Habari za Punde

ZEC kugawa vitambulisho Wilaya zote za Unguja kuanzia tarehe 25 Julai

 Watendaji ambao wameteuliwa kusimamia kazi hiyo katika vituo vya Unguja wakiwasikiliza kwa makini viongozi wa ZEC 


Na Jaala Makame Haji-- ZEC

Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ZEC itagawa vitambulisho vya Kupigia Kura tarehe 25 na 26/7/2020 kwa Wilaya zote za Unguja baada ya kukamilika ugawaji huo katika Wilaya za Pemba wiki iliyopita.

Mkurugenzi wa Uchaguzi ZEC THABIT IDAROUS FAINA wakati akizungumza na watendaji ambao wameteuliwa kusimamia kazi hiyo katika vituo vya Unguja alisema, Tume imeandaa utaratibu maalum ambao utarahisha zoezi hilo kufanyika kwa urahisi zaidi.

Mkurugenzi Faina, aliwataka watendaji walioteuliwa kutoa elimu kwa wapiga kura ya kutumia huduma ya mtandao wa Zantel ambayo itawawezesha Wapiga Kura wanaokwenda kuchukua vitambulisho vyao kupata huduma hiyo kwa haraka Zaidi na bila ya usumbufu wa aina yeyote.

Kwa kutumia mtandao wa Zantel unaweza kupiga *152*29# ili kujua kibox ambacho kipo kitambulisho chako cha kupigia kura

Ndugu Faina alisisitiza kuwa, malengo ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ni kuendesha Uchaguzi mkuu ambao utazingatia misingi ya haki, uhuru na uwazi

Mkuu wa kurugenzi ya Elimu ya Wapiga Kura, Habari na Mawasiliano kwa Umma Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar JUMA SANIFU SHEHA aliwataka watendaji hao huifanya kazi hiyo kwa uadilifu, uaminifu na umakini wa hali ya juu ili kusaidia kuondosha malalamiko baina yao.

Naye Msimamizi wa Uchaguzi Wilaya ya Mjini SAFIA IDDI MUHAMMAD na Msimamizi wa Uchaguzi Wilaya ya Magharibi “B” FATMA GHARIB HAJI, kwa wakati tofauti waliasa watendaji kutumia lugha nzuri wakati wanapokuwa vituoni kutoa huduma pamoja na kuzingatia sera ya jinsia na ushirikishwa wa makundi ya kijamii ya mwaka 2014 iliyoanzishwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ambayo inawaelekeza Tume kuwapata fursa watu wenye mahitaji maalum.

Watendaji walioteulia kusimamia ugawaji wa Vitambulisho katika Vituo vilivyotumika kuandikisha Wapiga kura kwa kazi ya uandikishaji iliyopita wamepongeza utaratibu uliowekwa na Tume katika kutoa huduma vituoni  ambayo itawapa urahisi wa kufanya kazi hiyo.

Mafunzo hayo yametolewa kwa watendaji wote wa Wilaya za Unguja walioteuliwa kusimamia kazi ya ugawaji wa vitambulisho vya Wapiga Kura.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.