Habari za Punde

Serikali Haitamvumilia Mtu au Kikundi Kitakachoashiria Uvunjaji wa Amani ya Nchi.


Na.Othman Khamis.OMPR. 

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameonya kwamba Serikali haitamvumilia Mtu au Kikundi chochote kitakachoashiria kuhusika na uvunjifu wa Amani ya Nchi hasa kipindi hichi kinachoendelea na harakati za Kampeni, wakati za Uchaguzi na baada ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi.

Balozi Seif Ali Iddi alitoa onyo hilo wakati akimfariji na kumpa pole Msanii Mkongwe wa Muziki wa Tarab Nchini Khamis Nyange Makame maarufu Profesa Gogo aliyelazwa katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja akipatiwa huduma za matibabu baada ya kushambuliwa kwa mapanga alfajiri ya Jumatatu.

Profesa Gogo na wenzake Watatu walishambuliwa kwa Mapanga wakiwa kwenye Ibada ya Sala ya Alfajiri Kijijini kwao Kangagani Wete Pemba na kukimbizwa Hospitali kwa huduma ya kwanza na baadae kusafirishwa katika Hospitali ya Rufaa Mnazi Mmoja.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema inasikitisha kuona kwamba Jamii nzima ikiongozwa na Viongozi wa Dini wamekuwa katika Ibada mbali mbali za kuliombea Taifa kuendelea kuwa na Amani wakati wote lakini bado wapo baadhi ya Watu wanadiriki kuichezea Amani hiyo jambo ambalo Serikali haitakuwa tayari kuona inachezewa.

“ Jamii yote imejikita kudumisha Amani hasa Viongozi wa Dini wakiwa mstari wa mbele katika jambo hilo lakini wapo watu wanajaribu kuichezea Amani hiyo ambayo ni tunu ya Taifa”. Alisisitiza Balozi Seif.

Aliwatoa hofu Wananchi wote kwamba Uchaguzi Mkuu wa Mwezi Oktoba Mwaka huu utafanyika kwa Amani na kila mwenye haki ya kuchaguliwa atapata fursa hiyo muhimu kwa maendeleo na ustawi wa Taifa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.