtakapohitaji msaada wowote ulio ndani ya uwezo wa mkoa, napenda kuwaahidi RITA na wadau wengine wa maendeleo kwamba kama mpango huo umefanikiwa katika mikoa mingine na sisi itawezekana tena kwa kishindo" alisema.

Kwa upande wake Kaimu Kabidhi Wasii Mkuu wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhibiti Emmy Hudson alisema kuwa mpango huo ni endelevu na utatekelezwa katika vipindi viwili tofauti ambapo pia kutakuwa na maboresho ya usajili kwa njia ya tekinolojia (TEHAMA).

Hudson alibainisha kwamba mpango huo hauna ubaguzi na una umuhimu wa kipekee kwa kuwa unazingatia misingi ya haki na ulinzi wa mtoto, usawa kwa watoto wote ambao wanasajiliwa bila kujali jinsia, hali ya kipato kwa familia au makazi wanayotoka. 

"Kila mtoto aliye na sifa stahiki ni lazima asajiliwe na ndio maana serikali imeondoa ada ya cheti kupitia mpango huo ili kuwezesha kila mtoto kunufaika bila kujali jinsia, hali ya familia anayotoka pamoja na eneo la makazi yaani mjini au vijijini" alisema Hudson.

Hata hivyo aliwashukuru wadau wa maendeleo ambao wanashirikiana na serikali katika utekelezaji wa mpango huo huku akiwataja wadau hao kuwa ni Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto Duniani (UNICEF), Serikali ya Canada kupitia Idara ya mambo ya nje, Biashara na Maendeleo (DFATD) na Kampuni ya aimu za mkononi (TIGO). 

Alifafanua kwamba RITA imezindua mfumo wa usajili kwa njia ya mtandao unaojulikana kama E-Huduma ambapo wananchi anaweza kujaza na kutuma maombi yake popote alipo na mpaka sasa wananchi mia sita wamekwisha hudumiwa kupitia mfumo huo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.