Kamishna wa Idara ya Uendelezaji
Sekta ya Fedha wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Charles Mwamwaja akiwakaribisha
wageni katika mafunzo ya Sera, Sheria na Kanuni za Huduma Ndogo za Fedha kwa
watendaji wa Taasisi za Umma, Fedha na Program za Serikali, yaliyofanyika mjini
Morogoro kushoto ni Kamishna Msaidizi wa Idara hiyo, Bi. Dionisia Mjema.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya
Sera, Sheria na Kanuni za Huduma Ndogo za Fedha kwa watendaji wa Taasisi za
Umma, Fedha na Program za Serikali, wakifuatilia kwa makini mada mbalimbali
zilizowasilishwa wakati wa mafunzo hayo, yaliyofanyika mjini Morogoro.
Kamishina wa Idara ya Uendelezaji
wa Sekta ya Fedha wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Charles Mwamwaja akiwa katika
picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo ya Sera, Sheria na Kanuni za Huduma
Ndogo za Fedha kwa watendaji wa Taasisi za Umma, Fedha na Program za Serikali,
iliyofanyika mjini Morogoro, kushoto ni Naibu Kamishna wa Idara hiyo Bi. Mameltha
Mtagwaba, Kulia ni Afisa Mkuu wa Idara ya Usimamizi wa Sekta Ndogo ya Fedha
kutoka BoT, Bw. Deogratius Mnyamani na wapili kulia ni Kamishna Msaidizi wa Idara
ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Dionisia
Mjema.
Na Farida Ramadhani, Morogoro
Serikali imeeleza kuwa utekelezaji wa Sheria ya Huduma
Ndogo za Fedha hauna lengo la kuua biashara ya huduma ndogo za fedha nchini
bali unalenga kuendeleza na kuboresha usimamizi na udhibiti wa Sekta Ndogo ya
Fedha ili kuwa na Sekta ya Fedha imara katika ukuaji uchumi na kupunguza umaskini.
Haya yameelezwa na Kamishna wa Idara ya Uendelezaji wa
Sekta ya Fedha kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Charles Mwamwaja wakati
wa mafunzo ya Sera, Sheria na Kanuni za Huduma Ndogo za Fedha kwa baadhi ya watendaji
wa Taasisi za Umma,Fedha na program za Serikali yaliyofanyika mjini Morogoro.
Dkt. Mwamwaja alisema kuwa ni vema baadhi ya watu
wakaacha upotoshaji ambao unawatia hofu kuhusu Sheria hiyo kwa kuwa utekelezaji
wake utasaidia kutatua changamoto mbalimbali zilizoathiri Sekta ya Fedha kwa
kuweka miongozo ya usimamizi na utaratibu wa kumlinda mtumiaji wa huduma ndogo
za fedha ambao ni takribani asilimia 55.3 ya nguvu kazi ya Taifa.
“Sheria hii imetoa muongozo wa shughuli zinazotakiwa
kufanywa na watoa huduma ndogo za fedha, namna ya kuendasha biashara ya huduma
hizo pamoja na haki za msingi za watumiaji ili kuwawezesha watumiaji kupata faida
ambayo itakuza uchumi wa nchi”, alifafanua Dkt. Mwamwaja.
Wawasilishaji katika mafunzo hayo walitoa maelezo ya
kina kuhusu taratibu za usajili na uombaji wa leseni kulingana na daraja husika
kwa mujibu wa Sheria na kuwatoa hofu wananchi kuwa taritibu hizo ni rafiki na
wananchi wote wanaweza kuzifuata na kutekeleza matakwa ya kisheria.
Mwanasheria kutoka Ofisi ya Rais TaAMISEMI, Bi.
Antelma Mtemahanji ni miongoni mwa wawezeshaji hao ambae ameeleza kuwa Vikundi
vya Kijamii vya Huduma Ndogo za Fedha vinatakiwa kusajiliwa katika Mamlaka za
Serikali za Mitaa ambapo vinatakiwa kuwa na fomu ya maombi ya usajili, katiba
iliyosainiwa na wanachama wote, muhtasari wa mkutano wa uazishwaji pamoja na
barua ya utambulisho kutoka Kata, Mtaa au Kijiji ili viweze kusajiliwa.
Kwa upande wa washiriki wa mafunzo hayo waliipongeza
Serikali kwa kutoa mafunzo hayo ambayo kwa kiasi kikubwa yatarahisisha zoezi la
usajili na ukataji leseni hususan katika kipindi hiki kidogo kilicho bakia kabla
ya muda wa kipindi cha mpito kuisha ifikapo tarehe 31 Oktoba, 2020.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji
Wananchi Kiuchumi, Bi. Beng’i Issa ni miongoni mwa washiriki wa mafunzo hayo
ambaya ameeleza kuwa utekelezaji wa Sheria hiyo utarahisisha zoezi la kupata
takwimu sahihi ya wananchi hususani wa kwenye vikundi vya kijamii vya huduma
ndogo za fedha kwa ajili ya kuviwezesha.
No comments:
Post a Comment