Habari za Punde

DAS- Vijana wa Jinsia Zote Wapatiwe Elimu ya Hedhi Salama ili Kumuweka Huru Kijana wa Kike.

Na Hamida Kamchalla, TANGA.
VIJANA wa kike na wa kiume wametakiwa kupatiwa elimu kuhusu hedhi salama baina yao kwa lengo la kumpa uelewa mtoto wa kiume ili kuweza kutoa msaada pindi atakapomuona mtoto wa kike ametokewa na hali hiyo kwa dharura.

Katibu Tawala wa wilaya ya Tanga Faidha Salim alitoa wito huo juzi wakati akifungua semina ya kuhamasisha halmashauri kuwa na muongozo wa sheria ndogo ndogo na mpango na bajeti kuhusu taulo za kike kwa watoto mashuleni mkoani Tanga ilioandaliwa na
Asasi isiyokuwa ya Kiserikali (NGO’s) ya Shdepha.

Alisema kuwa ni muhimu wavulana na wasichana wakapatiwa elimu ya
pamoja kwani itamjengea kujiamini pale linapotokea tatizo kwakuwa ikitokea bahati mbaya amechafuka hatapata aibu hata siku akiwa hana vazi maalumu (Padi).

Salim alisema kuwa elimu hiyo pia itawasaidia wavulana kuweza kuona namna inavyokuwa na inapoanza na endapo ikitokea tatizo watajua jinsi gani wamsaidie msichana akiwa kwenye hali hiyo.

"Nitoe msisitizo kwenye jambo moja, ni vizuri itolewe elimu ya pamoja baina ya wasichana na wavulana kuhusu hedhi salama ili msichana atakapoweza kupata
tatizo akichafuka hata ona aibu na wote watajua ni jambo la
kawaida” alisema.

Alibainisha kwamba kipindi cha zamani mambo yalikuwa tofauti lakini hivi sasa kila siku watu
wanabadilika kutokana na utandawazi na pia mbali na msaada ambao utatoka kwenye
Halmshauri baada ya kutenga bajeti ni vizuri kuwafunidsha watoto
kutengeneza padi zao ambazo zitawasaidia kwa muda mrefu.

“Yaani anapotoka nyumbani kama ana padi ya kitambaa ya kufua, mbali na kutenga bajeti za halmashauri ni vizuri kuwafundisha watoto wenyewe kutengeneza padi
zao ambazo zitatumika kwa muda mrefu kabla ya wakurugenzi kuwa na bajeti ya kuendesha semina ya kuwafundisha walimu au wakina mama namna ya kutengeneza padi hizo” alieleza.

Awali akizungumza katika semina hiyo Mkurugenzi wa Asasi ya SHDEPHA Mariam Kamote alisema Asasi hiyo imefanikiwa kutekeleza miradi mingi ukiwemo wa kutokomoza ajira kwa mtoto uliokuwa chini ya Wekeza na mradi wa kupima makundi maalumu ikiwemo wanaofanya ngono
jinsia moja watu waliohatari zaidi kwenye migodi.

Kamote alifafanua kwamba pia waliingia kwenye afya ya jamii ikiwemo kutoa elimu ya afya ya uzazi kwa watoto wa kiume na wa kike ambao ulipelekea wao kuweza kuandika andiko kuhusu taulo za
watoto wa kike kuomba ufadhili kupitia AmplifyChange.

Aidha alisema wakati wanatekeleza afya ya uzazi waligundua mtoto wa
shule wa kike anashindwa kuhudhuria masomo ipasavyo kutokana na kwamba anapoingia kwenye siku zake anakosa vitendea kazi ambavyo vitamsaidia kujikinga na kuhudhruia masomo yake.

Hata hivyo alisema kilichowasukuma kuandika andiko la mradi huo ni kugundua kwamba asilimia kubwa ya watoto wa kike wanashindwa kuhudhuri masomo pindi wanapoingia kwenye siku zao jambo linalosababisha wengi wao kufeli kwani muda wanapokaa nyumbani wenzao wanakuwa wakiendelea na masomo nawao kupitwa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.